Hali ya kichwa kidogo ni kichwa kidogo kisicho cha kawaida. Mara nyingi kichwa huwa kidogo kwa sababu ubongo ni mdogo na haukukua vizuri. Mikrosefali si hali ya kawaida.
Mikrosefali inaweza kusababishwa na matatizo mengi, ikiwa ni pamoja na hitilafu za jeni, maambukizi na kasoro za ubongo, au wakati mwingine inaweza kurithiwa katika familia.
Watoto wachanga wenye mikrosefali kali kwa kawaida huwa na dalili za uharibifu wa ubongo.
Utambuzi hufanywa kabla ya kuzaliwa kwa kufanya vipimo vya picha vinavyotumia mawimbi ya sauti au baada ya kuzaliwa kwa kupima mzingo wa kichwa.
Baada ya kuzaliwa, madaktari kwa kawaida hufanya vipimo vya picha ili kutafuta hitilafu za ubongo na wakati mwingine vipimo vya damu ili kutafuta chanzo.
Kwa sababu mikrosefali inaweza kuanzia kiasi kidogo hadi kali sana, machaguo ya matibabu yanaweza kutofautiana pia.
Uingiliaji wa mapema unaweza kusaidia sana.
Ukubwa wa kichwa kwa kawaida huamuliwa na ukubwa wa ubongo. Hivyo, kupungua kwa ukuaji wa ubongo, au sehemu ya ubongo, ndiyo chanzo cha mikrosefali. Mikrosefali inaweza kutokea peke yake au pamoja na kasoro nyingine kuu za kuzaliwa, na inaweza kuwepo wakati wa kuzaliwa au ikatokea baadaye wakati wa uchanga.
Sababu za Kichwa Kidogo cha Mtoto
Mikrosefali inaweza kusababishwa na matatizo kadhaa, ikiwa ni pamoja na:
Ukosefu wa oksijeni kabla au wakati wa kuzaliwa (birth asphyxia)
Kuhatarishwa kwa dawa za kulevya, pombe au sumu kabla ya kuzaliwa
Lishe duni kupindukia kwa mama
Kasoro fulani za kuzaliwa kwenye ubongo
Maambukizi kabla ya kuzaliwa (kama vile rubela, kirusi cha sitomegalo, toksoplasmosisi, kaswende au maambukizi ya virusi vya Zika).
Mikrosefali ya kurithi, ambapo ukubwa wa kichwa kidogo upo kwenye ukoo wa mtoto, kwa kawaida huwa ni ya kiasi kidogo na haisababishi dalili za mfumo wa neva kama vile kifafa au ulemavu wa akili.
Dalili za Kichwa Kidogo cha Mtoto
Dalili hutegemea kiwango cha uharibifu wa ubongo au jinsi ubongo ulivyoshindwa kukua vizuri.
Baadhi ya matatizo ambayo watoto wenye mikrosefali kali wanaweza kuwa nayo ni pamoja na vifafa, uchelewaji wa ukuaji, matatizo ya kulisha, matatizo ya kusikia au kuona, matatizo ya kutembea au usawa, kukosa utulivu (hyperactivity), na ulemavu wa akili.
Picha kwa hisani ya Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa, Kituo cha Kitaifa cha Kasoro za Kuzaliwa Nazo na Ulemavu.
© Springer Science+Business Media
Utambuzi wa Kichwa Kidogo cha Mtoto
Kabla ya kuzaa, ultrasound
Baada ya kuzaliwa, uchunguzi wa kimwili na vipimo vya picha hufanyika
Upimaji wa jeni
Kabla ya kujifungua, wakati mwingine utambuzi hufanywa kwa utaratibu kipimo cha ultrasound kufanyika mwishoni mwa muhula wa pili au mapema katika muhula wa tatu.
Baada ya kujifungua, madaktari hupima mtoto mzingo wa kichwa (kipimo cha kichwa kuzunguka eneo lake kubwa zaidi) wakati wa uchunguzi wa kawaida wa kimwili. Madaktari hugundua mikrosefali wakati mzingo wa kichwa unapoonekana kuwa mdogo kiasi kikubwa kuliko wastani wa kawaida wa watoto wa jinsia, umri, na kabila moja katika eneo ambalo mtoto anaishi. Mara chache, utambuzi hufanywa wakati mzingo wa kichwa cha mtoto ulipoanza katika kipimo cha kawaida lakini hauongezeki ipasavyo kadiri mtoto anavyokua.
Wakati wa kufanya utambuzi, madaktari pia huzingatia mzingo wa kichwa wa wazazi wa mtoto kwa sababu ukubwa wa kichwa ulio mdogo kidogo unaweza kuwa ni sifa ya familia (hali inayoitwa benign familial microcephaly).
Ikiwa mikrosefali ipo, madaktari kwa kawaida hufanya tomografia ya kompyuta (CT) au MRI ya ubongo ili kutafuta hitilafu. Madaktari pia huwafanya uchunguzi kwa mtoto mchanga na wazazi wake ili kutafuta vyanzo vinavyowezekana vya mikrosefali na kisha hufanya vipimo kwa ajili ya chanzo chochote wanachokihisi. Wakati mwingine daktari anaweza kuomba vipimo vya damu ili kusaidia kubaini kisababishaji.
Mtoto aliye na kasoro hii ya kuzaliwa anaweza kuchunguzwa na mtaalamu wa jeni. Mtaalamu wa vinasaba ni daktari ambaye amebobea katika elimu ya jeni (sayansi ya jeni na jinsi sifa au tabia fulani zinavyorithishwa kutoka kwa wazazi kwenda kwa watoto). Upimaji wa kijenetiki wa sampuli ya damu ya mtoto unaweza kufanywa ili kuangalia kasoro za kromosomu na jeni. Upimaji huu unaweza kuwasaidia madaktari kubaini kama tatizo maalum la kijenetiki ndilo chanzo na kufutilia mbali sababu nyingine.
Matibabu ya Kichwa Kidogo cha Mtoto
Matibabu ya dalili
Mkakati wa kutatua matatizo ya akili na mwili
Mikrosefali ni hali ya maisha yote, na haina tiba, lakini dalili zinazotokana na uharibifu wa ubongo hutibiwa, na baadhi ya matatizo yanayosababisha mikrosefali yanaweza kutibiwa.
Uchunguzi wa mara kwa mara na ufuatilizi na timu ya utunzaji ni muhimu sana. Huduma za ukuaji, zinazojulikana kama uingiliaji wa mapema, mara nyingi huwasaidia watoto wenye mikrosefali kuongeza uwezo wao wa kimwili na wa kiakili.
Ikiwa familia ya mtoto ina kichwa kidogo, kwa kawaida matibabu si ya lazima.
Taarifa Zaidi
Nyenzo zifuatazo za lugha ya Kiingereza zinaweza kuwa muhimu. Tafadhali kumbuka kuwa Mwongozo hauwajibiki kwa maudhui ya nyenzo hizi.