Homa kwa watu wazima

NaLarry M. Bush, MD, FACP, Charles E. Schmidt College of Medicine, Florida Atlantic University;
Maria T. Vazquez-Pertejo, MD, FACP, Wellington Regional Medical Center
Imekaguliwa naBrenda L. Tesini, MD, University of Rochester School of Medicine and Dentistry
Imepitiwa/Imerekebishwa Jul 2024 | Imebadilishwa Jul 2025
v1587928_sw

Homa ni ongezeko la joto la mwili linalotokea wakati kipimajoto cha mwili (kilichopo kwenye hypothalamus kwenye ubongo) kinapojiweka upya kwa halijoto ya juu, hasa kutokana na maambukizi. Joto la mwili lililoongezeka ambalo halisababishwi na kuweka upya alama iliyowekwa ya joto huitwa hyperthermia.

Ingawa nyuzijoto 98.6° F (37° C) inachukuliwa kuwa halijoto ya kawaida, halijoto ya mwili hutofautiana siku nzima. Huwa chini kabisa asubuhi na mapema na juu zaidi alasiri—wakati mwingine hufikia nyuzijoto 99.9° F (37.7° C). Vilevile, homa haibaki kwenye halijoto isiyobadilika. Wakati mwingine halijoto huongezeka kila siku na kisha hurudi katika hali ya kawaida. Hali hii huitwa homa ya vipindi. Vinginevyo, halijoto hutofautiana lakini hairudi katika hali ya kawaida. Hali hii huitwa homa ya kusalia juu. Madaktari hawafikirii tena kwamba mtindo wa kupanda na kushuka kwa homa ni muhimu sana katika utambuzi wa magonjwa fulani.

Joto la mwili linaweza kupimwa katika maeneo kadhaa ya mwili. Maeneo yaliyozoeleka sana ni mdomo (joto la mdomo) na rektamu (joto la rektamu). Maeneo mengine ni pamoja na sikio, paji la uso, na mara chace sana, kwapa. Joto hupimwa kwa kutumia kipimajoto cha dijitali. Vipimajoto vya kioo vilivyo na zebaki havipendekezwi kwa sababu vinaweza kuvunjika na kuwaweka watu katika hatari ya kupata zebaki.

Joto la mdomo huchukuliwa kuwa juu wakati

  • Likiwa juu zaidi ya nyuzijoto 99° F (37° C) asubuhi na mapema.

  • Joto ni zaidi ya nyuzijoto 38°C (100.4°F) wakati wowote baada ya asubuhi na mapema.

  • Ni juu kuliko halijoto ya kawaida ya kila siku inayojulikana kwa mtu.

Halijoto ya rektamu na sikio ni takriban nyuzijoto 0.6°C (1.0°F) juu zaidi kuliko joto la mdomo.

Halijoto ya ngozi (kwa mfano, paji la uso) ni takriban nyuzijoto 0.6°C (1.0°F) chini zaidi ya joto la mdomo.

Watu wengi hutumia neno "homa" kwa jumla, mara nyingi wakimaanisha kwamba wanahisi joto kupita kiasi, baridi sana, au kutokwa na jasho, lakini hawajapima halijoto yao.

Uwezo wa kusababisha homa hupungua kwa watu fulani (kwa mfano, wale ambao ni wazee sana, wadogo sana, au ambao wana tatizo la matumizi ya pombe).

(Angalia pia Muhtasari wa Magonjwa ya Kuambukiza na Homa kwa Watoto Wachanga na Watoto Wakubwa.)

Matokeo ya homa

Dalili ambazo watu wanazo husababishwa zaidi na hali inayosababisha homa badala ya homa yenyewe.

Ingawa watu wengi wana wasiwasi kwamba homa inaweza kusababisha madhara, ongezeko la joto la mwili kwa muda mfupi kuanzia nyuzi joto 100.4° hadi 104° F (38° hadi 40° C) linalosababishwa na maambukizi mengi ya muda mfupi (ya papo hapo) huvumiliwa vyema na watu wazima wenye afya njema. Kama mojawapo ya kinga za mwili dhidi ya maambukizi, homa inaweza kusababisha uzalishaji wa kingamwili na kufanya iwe vigumu zaidi kwa vijiumbe kukua, na inaweza kupunguza ukali wa maambukizi na kusaidia kutoweka.

Hata hivyo, homa ya wastani inaweza kuwa hatari kidogo kwa watu wazima wenye ugonjwa wa moyo au mapafu kwa sababu homa husababisha mapigo ya moyo na kiwango cha kupumua kuongezeka. Homa inaweza pia kusababisha hali ya kiakili kuwa mbaya zaidi kwa watu wenye shida ya akili.

Zaidi ya hayo, ongezeko kubwa la halijoto (kawaida zaidi ya nyuzijoto 105.8°F, au 41°C) huweza kuwa na madhara. Joto la mwili la juu kiasi hiki linaweza kusababisha hitilafu na hatimaye kushindwa kwa viungo vingi kufanya kazi. Ongezeko hilo kubwa wakati mwingine husababishwa na maambukizi makali sana (kama vile sepsis, malaria au homa ya uti wa mgongo) lakini kwa kawaida husababishwa na kiharusi cha joto au matumizi ya dawa fulani haramu (kama vile kokeini au PCP).

Homa kwa watoto wenye afya njema inaweza kusababisha kifafa.

Sababu za Homa kwa Watu Wazima

Vitu vinavyosababisha homa huitwa pyrogens. Pyrogens zinaweza kutoka ndani au nje ya mwili. Vijiumbe na vitu ambavyo huzalisha (kama vile sumu) ni mifano ya pyrogens zinazoundwa nje ya mwili. Pyrogens zinazoundwa ndani ya mwili kwa kawaida huzalishwa na aina mbili za seli nyeupe za damu zinazoitwa monocytes na macrophages. Pyrogens kutoka nje ya mwili zinaweza kusababisha homa kwa kuchochea mwili kutoa pyrogens zake au kwa kuathiri moja kwa moja eneo la ubongo linalodhibiti halijoto.

Matatizo mengi yanaweza kusababisha homa. Kwa ujumla zimeainishwa kama

  • Za kuambukiza (inajulikana zaidi)

  • Neoplastic (saratani)

  • Za uvimbe (ikiwa ni pamoja na ugonjwa wa kingamwili kwenda kinyume na mwilii, athari za mzio, na baadhi ya athari za dawa)

Chanzo cha kuambukiza kina uwezekano mkubwa kwa watu wazima wenye homa inayodumu kwa siku 4 au chini ya hapo (inayoitwa homa ya muda mfupi). Homa ya muda mfupi kwa watu wenye saratani au ugonjwa unaojulikana wa uvimbe pia ina uwezekano mkubwa wa kuwa na chanzo cha kuambukiza. Kwa watu wenye afya njema, homa ya muda mfupi haitakuwa ishara ya kwanza ya ugonjwa sugu. Sababu isiyoambukiza ina uwezekano mkubwa wa kusababisha homa ambayo hudumu kwa muda mrefu au kujirudia.

Sababu za maambukizi

Maambukizi ndiyo sababu kuu za homa. Maambukizi yanaweza kusababishwa na bakteria, virusi, au kuvu. Karibu maambukizi yote yanaweza kusababisha homa, lakini, kwa ujumla, sababu zinazowezekana zaidi za kuambukiza ni zifuatazo:

Maambukizi mengi ya muda mfupi ya njia ya upumuaji na njia ya utumbo ni ya virusi.

Sababu za neoplastiki

Saratani nyingi husababisha homa, kwa mfano, leukemia, limfoma na saratani ya figo.

Sababu za kuvimba

Matatizo ya uvimbe yanayosababisha homa ni pamoja na matatizo ya kimfumo ya homa ya baridi yabisi kama vile baridi yabisi ya rheumatoid, lupus erythematosus ya kimfumo (lupus), na arteritis ya seli kubwa.

Homa inaweza pia kutokea kutokana na athari ya mzio.

Dawa wakati mwingine husababisha homa. Kwa mfano, viuavijasumu za beta-lactam (kama vile penicillin) na dawa za salfa zinaweza kusababisha homa. Baadhi ya dawa haramu za kulevya (kama vile kokeini, amfetamini au fensiklidini) na dawa kama vile dawa za ganzi na dawa za kuzuia magonjwa ya akili huweza kusababisha joto la juu sana.

Viashiria vya hatari

Mambo fulani huwasaidia madaktari kubaini ni nini chanzo kikubwa cha homa kwa mtu. Vigezo hivi vinajumuisha vifuatavyo:

  • Hali ya afya ya mtu, umri, na kazi yake

  • Kulazwa hospitalini

  • Matumizi ya dawa fulani au dawa haramu

  • Kuwa katika hatari ya kuambukizwa (kwa mfano, kupitia usafiri au kugusana na watu, wanyama, au wadudu walioambukizwa)

Jedwali

Tathmini ya Homa kwa Watu wazima

Kwa kawaida, daktari anaweza kubaini kuwa kuna maambukizi kulingana na historia fupi, uchunguzi wa kimwili, na wakati mwingine vipimo vichache rahisi, kama vile eksrei ya kifua na vipimo vya mkojo. Hata hivyo, wakati mwingine chanzo cha homa hakitambuliki kwa urahisi.

Madaktari wanapowapima watu wenye homa kali mwanzoni, huzingatia masuala mawili ya jumla:

  • Kutambua dalili zingine kama vile maumivu ya kichwa au kikohozi: Dalili hizi husaidia kupunguza idadi ya visababishi vinavyowezekana.

  • Kuamua kama mtu huyo ni mgonjwa sana au mgonjwa sugu: Maambukizi mengi ya muda mfupi ya virusi yanayoweza kutokea hupotea yenyewe na pia ni vigumu kwa madaktari kutambua (yaani, kubaini haswa ni virusi gani vinavyosababisha maambukizi). Kupunguza upimaji kwa watu ambao ni wagonjwa sana au sugu kunaweza kusaidia kuepuka uchunguzi mwingi wa gharama kubwa, usio wa lazima, na mara nyingi usio na matokeo.

Ishara za onyo

Kwa watu wenye homa kali, dalili na sifa fulani husababisha wasiwasi. Zinajumuisha

  • Mabadiliko katika utendaji wa akili, kama vile kuchanganyikiwa

  • Maumivu ya kichwa, shingo iliyokaza, au vyote

  • Madoa mekundu bapa, madogo, ya zambarau kwenye ngozi (petechiae), ambayo yanaonyesha kutokwa na damu chini ya ngozi

  • Shinikizo la chini la damu

  • Mapigo ya moyo ya haraka au kupumua kwa kasi

  • Kuishiwa na pumzi

  • Halijoto ambayo ni ya juu zaidi ya nyuzijoto 40°C (104°F) au chini zaidi ya nyuzijoto 95°F (35°C)

  • Safari ya hivi karibuni kwenda kwenye maeneo ambapo ugonjwa mbaya wa kuambukiza, kama vile malaria unapatikana kwa wingi

  • Matumizi ya hivi karibuni ya dawa zinazodhoofisha mfumo wa kinga (dawa za kudhoofisha kinga mwilini)

Wakati wa kuona daktari

Watu ambao wana dalili zozote za tahadhari wanapaswa kumuona daktari mara moja. Watu kama hao kwa kawaida huhitaji kupimwa mara moja na mara nyingi hulazwa hospitalini.

Watu wasio na dalili za tahadhari wanapaswa kumpigia simu daktari ikiwa homa inadumu kwa zaidi ya saa 24 hadi 48. Kulingana na umri wa mtu huyo, dalili zingine, na hali za kiafya zinazojulikana, daktari anaweza kumwomba mtu huyo kwenda kwa ajili ya uchunguzi au kupendekeza matibabu nyumbani. Kwa kawaida, watu wanapaswa kumuona daktari ikiwa homa inadumu kwa zaidi ya siku 3 au 4 bila kujali dalili zingine.

Anachofanya daktari

Madaktari huuliza maswali kwanza kuhusu dalili za mtu huyo na historia ya matibabu. Kisha madaktari hufanya uchunguzi wa kimwili. Wanachokipata wakati wa historia na uchunguzi wa kimwili mara nyingi huashiria chanzo cha homa na vipimo ambavyo vinaweza kuhitaji kufanywa.

Daktari huanza kwa kumuuliza mtu kuhusu dalili na matatizo ya sasa na ya awali, dawa anazotumia kwa sasa, upokeaji wa damu wowote, kuathiriwa na maambukizi, usafiri wa hivi karibuni, chanjo, na kulazwa hospitalini hivi karibuni, upasuaji, au taratibu zingine za kimatibabu. Mtindo wa homa mara chache humsaidia daktari kufanya utambuzi. Hata hivyo, homa inayorudi kila baada ya siku mbili au kila baada ya siku tatu ni kawaida kwa malaria. Madaktari wanazingatia malaria na maambukizi mengine yanayoambukizwa na wadudu kama chanzo kinachowezekana tu ikiwa watu wamesafiri hadi eneo ambalo maambukizi ni ya kawaida.

Safari za hivi karibuni zinaweza kumpa daktari dokezo kuhusu chanzo cha homa kwa sababu baadhi ya maambukizi hutokea katika maeneo fulani. Kwa mfano, coccidioidomycosis (maambukizi ya kuvu) hutokea zaidi kusini-magharibi mwa Marekani.

Kuwa katika hatari ya kuambukizwa hivi karibuni pia ni muhimu. Kwa mfano, watu wanaofanya kazi katika kiwanda cha kufungasha nyama wana uwezekano mkubwa wa kupata bruselosisi (maambukizi ya bakteria yanayoenea kupitia kugusana na wanyama wa kufugwa). Mifano mingine ni pamoja na maji au chakula kisicho salama (kama vile maziwa na bidhaa za maziwa ambazo hazijaoondolewa vijijdudu, na nyama mbichi au isiyopikwa vizuri), wadudu (kama vile mbu) na kuumwa na kupe, ngono isiyo salama, na kuathiriwa na shughuli za kazi au burudani (kama vile uwindaji, matembezi marefu, na spoti za majini).

Maumivu ni kidokezo muhimu cha chanzo kinachowezekana cha homa, kwa hivyo daktari huuliza kuhusu maumivu yoyote masikioni, kichwani, shingoni, kwenye meno, kooni, kifuani, tumboni, ubavuni, kwenye rektamu, kwenye misuli na viungo.

Dalili zingine zinazosaidia kubaini chanzo cha homa ni pamoja na kujaa kwa kamasi puani na/au kutokwa na kamasi, kikohozi, kuharisha, na dalili za mkojo (kwenda haja mara kwa mara, uharaka, na maumivu wakati wa kukojoa). Kujua kama mtu huyo ana vinundu vya limfu vilivyopanuka au upele (ikiwa ni pamoja na jinsi unavyoonekana, mahali ulipo, na wakati ulipoonekana kuhusiana na dalili zingine) kunaweza kumsaidia daktari kubaini chanzo. Watu wenye homa zinazojirudia, kutokwa na jasho usiku, na kupunguza uzito wanaweza kuwa na maambukizi sugu kama vile kifua kikuu au endokadaitisi (maambukizi ya utando wa moyo na kwa kawaida vali za moyo).

Daktari anaweza pia kuuliza kuhusu yafuatayo:

Uchunguzi wa kimwili huanza na uthibitisho wa homa. Homa huamuliwa kwa usahihi zaidi kwa kupima joto la rektamu, lakini joto la mdomo au sikio mara nyingi hupimwa. Joto la paji la uso si sahihi kama la rektamu, lakini madaktari wanaweza kupima joto la paji la uso ili kuwachunguza watu ikiwa wana homa. Halijoto ya kwapa haitoi majibu sahihi sana, kwa hivyo madaktari mara chache huitumia kuthibitisha homa. Kisha madaktari hufanya uchunguzi wa kina kuanzia kichwani hadi miguuni ili kuangalia chanzo cha maambukizi au ushahidi wa ugonjwa.

Kupima

Uhitaji wa kupima hutegemea kile ambacho daktari anakipata wakati wa historia ya matibabu na uchunguzi wa kimwili.

Vinginevyo, watu wenye afya njema ambao wana homa kali na dalili za jumla zisizo wazi (kwa mfano, wanahisi wagonjwa kwa ujumla au maumivu) huenda wana ugonjwa wa virusi ambao utatoweka bila matibabu. Kwa hiyo, kwa kawaida hawahitaji kupimwa. Hali za kipekee ni watu walio katika eneo ambalo COVID-19 inaenezwa, watu ambao wamekuwa katika hatari ya kuathiriwa na mnyama au mdudu anayebeba na kueneza ugonjwa maalum (anayeitwa mwenezaji), kama vile watu walioumwa na kupe, na watu ambao hivi karibuni wamekuwa katika eneo ambalo ugonjwa fulani (kama vile malaria) ni wa kawaida.

Ikiwa vinginevyo watu wenye afya njema wana matokeo yanayoashiria ugonjwa fulani, upimaji unaweza kuhitajika. Madaktari huchagua vipimo kulingana na matokeo hayo. Kwa mfano, ikiwa watu wana maumivu ya kichwa na shingo yenye mkazo, uchukuaji wa majimajia ya uti wa mgongo (kutobolewa kwa kiuno) hufanywa ili kuangalia homa ya uti wa mgongo. Ikiwa watu wana kikohozi na msongamano wa mapafu, eksrei ya kifua hufanywa ili kubaini nimonia. Kwa magonjwa fulani ya kupumua, kama vile COVID-19 au mafua, kuna vipimo vya haraka vya molekuli ambavyo vinaweza kutoa matokeo ndani ya dakika chache au saa chache. Baadhi ya vipimo vya haraka vinaweza kufanywa nyumbani au katika ofisi ya daktari kwa kutumia sampuli iliyopatikana kwa kutumia usufi wa pamba. Vipimo vingine vya haraka ili kubaini chanzo maalum cha maambukizi vinahitaji sampuli ya damu kutumwa kwenye maabara.

Watu walio katika hatari kubwa ya kuambukizwa, watu wanaoonekana kuwa wagonjwa sana, na wazee mara nyingi wanahitaji kupimwa hata wakati ambapo matokeo hayaashirii ugonjwa fulani. Kwa watu kama hao, madaktari wanaweza kufanya yafuatayo:

  • Kipimo kamili cha vipengele vya damu (ikiwa ni pamoja na idadi na uwiano wa aina tofauti za seli nyeupe za damu)

  • Ukuzaji wa bakteria wa mkojo na damu

  • Eksirei ya kifua

  • Uchambuzi wa mkojo

Kipimo cha Maabara

Kuongezeka kwa idadi ya seli nyeupe za damu kwa kawaida huashiria maambukizi. Uwiano wa aina tofauti za seli nyeupe za damu (utofauti wa idadi) hutoa vidokezo zaidi. Kwa mfano, ongezeko la neutrophils linaashiria maambukizi mapya ya bakteria. Ongezeko la eosinophils linaashiria uwepo wa vimelea, kama vile minyoo ya tegu au minyoo ya mviringo.

Pia, damu, mkojo, na majimaji mengine ya mwili yanaweza kutumwa kwenye maabara ili kujaribu kukuza vijiumbe katika ukuzaji wa bakteria kwenye maabara. Vipimo vingine vya damu vinaweza kutumika kugundua kingamwili dhidi ya vijiumbe maalum.

Homa ya asilia isiyojulikana (FUO)

Homa isiyojulikana chanzo chake inaweza kugunduliwa wakati

  • Watu wana homa ya angalau nyuzijoto 101° F (38.3°C) kwa wiki kadhaa.

  • Uchunguzi wa kina haugundui sababu.

Katika hali kama hizo, chanzo kinaweza kuwa maambukizi sugu yasiyo ya kawaida (kama vile kifua kikuu, maambukizi ya bakteria wa moyo, maambukizi ya VVU, cytomegalovirus au virusi vya Epstein-Barr) au kitu kingine isipokuwa maambukizi, kama vile homa ya baridi yabisi ya kimfumo (kama vile lupus au baridi yabisi ya rheumatoid) au saratani (kama vile limfoma, saratani ya ovari au leukemia). Sababu zingine ni pamoja na dawa au athari za dawa haramu, kuganda kwa damu (kuganda damu kwenye mshipa mkubwa), uvimbe wa tishu za viungo (sakoidosisi), na ugonjwa wa uvimbe wa utumbo.

Kwa wazee, sababu za kawaida za FUO ni arteritis ya seli kubwa, limfoma, majipu, na kifua kikuu.

Madaktari kwa kawaida hufanya vipimo vya damu, ikiwemo kiwango kamili cha damu, hali ya damu, vipimo vya damu ya ini, na vipimo vya kuangalia matatizo ya mfumo wa baridi yabisi. Vipimo vingine, kama vile eksrei ya kifua, uchunguzi wa mkojo, na ukuzaji wa bakteria wa mkojo, vinaweza kufanywa.

Kipimo cha Maabara

Uchunguzi wa picha ya mawimbi ya sauti, tomografia iliyokokotolewa (CT) au upigaji picha kwa mwangwi wa sumaku (MRI), hasa maeneo yanayosababisha usumbufu, zinaweza kumsaidia daktari kutambua chanzo. Uchanganuzi wa radionuclide, hufanyika baada ya seli nyeupe za damu zilizowekwa alama mionzi kudungwa kwenye mshipa, au tomografia ya utoaji wa posititroni (PET) inaweza kutumika kutambua maeneo ya maambukizi au uvimbe.

Ikiwa matokeo haya ya kipimo ni hasi, madaktari wanaweza kuhitaji kuchukua sampuli ya tishu kutoka kwenye ini, uboho, au sehemu nyingine inayoshukiwa kuwa na maambukizi kwa ajili ya uchukuaji wa tishu kwa uchunguzi. Sampuli huchunguzwa kwa darubini, hukuzwa na kuchambuliwa.

Matibabu ya FUO yanalenga kutibu ugonjwa unaosababisha homa ikiwa unajulikana. Madaktari wanaweza kutoa dawa za kupunguza joto la mwili (angalia matibabu ya homa).

Matibabu ya Homa kwa Watu wazima

Matibabu bora ya homa ni kutibu kisababishi chake.

Kwa sababu homa husaidia mwili kujikinga dhidi ya maambukizi na kwa sababu homa yenyewe si hatari (isipokuwa ikiwa inazidi takriban nyuzijoto 106° F [41° C), kuna mjadala kuhusu kama homa inapaswa kutibiwa mara kwa mara. Hata hivyo, watu wenye homa kali kwa ujumla huhisi vizuri zaidi homa inapotibiwa. Aidha, watu wenye ugonjwa wa moyo au mapafu na wale walio na shida ya akili wanazingatiwa kuwa katika hatari kubwa ya kupata matatizo hatarishi, kwa hivyo wanapokuwa na homa, wanapaswa kutibiwa.

Dawa zinazotumika kupunguza joto la mwili huitwa antipyretics.

Dawa za antipyretics zenye ufanisi zaidi na zinazotumika sana ni acetaminophen na dawa zisizo za steroidi za kuzuia uvimbe (NSAIDs), kama vile aspirini, ibuprofen na naproxen. Dawa hizi hutumiwa kulingana na maelekezo yaliyotolewa kwenye lebo ya chombo.

Kwa sababu dawa nyingi za homa au mafua zinayouzwa bila agizo la daktari zina acetaminophen, watu lazima wawe waangalifu wasitumie acetaminophen na moja au zaidi ya dawa hizi za mafua au homa kwa wakati mmoja.

Hatua zingine za kupoza (kama vile kupoza kwa kutumia ukungu wa maji ya vuguvugu na kutumia blanketi za kupoza) zinahitajika tu ikiwa halijoto ni takriban 106° F (41.1° C) au zaidi.

Watu hawapaswi kupaka kileo cha kusugua kwenye ngozi zao kwa kitambaa cha kuoshea au sponji kwa sababu kileo kinaweza kufyonzwa kupitia ngozi na kinaweza kuwa na madhara.

Watu walio na maambukizi ya damu (bakteremia) au ambao wana dalili zisizo za kawaida (kama vile shinikizo la chini la damu na mapigo ya moyo na kiwango cha kupumua cha haraka) hulazwa hospitalini.

Mahitaji muhimu kwa Wazee: Homa

Homa inaweza kuwa sumbufu kwa wazee kwa sababu mwili huenda usikabiliane kama vile unavyofanya kwa vijana. Kwa mfano, kwa wazee dhaifu, maambukizi hayasababishi homa kwa urahisi. Hata ikiongezeka kutokana na maambukizi, halijoto inaweza kuwa chini zaidi kuchukuliwa kwa kawaida kuwa homa, na kiwango cha homa kinaweza kisilingane na ukali wa ugonjwa. Vilevile, dalili nyingine, kama vile maumivu, zinaweza kuwa hazionekani sana. Mara nyingi, mabadiliko katika utendakazi wa akili au kupungua kwa utendakazi wa kila siku ndio ishara nyingine pekee ya awali ya nimonia au maambukizi ya njia ya mkojo.

Hata hivyo, wazee wenye homa wana uwezekano mkubwa wa kuwa na maambukizi makali ya bakteria kuliko vijana wenye homa. Kama ilivyo kwa watu wazima wadogo, sababu yake kwa kawaida ni maambukizi ya njia ya upumuaji au njia ya mkojo. Maambukizi ya ngozi na tishu laini pia ni sababu za kawaida za homa kwa wazee. Watu wazima wana uwezekano mkubwa wa kuwa na dalili mbaya za maambukizi ya virusi vya kupumua kama vile mafua, COVID-19 na virusi vinavyosababisha nimonia (RSV).

Utambuzi wa homa kwa wazee ni sawa na ule wa vijana, isipokuwa kwamba kwa wazee, madaktari kwa kawaida hupendekeza vipimo vya mkojo (ikiwa ni pamoja na ukuzaji wa bakteria kwenye maabara) na eksrei ya kifua. Sampuli za damu hukuzwa kwenye maabara ili kufutilia mbali maambukizi ya damu (bacteremia).

Mambo Muhimu

  • Homa nyingi kwa watu wenye afya njema husababishwa na maambukizi ya njia ya upumuaji au utumbo kutokana na virusi.

  • Ikiwa watu wenye homa wana ishara za tahadhari, wanapaswa kumuona daktari mara moja.

  • Kwa kawaida madaktari wanaweza kutambua maambukizi kwa kutegemea historia fupi ya kimatibabu, uchunguzi wa kimwili, na wakati mwingine vipimo vichache rahisi, na kisha madaktari hutumia matokeo haya, hasa dalili, kubaini ni vipimo vipi vingine vinavyohitajika.

  • Madaktari huzingatia magonjwa sugu yaliyopo, hasa yale yanayodhoofisha mfumo wa kinga, kama chanzo kinachowezekana cha homa inayodumu kwa muda mrefu.

  • Kutumia dawa za acetaminophen au NSAID kwa kawaida hupunguza homa na kwa kawaida huwafanya watu wajisikie vizuri, ingawa kwa watu wengi, matibabu si muhimu.

  • Kwa watu wazima, maambukizi hayasababishi homa kwa urahisi, na dalili zingine zinaweza kuwa hazionekani sana.