Maambukizi yanayopatikana hospitalini (hospital-acquired infections) ni yale yanayotokea baada ya mtoto mchanga kulazwa katika wodi ya watoto (nursery). Maambukizi haya hayatoki kwa mama wakati mtoto akiwa tumboni na hayatokei wakati wa mchakato wa kujifungua.
Maambukizi haya yanaweza kusababishwa na bakteria, virusi, au fangasi.
Dalili hutofautiana lakini zinaweza kujumuisha kutapika, homa, na upele kwenye ngozi.
Utambuzi kwa kawaida hutegemea uchunguzi wa kimwili unaofanywa na daktari.
Maambukizi hutibiwa kulingana na chanzo chake (aina ya kimelea).
Hatua mbalimbali, kama vile kunawa mikono kwa usahihi, zinaweza kusaidia kuzuia kuenea kwa maambukizi haya.
(Tazama pia Muhtasari wa Maambukizi kwa Watoto Wachanga.)
Baadhi ya watoto wachanga hupata maambukizi wakiwa tayari wamelazwa wodini badala ya kuyapata kutoka kwa mama yao wakiwa tumboni au wakati wa kuzaliwa. Wakati mwingine huwa haijulikani wazi ikiwa chanzo cha maambukizi ni mama au ni mazingira ya hospitali.
Maambukizi yanayopatikana hospitalini ni tatizo kubwa hasa kwa watoto wanaolazimika kukaa hospitalini kwa muda mrefu, kwa mfano, watoto waliozaliwa kabla ya wakati (njiti) na watoto waliozaliwa kwa wakati lakini wenye matatizo makubwa ya kiafya.
Maambukizi ya kawaida yanayopatikana hospitalini ni nimonia (maambukizi ya mapafu) na maambukizi ya kwenye damu (bacteremia) yanayotokana na mpira wa dawa (katheta/IV) uliowekwa kwenye mshipa ili kumpa mtoto majimaji au dawa.
Kwa watoto waliozaliwa kwa wakati (full-term), maambukizi yanayotokea mara nyingi hospitalini ni ya ngozi yanayosababishwa na bakteria ya Staphylococcus aureus. Mara nyingi, maambukizi haya hayatambuliki mpaka mtoto anapokuwa tayari ameshafika nyumbani.
Kwa watoto waliozaliwa na uzito mdogo sana, maambukizi mengi ya hospitalini pia husababishwa na bakteria za staphylococci. Lakini bakteria na fangasi wengine pia wanaweza kuwa chanzo. Kadiri uzito wa mtoto wakati wa kuzaliwa unavyokuwa mdogo, ndivyo hatari ya kupata maambukizi inavyoongezeka, hasa kwa watoto wanaohitaji mashine ya kupumulia au mrija wa IV kwa muda mrefu. Kadiri watoto wanavyokaa muda mrefu katika wodi maalum za watoto au vitengo vya uangalizi maalum wa watoto wachanga (NICU) na kufanyiwa taratibu nyingi za kitabibu, ndivyo uwezekano wa kupata maambukizi unavyoongezeka.
Dalili za Maambukizi Yanayopatikana Hospitalini kwa Watoto Wachanga
Dalili za maambukizi kwa watoto wachanga mara nyingi hazionyeshi ugonjwa mmoja mahususi (nonspecific). Kwa mfano, watoto wanaweza kutapika, kutokunyonya vizuri, kusinzia sana au kuwa wanyonge (lethargy), kuwa na homa au joto la chini sana, kupumua haraka, kupata vipele, kuharisha, au tumbo kuvimba
Utambuzi wa Maambukizi Yanayopatikana Hospitalini kwa Watoto Wachanga
Vipimo mbalimbali
Maambukizi ya hospitalini hushukiwa kulingana na hali ya mtoto na uchunguzi wa daktari.
Madaktari wanaweza kupima sampuli za damu, mkojo, na majimaji ya uti wa mgongo ili kubaini sehemu iliyoathirika na kimelea kinachosababisha maambukizi.
Matibabu ya Maambukizi Yanayopatikana Hospitalini kwa Watoto Wachanga
Inategemea na kimelea (organism)
Matibabu ya maambukizi yanayopatikana hospitalini hutegemea aina ya kimelea mahususi kilichosababisha ugonjwa huo.
Uzuiaji wa Maambukizi Yanayopatikana Hospitalini kwa Watoto Wachanga
Hatua za jumla ambazo wafanyakazi wa hospitali hutumia kusaidia kuzuia maambukizi haya ni pamoja na:
Hatua za kupunguza kuenea kwa bakteria ya Staphylococcus aureus
Kuzuia maambukizi kusambaa katika wodi maalum kama NICU
Kunawa mikono kwa uangalifu mkubwa
Ufuatiliaji wa karibu wa maambukizi hospitalini
Wakati mwingine dawa za kuua bakteria
Kuchanja
Ili kupunguza kuenea kwa maambukizi katika wodi maalum kama NICU, wafanyakazi huhakikisha kuna nafasi ya kutosha kati ya watoto walio kwenye vichanja vya joto (incubators). Pia wanakuwa makini sana kusafisha na kuua vijidudu (sterilize) kwenye vifaa, na kutumia mirija ya IV na mashine za kupumulia kwa muda mfupi tu iwezekanavyo.
Wafanyakazi wa hospitali, wazazi, na walezi wanaweza kusaidia kuzuia maambukizi kwa kunawa mikono yao vizuri kwa sabuni na maji au kutumia vitakasa mikono (sanitizers) kabla ya kumshika mtoto.
Wakiwa hospitalini, watoto hufuatiliwa kwa ukaribu ili kuona ishara zozote za maambukizi.
Ikiwa madaktari wataona kuwa maambukizi yanaenea wodini, wanaweza kuwapa antibiotiki watoto ambao bado hawajaambukizwa ili kuwalinda. Hatua hii ya kuzuia inaitwa prophylaxis.
Wafanyakazi wa hospitali hutoa chanjo kulingana na ratiba ya kawaida kwa mtoto yeyote aliye hospitalini wakati huo. Chanjo nyingine hazitolewi mpaka wakati mtoto anaporuhusiwa kurudi nyumbani (discharge).