Mtoto kuzaliwa akiwa amekufa ni kifo cha kijusi katika wiki 20 za ujauzito au baadaye (au baada ya wiki 28 katika baadhi ya ufafanuzi).
Kuzaliwa mfu kunaweza kusababishwa na tatizo katika mwanamke, kondo la nyuma au kijusi.
Madaktari hufanya vipimo vya damu ili kujaribu kubaini chanzo cha kuzaliwa mtoto akiwa amekufa.
Ikiwa kijusi kilichokufa hakitatoka, mwanamke anaweza kupewa dawa za kusaidia uterasi kutoa yaliyomo ndani yake, au yaliyomo yataondolewa kwa upasuaji kwa kupanua na kuondoa.
Kuzaliwa mtoto mfu, kwa ufafanuzi, kunahusisha kifo cha kijusi. Nchini Marekani, kuzaliwa mtoto mfu hufafanuliwa kama kifo cha kijusi kabla au wakati wa kuzaliwa katika wiki 20 za ujauzito au baadaye. Shirika la Afya Duniani linafafanua kuzaliwa kwa mtoto ambaye amekufa kama kifo cha kijusi baada ya wiki 28. Kuna karibu watoto milioni 2 wanaozaliwa wakiwa wamekufa duniani kote kila mwaka. Kuzaliwa kwa mtoto akiwa amekufa hapo awali huongeza hatari ya kifo cha kijusi katika ujauzito unaofuata.
Ikiwa kijusi kitakufa wakati wa ujauzito wa muhula wa mwisho au karibu na wakati wake wa kuzaliwa lakini kinabaki ndani ya uterasi kwa wiki kadhaa, mwanamke anaweza kupata ugonjwa wa kuganda kwa damu unaoweza kusababisha kuvuja damu nyingi (unaoitwa kuganda kwa damu kunakosambaa ndani ya mishipa ya mwili).
Sababu za Kuzaliwa Mfu
Kuzaliwa mfu kunaweza kusababishwa na tatizo katika mwanamke, kondo la nyuma au kijusi. Wakati mwingine kinachosababisha kuzaliwa kwa mtoto akiwa amekufa hakijulikani.
Kijusi kinaweza kufa wakati wanawake wana matatizo fulani, kama vile
Preklampsia (aina ya shinikizo la juu la damu linalotokea wakati wa ujauzito) au eklampsia
Majeraha
Matatizo ya kuganda kwa damu kama vile ugonjwa wa antiphospholipid
Kisukari ambacho hakijadhibitiwa vizuri
Udhibiti usiofaa ugonjwa wa tezi ya dundumio
Unene kupita kiasi sana (kiashiria cha uwiano kati ya kimo na uzani wa mwili [BMI] cha 40 au zaidi)
Matumizi ya dawa za kulevya, kama vile kokeini, pombe au tumbaku
Matatizo na kondo la nyuma yanaweza pia kusababisha kifo cha kijusi. Matatizo haya yanaweza kujumuisha yafuatayo:
Kutenguka kwa kondo la nyuma (wakati kondo la nyuma linapotengana na ukuta wa uterasi mapema sana)
Kuingia kwa damu ya kijusi kwenye damu ya mama
Kiungamwana kilichotokeza kwanza (wakati kiungamwana kinapotoka ukeni kabla ya mtoto kuzaliwa)
Matatizo ya kiungamwana (kama vile kutokeza kwanza au fundo la kiungamwana)
Tatizo la kondo ya uzazi kufunga njia ya kutokea mtoto (wakati utando wenye mishipa ya damu inayounganisha kiungamwana na kondo la nyuma unalala kando au karibu na shingo ya shingo ya kizazi)
Hali zinazopunguza mtiririko wa damu (na hivyo oksijeni na virutubisho) kwa kijusi
Maambukizi ya utando unaozunguka kijusi (maambukizi ya ndani ya majimaji ya amniotiki)
Wakati mwingine kijusi hufa kinapokuwa na tatizo, kama vile
Anemia (seli nyekundu za damu chache sana)
Mimba yenye watoto zaidi ya mmoja (mimba ya watoto wengi)
Maambukizi
Utambuzi wa Kuzaliwa Mfu
Tathmini ya daktari
Uchunguzi wa kutambua sababu
Madaktari wanaweza kushuku kwamba kijusi kimekufa ikiwa kijusi kitaacha kusonga, ingawa kusongai mara nyingi hupungua kadri kijusi kinachokua kinavyokuwa na nafasi ndogo ya kusonga. Vipimo vya kutathmini kijusi kwa kawaida hufanywa. Vipimo hivi ni pamoja na:
Kipimo kisicho na mkazo: Mapigo ya moyo ya kijusi hufuatiliwa wakati kijusi kimelala tuli na kinaposonga. Kwa kipimo hiki, madaktari hutumia kifaa kilichoambatishwa kwenye tumbo la mwanamke.
Kipimo cha kibiolojia na kimwili: Kipimo cha ultrasonografia hutumika kutoa picha za kijusi kwa wakati halisi, na kijusi huchunguzwa. Kipimo hiki huwawezesha madaktari kutathmini kiasi cha majimaji ya amniotiki na kuangalia kijusi kwa vipindi vya kupumua kwa mdundo, mwendo, na mkazo wa misuli.
Ili kujaribu kubaini chanzo cha kuzaliwa kwa mtoto mfu, madaktari hufanya vipimo vya kijenetiki na damu (kama vile vipimo vya maambukizi, kisukari, matatizo ya tezi ya dundumio na ugonjwa wa antiphospholipid). Madaktari pia wanapendekeza kutathmini kijusi ili kutafuta visababishi vinavyoweza kutokea, kama vile maambukizi na kasoro za kromosomu. Kondo la nyuma na uterasi huchunguzwa. Mara nyingi, kisababishi hakiwezi kubainishwa.
Matibabu ya Kuzaliwa Mfu
Ikiwa inahitajika, dawa za kuondoa kijusi
Ikiwa inahitajika, taratibu za kuondoa tishu zozote zilizobaki kwenye uterasi
Usaidizi wa kihisia na ushauri nasaha
Ikiwa kijusi kilichokufa hakitatolewa, mwanamke anaweza kupewa prostaglandini (dawa inayofanana na homoni inayochochea uterasi kubana), kama vile misoprostol, ili kusababisha shingo ya kizazi kufunguka (kupanuka). Kisha kwa kawaida hupewa oxytocin, dawa inayochochea uchungu wa kujifungua, kulingana na muda wa ujauzito.
Ikiwa ujauzito ni chini ya wiki 24 au kijusi ni kidogo, upanuzi na uondoaji (D na E) unaweza kufanywa ili kuondoa kijusi kilichokufa. Kabla ya D na E, madaktari wanaweza kutumia dutu asilia zinazofyonza majimaji (kama vile mashina ya mwani) au dawa (kama vile misoprostol) kusaidia kufungua shingo ya kizazi.
Ikiwa tishu yoyote kutoka kwa kijusi au kondo la nyuma itabaki kwenye uterasi, ufyonzaji wa kuchukua tishu hufanywa ili kukiondoa. Spekulamu hutumika kupanua kuta za uke, na shingo ya kizazi hupanuka. Kisha mrija unaonyumbulika huingizwa ndani ya uterasi ili kuondoa kijusi na kondo la nyuma. Mrija huo umeunganishwa kwenye sirinji ya mkononi au mashine ya kufyonza ya umeme, ambayo hufyonza tishu yoyote iliyobaki.
Huduma ya kimwili kwa wanawake waliojifungua mtoto mfu ni sawa na ile inayotolewa kwa kawaida baada ya kujifungua mtoto (huduma ya baada ya kujifungua). Hata hivyo, usaidizi wa ziada wa kihisia na kijamii unahitajika.
Kama kuganda kwa damu kunakosambaa ndani ya mishipa ya mwili kutatokea, wanawake huongezewa damu inapohitajika.
Mabadiliko na hisia zinazotokea kwa wanawake baada ya kujifungua mtoto mfu ni sawa na zile zinazotokea baada ya kuharibika kwa mimba. Wanawake kwa kawaida huhisi huzuni kwa kufiwa na huhitaji usaidizi wa kihisia na wakati mwingine ushauri nasaha.
Ikiwa mimba ya baadaye inaweza kusababisha kuzaliwa kwa mtoto mfu inategemea chanzo.