Kasoro ya kuzaliwa nayo inaweza kutokea katika ogani yoyote inayounda njia ya mmeng'enyo wa chakula: umio, tumbo, utumbo mdogo, utumbo mkubwa, rektamu na tundu la haja kubwa.
Ogani za njia ya mmeng'enyo wa chakula zinaweza kuwa hazijaumbika vizuri au zimekaa isivyo kawaida, na kusababisha kuziba, au misuli au neva za njia ya mmeng'enyo wa chakula zinaweza kuwa na kasoro.
Dalili hutegemea eneo la kasoro lakini zinaweza kujumuisha maumivu ya tumbo, kuvimba kwa tumbo, na kutapika.
Utambuzi wa ugonjwa kwa kawaida hutegemea vipimo vya picha na vipimo vingine.
Kwa kawaida upasuaji unahitajika.
Kasoro za kuzaliwa nazo kwenye njia ya mmeng'enyo wa chakula zinaweza kujumuisha yafuatayo:
Kasoro za ukuta wa tumbo (ikiwa ni pamoja na omphalocele na gastroschisis)
Kuziba kwa nyongo (kasoro ya kuzaliwa nayo inayohusisha mifereji ya nyongo, ambayo iko nje ya njia ya kumeng'enya chakula lakini husaidia katika mmeng'enyo wa chakula)
Kuziba kwa umio na muingiliano wa koo la hewa na umio (tracheoesophageal fistula)
Mara nyingi, ogani haijaumbika kikamilifu au imekaa isivyo kawaida, ambayo mara nyingi husababisha kupungua au kuziba (kizuizi). Kuziba kunaweza kutokea sehemu yoyote kwenye njia ya mmeng'enyo wa chakula, ikiwa ni pamoja na kwenye umio, matumbo, rektamu au tundu la haja kubwa. Wakati mwingine sehemu ya njia ya mmeng'enyo wa chakula haiumbiki au kukua kawaida au huumbika kisha huharibiwa na tatizo linalotokea katika tumbo la uzazi kabla ya kuzaliwa. Misuli ya ndani au ya nje inayozunguka utobo wa tumbo inaweza kudhoofika au kutengeneza mashimo, kama ilivyo kwa kasoro za ukuta wa tumbo na ngiri ya kiwambo. Mishipa ya neva kwenye utumbo inaweza isiumbike, kama ilivyo kwa ugonjwa wa Hirschsprung (wa kuziba kwa utumbo mpana).
Dalili za Kasoro za Kuzaliwa za Njia ya Mmeng'enyo wa Chakula
Dalili hutegemea aina ya kasoro ya kuzaliwa nayo na mahali ilipo.
Watoto wachanga wanaweza kuwa na maumivu ya tumbo, kuvimba tumbo, kutapika, au mchanganyiko wa hayo. Shida ya ulaji inaweza kutokea, na watoto wachanga wanaweza wasiongezeke uzito kawaida.
Baadhi ya watoto wachanga hupata rangi ya manjano kwenye ngozi na weupe wa macho inayoitwa homa ya nyongo ya manjano.
Utambuzii wa Kasoro za Kuzaliwa za Njia ya Mmeng'enyo wa Chakula
Vipimo vya picha (eksirei na ultrasound)
Vipimo vya picha kwa kawaida huhitajika ili kugundua kasoro ya kuzaliwa ya njia ya mmeng'enyo wa chakula.
Mara nyingi, kasoro zinaweza kugunduliwa kabla ya kuzaliwa wakati wa ultrasound ya kabla ya kujifungua ya kawaida.
Baada ya kuzaliwa, kasoro zingine hugunduliwa kwa eksirei ya kifua au tumbo. Ultrasound inaweza pia kufanywa baada ya kuzaliwa ili kutambua na kupata kasoro.
Vipimo vingine vinaweza kujumuisha vipimo vya damu na utoaji wa kipande cha tishu kwa uchunguzi, biopsi. Wakati wa kuchukua kipande cha tishu kwa uchunguzi, biopsi, kipande cha tishu hutolewa kwa ajili ya uchunguzi kwenye hadubini.
Vipimo vingine, kama vile upimaji wa jeni, vinaweza kufanywa kulingana na matokeo na dalili zingine za vipimo.
Matibabu ya Kasoro za Kuzaliwa za Njia ya Mmeng'enyo wa Chakula
Upasuaji
Kasoro nyingi za njia ya mmeng'enyo wa chakula zinahitaji upasuaji. Kwa kawaida, uzibe hufunguliwa kwa upasuaji. Mashimo kwenye kuta za utobo wa tumbo hurekebishwa kwa upasuaji.