BRUE (matukio mafupi, yaliyotatuliwa, yasiyoelezeka) si ugonjwa mahususi. Ni neno linalotumika kuelezea tukio la ghafla la mabadiliko ya kupumua, mabadiliko ya rangi, mabadiliko ya ulaini wa misuli, au mabadiliko ya kiwango cha mwitikio kwa watoto wachanga walio chini ya mwaka 1.
Tukio huainishwa kama BRUE ikiwa hakuna sababu ya dalili zinazopatikana baada ya tathmini ya kwanza na ya kina ya kimatibabu.
Dalili zinazofanana zinaweza kusababishwa na matatizo ya mmeng'enyo wa chakula, mfumo wa neva, kupumua, magonjwa ya kuambukiza, moyo, na matatizo ya umetaboli pamoja na majeraha ya kimwili.
Utambuzi huo unategemea majadiliano na walezi, uchunguzi wa kimwili, na wakati mwingine matokeo ya vipimo fulani vya maabara.
Matibabu hulenga sababu maalum, ikiwa zitatambuliwa.
Wakati mwingine watoto wachanga huwa na vipindi vya dalili vinavyoongeza wasiwasi kuhusu afya zao. Hapo awali, madaktari walitumia neno "tukio linaloonekana kutishia maisha" (ALTE) kuelezea matukio yote ambapo watoto wachanga ghafla walipata dalili zilizomtia wasiwasi mtu aliyeshuhudia tukio hilo. Sasa, madaktari hurejelea matukio kama hayo kama tukio fupi, lililotatuliwa, lisiloelezeka (BRUE). Neno linalotumika sasa linalenga juhudi za kutafuta sababu ya tukio badala ya mtazamo kwamba linahatarisha maisha.
BRUE inaelezea vipindi vinavyotokea kwa watoto walio chini ya umri wa mwaka 1 pekee:
B = Fupi: Tukio hilo hudumu kwa chini ya dakika 1.
R = Limetatuliwa: Tukio linaisha na mtoto anarudi katika hali yake ya kawaida ya afya.
U = Halielezeki: Hakuna sababu inayoweza kupatikana baada ya tathmini ya daktari.
E = Tukio: Mtoto ana dalili kama vile mabadiliko ya kupumua au kipindi cha kutopumua (apnea), mabadiliko ya rangi, mabadiliko ya ulaini wa misuli, na/au mabadiliko katika kiwango cha mwitikio.
Vipindi kama hivyo vinaweza kuonekana vinahusishwa na kifo cha ghafla kisichoelezeka cha watoto wachanga (SUID) na ugonjwa wa kifo cha ghafla cha watoto wachanga (SIDS), lakini BRUE ni utambuzi tofauti ambao una visababishi tofauti na huwaathiri watoto wachanga katika umri tofauti na katika hali tofauti.
Dalili za BRUE
BRUE hujulikana kwa mabadiliko yasiyotarajiwa na ya ghafla kwa mtoto mchanga ambayo humtia wasiwasi mzazi au mlezi.
Matukio ya BRUE ambayo yanaweza kumtisha mzazi au mlezi ni pamoja na baadhi au yote yafuatayo:
Kusita kupumua kwa muda mfupi wa sekunde 20 au zaidi (apnea), kupumua bila utaratibu, au kutopumua kabisa
Mabadiliko ya rangi, bluu au rangi ya hudhurungi
Mabadiliko ya ulaini wa misuli, ngumu sana au laini
Mabadiliko katika kiwango cha mwitikio (kwa mfano, usingizi, kutulia sana, au kupoteza fahamu)
Sababu za dalili zinazofanana na BRUE
Sababu ya dalili hizi za kutisha hubainika katika takribani nusu ya watoto wachanga walioathiriwa. Wakati sababu ya dalili inapotambuliwa wakati wa tathmini ya kimatibabu, kipindi hicho hakizingatiwi kuwa BRUE.
Wakati sababu ipo, sababu zinazoweza kupatikana mara nyingi ni pamoja na:
Matatizo ya mmeng'enyo wa chakula: Ugonjwa wa refluksi gastroesofajia au ugumu wa kumeza
Matatizo ya mfumo wa neva: Vifafa au uvimbe wa ubongo, kushikilia pumzi, au haidrosefalasi
Matatizo ya kupumua: Husababishwa na, kwa mfano, virusi vya sinsishamu vya njia ya hewa, homa ya mafua (mafua), au kifaduro
Maambukizi: Sepsisi au meninjitisi
Sababu zisizoweza kupatikana mara nyingi ni pamoja na:
Matatizo ya moyo
Matatizo ya umetaboli
Kuziba njia za hewa kwa njia nyembamba au kamili (apnea ya usingizi inayoziba njia ya hewa)
Sababu nyingine (ikiwa ni pamoja na vitu kama vile pombe na dawa kama vile dawa za mafua zisizohitaji agizo la daktari, unyanyasaji wa watoto, au mmenyuko wa anafailaktiki)
Utambuzi wa BRUE
Tathmini ya daktari
Vipimo vingine kulingana na matokeo ya tathmini
Wakati kipindi chenye dalili za BRUE kinatokea, daktari huuliza maswali kadhaa muhimu:
Ni nini kilichoonekana na mlezi aliyeshuhudia tukio hilo (ikiwa ni pamoja na maelezo ya mabadiliko ya kupumua, rangi, ulaini wa misuli, na macho, kelele zilizotolewa, urefu wa tukio, na dalili zilizotokea kabla ya tukio)?
Ni hatua gani zilizochukuliwa (kama vile kusisimua taratibu, kupumua kwenye mdomo, au kurudisha fahamu [CPR])?
Je, mama alitumia dawa au dawa za kulevya wakati wa ujauzito? Je, walezi wa sasa au wanafamilia wanatumia dawa haramu za kulevya, tumbaku, au pombe kwa sasa?
Umri wa ujauzito wa mtoto ulikuwa upi (idadi ya wiki za ujauzito)? Je, kulikuwa na matatizo yoyote wakati wa kuzaliwa?
Je, mtoto hukohoa, au kutapika wakati wa kunyonyesha? Je, kumekuwa na tatizo la ongezeko duni la uzito?
Je, mtoto amefikia hatua zote za ukuaji na za maendeleozinazofaa kwa umri wake?
Je, mtoto amewahi kupata tukio kama hilo hapo awali au amepata jeraha au maambukizi hivi karibuni?
Je, kumekuwa na matukio yoyote kama hayo, vifo vya mapema, au midundo isiyo ya kawaida ya moyo katika familia?
Daktari hufanya uchunguzi wa kimwili ili kuangalia kasoro dhahiri, hasa kasoro za mfumo wa neva, kama vile kuwa mgumu sana (mkao), kuwa na ulaini mdogo wa misuli (laini sana), au kuwa na misuli ngumu au inayosogea kwa mtindo wa kutetemeka (mkazo wa ghafla), na kuangalia dalili za maambukizi, jeraha, au tuhuma za unyanyasaji wa watoto.
Kulingana na majadiliano na walezi pamoja na uchunguzi wa kimwili, daktari anaweza kuwa na taarifa za kutosha kuhakikisha mtoto yuko katika hatari ndogo au kubwa ya kuwa na tatizo mbaya la kiafya. Ikiwa hatari ni ndogo, mtoto anaweza kuhitaji ufuatiliaji mfupi tu (saa 1 hadi 4) wa kiwango cha oksijeni kwenye damu na wakati mwingine kipimo cha elektrokadiogramu au kipimo cha kifaduro. Ikiwa hatari ni kubwa, upimaji wa ziada, ufuatiliaji, au vyote viwili hupendekezwa.
Wakati mwingine daktari anaweza kufanya vipimo vya maabara (kama vile vipimo vya damu ili kuangalia upungufu wa damu au maambukizi na vipimo vya utenda kazi wa figo na ini, pamoja na utafiti wa kinyesi, mkojo, na maji ya uti wa mgongo), vipimo vya upigaji picha (kama vile eksirei ya kifua au uchanganuzi wa tomografia ya kompyuta [CT] ya kichwa), elektrokadiogrmu, au mchanganyiko wa vipimo kulingana na matokeo ya uchunguzi wa mtoto mchanga. Vipimo vingine vya kuangalia shughuli zinazowezekana za kifafa (kama vile electroencephalogram) pia vinaweza kufanywa.
Matibabu ya BRUE
Matibabu ya sababu zilizotambuliwa
Elimu kwa wazazi au walezi
Sababu, ikitambuliwa, hutibiwa.
Watoto wachanga waliohitaji CPR baada ya kipindi hicho, waliokuwa na kasoro zozote zilizotambuliwa wakati wa uchunguzi au upimaji wa maabara, au ambao historia yao inampa wasiwasi daktari hulazwa hospitalini kwa ufuatiliaji na tathmini zaidi.
Wazazi na walezi wanapaswa kuelimishwa kuhusu BRUEs na kufunzwa kuhusu CPR kwa watoto wachanga na katika utunzaji salama wa watoto wachanga kwa ujumla kama vile kuwalaza chali watoto wachanga.
Kuvuta sigara ni kisababishi cha BRUE, kwa hivyo watoto wachanga hawapaswi kukaribia moshi wa tumbaku.
Ubashiri wa BRUE
Hatari ya kupata matatizo makubwa baada ya BRUE yenye hatari ndogo ni ndogo sana na matarajio ni ya kutia moyo.
Takribani asilimia 10 ya watoto wachanga walio na BRUE watapata BRUE nyingine katika siku zijazo. Watoto wachanga wanaolazwa hospitalini baada ya BRUE wana hatari kubwa ya kupata nyingine. Hata hivyo, kifo hakiwezekani kabisa.
Taarifa Zaidi
Nyenzo zifuatazo za lugha ya Kiingereza zinaweza kuwa muhimu. Tafadhali kumbuka kuwa Mwongozo hauwajibiki kwa maudhui ya nyenzo hizi.