Kuvuja Damu Ukeni Wakati wa Ujauzito wa Mapema

NaEmily E. Bunce, MD, Wake Forest School of Medicine;
Robert P. Heine, MD, Wake Forest School of Medicine
Imekaguliwa naSusan L. Hendrix, DO, Michigan State University College of Osteopathic Medicine
Imepitiwa/Imerekebishwa Jul 2023 | Imebadilishwa Jun 2024
v1536153_sw

Katika wiki 20 za kwanza za ujauzito, asilimia 20 hadi 30 ya wanawake hutokwa na damu ukeni. Kwa wengi wa wanawake hawa, huwa kuna tatizo la ujauzito, lakini baadhi ya wanawake hutokwa na damu kidogo au madoa ya damu na kuwa na ujauzito wa kawaida na wenye afya njema. Kwa takriban nusu ya wanawake wanaovuja damu, ujauzito huisha kwa kuharibika kwa mimba. Ikiwa mimba haitaharibika mara moja, kuna uwezekano wa matatizo kutokea baadaye katika ujauzito. Kwa mfano, uzito wa mtoto wa kuzaliwa nao unaweza kuwa mdogo, ujauzito unaweza kusababisha mtoto kuzaliwa akiwa ameshakufa (kifo cha kijusi baada ya wiki 20 za ujauzito), au mtoto anaweza kuzaliwa mapema (kuzaliwa kabla ya wakati) au kufa wakati wa kuzaliwa au muda mfupi baada ya kuzaliwa. Ikiwa kuna kutokwa na damu nyingi, shinikizo la damu linaweza kuwa chini sana, na kusababisha mshtuko. Hata hivyo, wanawake wengi wanaotokwa na damu kidogo katika ujauzito wa mapema huendelea na kuwa na ujauzito wenye afya na kujifungua vyema.

Kiwango cha kutokwa na damu kinaweza kuwa madoa madogo ya damu au kutokwa na damu nyingi. Kutoa damu nyingi ni jambo la kutia wasiwasi, lakini kutokwa na damu kidogo sana au kutokwa na damu kiasi kunaweza pia kuonyesha ugonjwa mbaya. Wanawake wanaotokwa na damu yoyote ukeni wanapaswa kuwasiliana na daktari wao.

Sababu za Kuvuja Damu Ukeni Wakati wa Ujauzito wa Mapema

Kutokwa na damu ukeni wakati wa ujauzito wa mapema kunaweza kusababishwa na matatizo ambayo yanahusiana na ujauzito (uzazi) au yasiyohusiana (tazama jedwali la ).

Visababishi vya kawaida zaidi vya kutokwa na damu wakati wa ujauzito wa mapema ni

Kutokwa na damu ukeni kunaweza kumaanisha kwamba mimba inaweza kuharibika, lakini wakati mwingine damu hukoma kutoka na ujauzito huendelea bila matatizo yoyote. Mimba inapoharibika, kwa kawaida hutokea katika hatua chache. Kwanza, kuna kutokwa na damu. Kisha maumivu ya tumbo huanza, ambayo huenda yakawa makali na damu inaweza kuwa nzito. Kisha mwanamke hupitisha ujauzito na anaweza kuona tishu za ujauzito zikitoka nje ya uke.

Wakati mwingine, kuharibika kwa mimba hakusababishi dalili zozote na hugunduliwa wakati kijusi kinapopimwa wakati wa ziara ya kawaida ya kimatibabu (hali inayoitwa utoaji mimba usiotambulka). Iwapo mwanamke anashuku kuwa ana mimba iliyoharibika, anapaswa kuwasiliana na daktari wake. Wakati mwingine wanawake wanaweza kupata kuharibika kwa mimba wakiwa nyumbani, lakini iwapo maumivu au kutokwa na damu kumekithiri, au ikiwa tishu za ujauzito hazijatoka kabisa, wanahitaji matibabu kwa dawa au utaratibu ili kuhakikisha kuwa wako salama na ujauzito unatoka kabisa.

Mabaki yaliyo kwenye uterasi yanaweza kuwa yameambukizwa hapo awali, wakati wa kuharibika kwa mimba au baadaye (hali inayoitwa sepsisi ya kuharibika mimba).

Kisababishi hatari zaidi cha kutokwa na damu wakati wa ujauzito wa mapema ni

  • Ujauzito ulio kwenye sehemu isiyo ya kawaida (mimba ya nje ya uterasi)—ile ambayo haiko katika nafasi yake ya kawaida kwenye uterasi—kwa mfano, ile iliyo kwenye mrija wa falopio

Ujauzito wa nje ya kizazi ni wa kutishia maisha. Mimba iliyopandikizwa nje ya uterasi haitakua kwa njia ya kawaida. Kadri mimba inavyokua kwenye mrija wa falopio au sehemu nyingine ya mwili (kama vile ovari, seviksi, au kovu la zamani la upasuaji kwenye uterasi au tumbo), inaweza kusababisha sehemu hiyo kupasuka. Hii husababisha maumivu makali na kuvuja damu nyingi, ambayo inaweza kusababisha madhara makubwa au hata kifo kwa mwanamke mjamzito. Wakati ujauzito wa nje ya kizazi inapogunduliwa, matibabu ni kumaliza ujauzito kwa dawa au kuiondoa kwa upasuaji.

Sababu nyingine ambayo inaweza kuwa hatari lakini isiyo ya kawaida ni kupasuka kwa uvimbe wa kopasi luteamu. Baada ya yai kutolewa kutoka kwenye ovari, muundo uliolitoa (kopasi luteamu) unaweza kujaa umajimaji au damu badala ya kuvunjika na kutoweka kama kawaida.

Viashiria vya hatari

Kwa kuharibika mimba, sababu za hatari ni pamoja na zifuatazo:

  • Umri wa zaidi ya miaka 35

  • Kuharibika mimba mara moja au zaidi katika mimba zilizopita

  • Uvutaji sigara

  • Matumizi ya dawa za kulevya haramu, kama vile kokeini, au kwa uwezekano wa mihadarati mingine, kama vile pombe

  • Matatizo katika uterasi, kama vile fibroma (fibroid), kovu, au umbo lisilo la kawaida la uterasi

Kwa mimba ya nje ya uterasi, viashiria vya hatari ni pamoja na:

  • Ujauzito wa nje ya kizazi wa awali (hali ya hatari ile muhimu zaidi)

  • Upasuaji wa awali wa tumbo, hasa upasuaji wa uzuiaji wa kudumu wa kushika mimba (kufunga mirija ya uzazi)

  • Matatizo ya mirija ya falopio

  • Matumizi ya sasa ya intrauterine device (IUD)

  • Matumizi ya mbinu za utungishaji mimba kwenye maabara ili kupata mimba ya sasa

Sababu zingine hatarishi kwa mimba ya nje ya uterasi ni pamoja na historia ya maambukizi ya ngono au ugonjwa wa kuchochewa kwa fupanyonga, matumizi ya sasa ya vidonge vya kupanga uzazi vya estrojeni/projestini, uvutaji sigara, utasa, mimba kwa awali au kutoa mimba kimakusudikutoa mimba.

Tathimini ya Kuvuja Damu Ukeni Wakati wa Ujauzito wa Mapema

Madaktari kwanza huamua iwapo chanzo cha kutokwa na damu ukeni ni mimba ya nje ya uterasi.

Ishara za onyo

Kwa wanawake wajawazito wanaotokwa na damu ukeni, dalili zifuatazo husababisha wasiwasi:

  • Kuzimia, kizunguzungu, au mapigo ya moyo ya haraka—dalili zinazoashiria shinikizo la chini sana la damu

  • Kupoteza kiasi kikubwa cha damu au damu iliyo na tishu au vipande vikubwa vya damu iliyoganda

  • Maumivu makali ya tumbo ambayo huzidi mwanamke anaposogea au kubadilisha mikao

  • Homa, baridi, na kutokwa na uchafu ukeni ambao una usaha uliochanganyika na damu

Wakati wa kuona daktari

Wanawake wenye dalili za hatari wanapaswa kumuona daktari mara moja.

Wanawake wasio na dalili za hatari wanapaswa kumuona daktari ndani ya saa 48 hadi 72.

Anachofanya daktari

Madaktari huuliza kuhusu dalili na historia ya matibabu (ikiwa ni pamoja na mimba za awali, kuharibika kwa mimba, utoaji mimba, na viashiria vya hatari za mimba ya nje ya uterasi na kuharibika kwa mimba). Kisha madaktari hufanya uchunguzi wa kimwili. Kile wanachopata wakati wa historia na uchunguzi wa kimwili mara nyingi huonyesha kisababishi na vipimo ambavyo vinaweza kuhitajika (tazama jedwali la ).

Madaktari wanauliza kuhusu kuvuja damu:

  • Kiwango chake (kwa mfano, ni pedi ngapi zinazotumika au kuloweka ndani ya saa moja)

  • Ikiwa madonge au tishu zilitoka

  • Ikiwa maumivu yanaambatana na kutokwa na damu

Ikiwa mwanamke ana maumivu pamoja na kutokwa na damu ukeni, madaktari huuliza ni lini na jinsi gani yalianza, hutokea wakati gani, hudumu kwa muda gani, iwapo ni makali au hafifu, na ikiwa ni ya kudumu au huja na kutoweka.

Wakati wa uchunguzi wa kimwili, madaktari huangalia kwanza homa na dalili za upotezaji mkubwa wa damu, kama vile mapigo ya moyo ya haraka na shinikizo la chini la damu. Kisha hufanya uchunguzi wa fupanyonga, wakichunguza iwapo njia ya kizazi (sehemu ya chini ya uterasi) imeanza kufunguka (kupanuka), jambo ambalo linaweza kuruhusu mimba kupita. Ikiwa tishu yoyote (labda kutokana na kuharibika kwa mimba) itagunduliwa, huondolewa na kupelekwa kwenye maabara ili kuchunguzwa.

Madaktari pia hufinya tumbo polepole ili kuona iwapo ni laini inapofinywa.

Jedwali
Jedwali

Kupima

Wakati wa uchunguzi, madaktari wanaweza kutumia kifaa cha Doppler ultrasound, kinachowekwa kwenye tumbo ya mwanamke, ili kuchunguza mapigo ya moyo katika kijusi.

Iwapo kipimo cha ujauzito cha nyumbani kinaonyesha ujauzito lakini ujauzito haujathibitishwa na mtaalamu wa afya, madaktari hufanya kipimo cha ujauzito kwa kutumia sampuli ya mkojo.

Mara tu ujauzito unapothibitishwa, vipimo kadhaa hufanywa:

  • Aina ya damu na hali ya Rh (chanya au hasi)

  • Kwa kawaida atrasonografia

  • Kipimo cha damu ili kupima homoni (human chorionic gonadotropin, au hCG) inayotengenezwa na kondo la nyuma wakati wa ujauzito wa mapema.

Hali ya Rh hubainishwa kwa sababu mwanamke mjamzito mwenye damu hasi ya Rh lazima atibiwe na globulini ya kinga ya Rho(D) iwapo anatokwa na damu yoyote ya uke. Matibabu huhitajiika ili kumzuia kutoa kingamwili ambazo zinaweza kushambulia seli nyekundu za damu za kijusi katika ujauzito unaofuata (tazama Kutolingana kwa Rh).

Ikiwa damu nyingi inatoka (zaidi ya kikombe), madaktari pia hufanya hesabu kamili ya seli za damu (CBC) au vipimo vingine ili kuangalia iwapo kuna tatizo na uwezo wa damu kuganda kawaida au iwapo kuongezewa damu kutahitajika.

Kwa kawaida, uchunguzi wa ultrasonografia hufanywa kwa kutumia kifaa cha ultrasound kinachoingizwa ndani ya uke. Ultrasonografia inaweza kugundua ujauzito kwenye uterasi na inaweza kugundua mapigo ya moyo baada ya takriban wiki 6 za ujauzito. Ikiwa hakuna mapigo ya moyo yanayogunduliwa baada ya wakati huu, kuharibika kwa mimba hutambuliwa. Ikiwa mapigo ya moyo yatagunduliwa, uwezekano wa kuharibika kwa mimba ni mdogo sana lakini bado unaweza kutokea.

Ultrasonografia pia inaweza kusaidia kutambua yafuatayo:

Kupima viwango vya hCG husaidia madaktari kutafsiri matokeo ya ultrasonografia na kutofautisha mimba ya kawaida na mimba ya nje ya uterasi. Ikiwa kuna wasiwasi kuwa mwanamke ana mimba ya nje ya uterasi, viwango vya hCG hupimwa mara kwa mara na uchunguzi wa ultrasonografia hurudiwa panapohitajika.

Mimba iliyopasuka ya nje ya uterasi ni dharura. Ikiwa uwezekano wa mimba ya nje ya uterasi kupasuka ni wa wastani au wa juu, huenda madaktari wakahitaji kufanya upasuaji. Katika hali zinazohatarisha maisha, wanaweza kuhitaji kufanya upasuaji wa dharura hata kabla ya kufanya vipimo vya damu au ultrasonografia. Kwa kawaida, madaktari hufanya mkato mdogo chini ya kitovu na kuingiza mrija wa kutazama uterasi na sehemu zilizo karibu (laparoskopu) na hivyo kuamua iwapo kuna mimba ya nje ya uterasi. Wakati mwingine huwa wanafanya mkato mkubwa katika sehemu ya chini ya tumbo (laparatomi).

Matibabu ya Kuvuja Damu Ukeni Wakati wa Ujauzito wa Mapema

Ingawa madaktari kwa kawaida hupendekeza kupumzika kitandani wakati mimba inaonekana kuwa na uwezekano wa kuharibika, hakuna ushahidi kwamba kupumzika kitandani husaidia kuzuia mimba kuharibika. Kujiepusha na ngono hushauriwa, ingawa ngono haijahusishwa kabisa na uharibikaji wa mimba.

Ikiwa damu nyingi inatoka, ikiwa mshtuko utatokea, au ikiwa kuna uwezekano wa mimba kupasuka nje ya uterasi, mojawapo ya mambo ya kwanza ambayo madaktari hufanya ni kuweka katheta kubwa kwenye mshipa ili mhusika aweze kuongezewa damu haraka kupitia mishipa. Upasuaji hufanywa mara moja wakati mimba ya nje ya uterasi imepasuka

Kutokwa na damu kunapotokana na ugonjwa maalum, ugonjwa huo hutibiwa, ikiwezekana.

Mambo Muhimu

  • Visababishi vya kawaida zaidi vya kutokwa na damu wakati wa ujauzito wa mapema ni kuharibika kwa mimba.

  • Kisababishi hatari zaidi cha kutokwa na damu ukeni ni mimba ya nje ya uterasi.

  • Mwanamke mjamzito anapaswa kumuona daktari mara moja ikiwa ana mapigo ya moyo ya haraka, anazimia, au anahisi kisulisuli.

  • Vipimo vya damu ili kubaini iwapo damu ina Rh hasi au Rh chanya hufanyika kwa kuwa iwapo mwanamke mjamzito aliye na damu yenye Rh hasi anatokwa na damu ukeni, lazima apewe immune globulini ya Rho(D) ili kumzuia kutoa kingamwili ambazo zinaweza kushambulia seli nyekundu za damu za kijusi katika ujauzito unaofuata.