Maambukizi ya Njia ya Mkojo (UTI) kwa Watoto

NaGeoffrey A. Weinberg, MD, Golisano Children’s Hospital
Imekaguliwa naBrenda L. Tesini, MD, University of Rochester School of Medicine and Dentistry
Imepitiwa/Imerekebishwa Feb 2024 | Imebadilishwa Jul 2025
v818519_sw

Maambukizi ya njia ya mkojo ni maambukizi ya bakteria ya kibofu cha mkojo (cystitis), figo (pyelonephritis), au zote mbwili.

  • Maambukizi ya njia ya mkojo husababishwa na bakteria.

  • Watoto wachanga na watoto wadogo ambao wana maambukizi ya njia ya mkojo wakati mwingine huwa na kasoro za kimaumbile katika mfumo wao wa mkojo ambazo huwafanya wawe katika hatari zaidi ya kuambukizwa magonjwa ya mkojo.

  • Watoto waliozaliwa majuzi na watoto wachanga huenda wasiwe na dalili zozote isipokuwa homa, ilhali watoto wakubwa huwa na maumivu au mwasho wakati wa kukojoa, maumivu katika eneo la kibofu cha mkojo, na huhisi kukojoa mara kwa mara.

  • Utambuzi huo unategemea uchunguzi na ukuzaji wa baktria wa mkojo kwenye maabara.

  • Viuavijasumu hutolewa ili kumaliza maambukizi.

  • Usafi sahihi unaweza kusaidia kuzuia maambukizi ya njia ya mkojo.

(Kwa watu wazima, angalia Muhtasari wa Maambukizi ya Njia ya Mkojo (UTI).)

Maambukizi ya njia ya mkojo (UTI) ni ya kawaida utotoni. Karibu magonjwa yote ya njia ya mkojo husababishwa na bakteria wanaoingia kwenye uwazi wa urethra (mrija unaotoa mkojo kutoka kwenye kibofu cha mkojo hadi nje ya mwili) na kwenda juu kwenye kibofu cha mkojo na wakati mwingine figo. Kwa nadra sana, katika maambukizi makali, bakteria wanaweza kuingia kwenye damu kutoka kwenye figo na kusababisha maambukizi kwenye damu (sepsis) au viungo vingine.

Wakati wa utotoni, wavulana wana uwezekano mkubwa wa kupata UTI. Wavulana wachanga ambao hawajatahiriwa pia wako katika hatari zaidi ya kupata UTI kwa sababu bakteria huwa wanajikusanya chini ya govi. Baada ya utoto, wasichana wana uwezekano mkubwa wa kupata UTI kwa sababu mirifa yao mifupi ya mkojo hurahisisha bakteria kufika kwenye njia ya mkojo. Kuvibiwa sana au matatizo ya utumbo pia yanadhaniwa kuwa chanzo cha UTI kwa watoto wachanga na watoto wakubwa.

Hata hivyo, watoto wachanga na wadogo ambao wana UTI kwa kawaida huwa na kasoro mbalimbali za kimaumbile katika mfumo wao wa mkojo ambazo huwafanya wawe katika hatari ya juu ya kuambukizwa magonjwa ya mfumo wa mkojo. Kasoro hizi ni pamoja na vesicoureteral reflux (VUR), ambayo ni kasoro ya ureta (mirija inayounganisha figo na kibofu cha mkojo) ambazo zinaruhusu mkojo kupita nyuma kutoka kwenye kibofu hadi kwenye figo, na hali kadhaa zinazozuia mtiririko wa mkojo. Takriban asilimia 50 ya watoto waliozaliwa majuzi na watoto wachanga wenye UTI na asilimia 20 hadi 30 ya watoto wenye umri wa kwenda shule wenye UTI wana matatizo kama hayo.

Kwa watoto wa umri wa kwenda shule na vijana waliobalehe, kisukari, majeraha, na, kwa wanawake, kufanya ngono huongeza hatari ya kupata UTI.

Njia ya Mkojo

Watoto wengi wachanga na watoto wa shule ya awali walio na UTI—hasa wale walio na homa—huwa na maambukizi ya kibofu cha mkojo na maambukizi ya figo. Ikiwa figo itaambukizwa mara kwa mara na VUR ni kali, takriban 25% ya watoto hupata makovu kwenye figo. Ikiwa kuna VUR kidogo au hakuna kabisa, ni watoto wachache sana hupata makovu kwenye figo. Makovu ni jambo la kutia wasiwasi kwa sababu linaweza kusababisha shinikizo la juu la damu na utendakazi wa figo wenye kasoro katika utu uzima.

(Angalia pia Muhtasari wa Maambukizi ya Bakteria Utotoni.)

Dalili za UTI kwa Watoto

Watoto waliozaliwa majuzi wenye UTI huenda wasiwe na dalili zozote isipokuwa homa. Wakati mwingine hawali vizuri au hawakui vizuri, huwa wavivu (walegevu), hutapika, au wanaharisha. Watoto waliozaliwa majuzi wanaweza kupata maambukizi makubwa mwilini (sepsis) kutokana na UTI ambayo haijatibiwa.

Watoto wachanga na watoto walio chini ya umri wa miaka 2 wenye UTI wanaweza kuwa na homa, kutapika, kuhara, maumivu ya tumbo, au mkojo wenye harufu mbaya.

Watoto zaidi ya umri wa miaka 2 kwa kawaida, wenye UTI huwa na dalili za kawaida za maambukizi ya kibofu cha mkojo au figo sawa na watu wazima.

Watoto wenye maambukizi ya kibofu cha mkojo (cystitis) kwa kawaida huwa na maumivu au mwasho wakati wa kukojoa, kuhisi kukojoa mara kwa mara na haraka, na maumivu katika eneo la kibofu. Wanaweza kuwa na ugumu wa kukojoa au kuzuia mkojo (kushindwa kujizuia kukojoa). Mkojo unaweza kutoa harufu mbaya.

Watoto wenye maambukizi ya figo (pyelonephritis) kwa kawaida huwa na maumivu upande au mgongoni juu ya figo zilizoathiriwa, homa kali, kibaridi na hisia ya jumla ya ugonjwa (unyonge).

Watoto walio na kasoro za njia ya mkojo wanaweza kuwa na uvimbe tumboni, figo zilizopanuka, uwazi usio wa kawaida kwenye mrija wa mkojo au uwezekano wa kuwa na kasoro kwenye uti wa mgongo wa chini. Watoto ambao hawana mtiririko thabiti wa mkojo wanaweza kuwa na kizuizi katika mojawapo ya mirija inayosafirisha mkojo kutoka kwenye figo hadi kwenye kibofu cha mkojo (ureta) au huenda hawawezi kudhibiti kibofu chao kwa sababu ya tatizo la neva.

Je, Ulijua...

  • Maambukizi ya njia ya mkojo kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 2 yanaweza kuwa na dalili na visababishi tofauti sana na vya watu wazima.

Utambuzi wa UTI kwa Watoto

  • Vipimo vya mkojo

  • Upigaji picha wa njia ya mkojo

  • Wakati mwingine vipimo vya damu

Vipimo vya mkojo

Daktari hutambua UTI kwa kuchukua sampuli ya mkojo (uchunguzi wa mkojo) na kuituma kwa ajili ya ukuzaji wa bakteria wa mkojo kwenye maabara ili kukuza bakteria yoyote aliyopo.

UTI huongeza viwango vya seli nyeupe za damu na bakteria kwenye mkojo. Ili kugundua seli hizi nyeupe za damu na bakteria, mtaalamu wa maabara huchunguza mkojo kwa darubini na kufanya vipimo kadhaa vya kemikali. Mtaalamu huyo pia hufanya ukuzaji wa bakteria wa mkojo na kutambua bakteria yoyote aliyopo. Ukuzaji wa bakteria ndio muhimu zaidi katika ya vipimo hivi.

Kipimo cha Maabara

Watoto waliofunzwa kwenda choo wanaweza kutoa sampuli ya mkojo kwa kutumia mbinu ya kukusanya sampuli bila uchafuzi. Kwa njia hii, uwazi wa mrija kwa mkojo husafishwa kwa pedi ndogo yenye dawa ya antiseptiki. Kisha mtoto hukojoa kiasi kidogo cha mkojo ndani ya choo, na kuosha mrija wa mkojo. Kisha watoto husitisha kukojoa chooni na kuendelea kukojoa kwenye kikombe kilichotakaswa.

Madaktari hupata mkojo wa watoto wadogo na watoto wachanga kwa kuingiza mrija mwembamba, unaonyumbulika na uliotakaswa (katheta) kupitia uwazi wa mrija wa mkojo ndani ya kibofu. Mchakato huu unaitwa utumiaji wa katheta.

Kwa baadhi ya wavulana waliozaliwa majuzi na watoto wachanga, govi huwa limebana sana kuweza kuvutwa nyuma juu ya kichwa cha uume, na hivyo kuzuia uwazi wa mrija wa mkojo, kwa hivyo daktari anahitaji kuvuta mkojo kutoka kwenye kibofu kwa sindano inayoingizwa kupitia ngozi juu kidogo ya mfupa wa kinena.

Wakati mwingine madaktari hubandika mfuko wa kukusanya mkojo kwenye eneo kati ya sehemu za siri na mkundu ili kukusanya mkojo kwa ajili ya vipimo vingine. Mkojo unaokusanywa kwa njia hii haufai kwa utambuzi wa UTI kwa sababu umechafuliwa na bakteria na vitu vingine kutoka kwenye ngozi.

Vipimo vya picha

Kasoro nyini za kimaumbile katika mfumo wa mkojo hutambuliwa kabla ya kuzaliwa wakati wa picha ya mawimbi ya sauti ya kabla ya kujifungua. Hata hivyo, wakati mwingine watoto huwa na kasoro ambazo haziwezi kuonekana wakati wa uchunguzi wa picha ya mawimbi ya sauti kabla ya kujifungua. Kwa hiyo, wavulana wa rika zote na wasichana walio chini ya miaka 3 ambao hupata hata UTI moja kwa kawaida huhitaji vipimo zaidi ili kuangalia kasoro za kimaumbile za mfumo wa mkojo. Wasichana wakubwa ambao wamekuwa na UTI zinazorudi pia wanahitaji vipimo hivi.

Vipimo hivyo ni pamoja na

  • Picha ya mawimbi ya sauti ya figo na kibofu cha mkojo

  • Bila shaka upigaji wa eksirei ya kibofu na urethra wakati wa kukojoa (VCUG)

  • Wakati mwingine radionuclide cystography (RNC) au uchunguzi wa figo wa radionuclide

Picha ya mawimbi ya sauti hupigwa ili kutambua kasoro na kuziba kwa figo na kibofu.

Upigaji wa eksirei ya kibofu na urethra wakati wa kukojoa (VCUG) unaweza kufanywa ili kutambua zaidi kasoro za figo, ureta, na kibofu cha mkojo na unaweza kutambua wakati ambapo kiasi cha mkojo kimerejeshwa (kurudi nyuma). Kwa upigaji wa eksirei ya kibofu na urethra wakati wa kukojoa, katheta hupitishwa kupitia mrija wa mkojo hadi kwenye kibofu, rangi huwekwa kupitia katheta, na eksrei hupigwa kabla na baada ya mtoto kukojoa. Upigaji wa eksirei ya kibofu na urethra wakati wa kukojoa unaweza kufanywa ikiwa uchunguzi wa picha ya mawimbi ya sauti hauonyeshi ukawaida au ikiwa watoto wanapata UTI inayojirudia.

Radionuclide cystography ni sawa na upigaji wa eksirei ya kibofu na urethra wakati wa kukojoa isipokuwa kwamba ajenti za mionzi huwekwa kwenye kibofu cha mkojo na picha hupigwa kwa kutumia skana ya nyuklia. Utaratibu huu huweka ovari au korodani za mtoto kwenye hatari ya mionzi kidogo kuliko upigaji wa eksirei ya kibofu na urethra wakati wa kukojoa. Hata hivyo, radionuclide cystography ni muhimu zaidi kwa kufuatilia uponaji wa mkojo kurudi nyuma kuliko kwa ajili ya kuutambua, kwa sababu maumbile hayaonyeshwi vizuri ikilinganishwa na upigaji wa eksirei ya kibofu na urethra wakati wa kukojoa.

Katika aina nyingine ya uchanganuzi wa nyuklia, dutu yenye mionzi (inayoitwa dimercaptosuccinic acid au DMSA) huingizwa kwenye vena na kuingia kwenye figo. Dutu hii hugunduliwa na kamera maalum zinazopiga picha za ndani ya figo. Uchanganuzi wa DMSA unaweza kutumika kuthibitisha utambuzi wa pyelonephritis na kutambua makovu kwenye figo. Inatumika zaidi kwa watoto wenye UTI kali au UTI zinazosababishwa na bakteria fulani.

Kipimo cha Maabara
Kipimo cha Maabara

Vipimo vya damu

Vipimo vya damu na vipimo vinavyobaini kama uvimbe upo (protini ya C-reactive na kiwango cha uundaji mashapo ya erythrocyte) hufanywa kwa watoto ambao matokeo ya vipimo vya mkojo hayathibitishi utambuzi, au hufanywa ili kuwasaidia madaktari kutambua maambukizi ya figo pamoja na maambukizi ya kibofu.

Ukuzaji wa bakteria za damu kwenye maabara hufanywa kwa watoto wachanga walio na UTI na kwa watoto wenye umri wa zaidi ya mwaka 1 hadi 2 ambao ni wagonjwa sana.

Matibabu UTI kwa Watoto

  • Dawa za kuua bakteria

  • Wakati mwingine upasuaji

UTI hutibiwa kwa kutumia viuavijasumu. Watoto wanaoonekana kuwa wagonjwa sana au ambao matokeo yao ya awali ya vipimo yanaashiria UTI hupewa viuavijasumu kabla ya matokeo ya ukuzaji wa bakteria kwenye maabara kupatikana. Vinginevyo, madaktari husubiri matokeo ya ukuzaji wa bakteria wa mkojo kwenye maabara ili kuthibitisha utambuzi wa UTI. Watoto ambao ni wagonjwa sana na watoto wote waliozaliwa majuzi hupokea viuavijasumu kwa sindano kwenye misuli (ndani ya misuli) au kwenye mshipa (ndani ya vena). Watoto wengine hupewa viuavijasumu vya kumeza. Matibabu kwa kawaida huchukua takriban siku 7 hadi 10. Watoto wanaohitaji vipimo ili kutambua kasoro za kimaumbile mara nyingi huendelea na matibabu ya viuavijasumu kwa dozi ya chini hadi vipimo vitakapokamilika.

Baadhi ya watoto wenye matatizo ya kimaumbile katika njia ya mkojo wanahitaji upasuaji ili kurekebisha tatizo hilo. Wengine wanahitaji kutumia viuavijasumu kila siku ili kuzuia maambukizi (vinavyojulikana kama prophylaxis). Watoto walio na VUR kali kwa kawaida huhitaji upasuaji na wanahitaji kutumia viuavijasumu hadi watakapofanyiwa upasuaji. Watoto ambao wana VUR isiyo kali hufuatiliwa kwa karibu na wanaweza kupewa viuavijasumu.

Baadhi ya visa vya VUR nyepesi hadi wastani huisha bila matibabu.

Ubashiri wa UTI kwa Watoto

Watoto wanaopokea matibabu sahihi mara chache hupata tatizo la figo kushindwa kufanya kazi (figo kutoweza kuchuja vya kutosha uchafu wa umetaboli kutoka kwenye damu) isipokuwa wana kasoro za njia ya mkojo ambazo haziwezi kurekebishwa. Hata hivyo, UTI zinazojirudia, hasa kwa watoto walio na VUR kali, zinadhaniwa kusababisha makovu kwenye figo, ambayo yanaweza kusababisha shinikizo la damu na ugonjwa sugu wa figo katika utu uzima.

Kinga ya UTI kwa Watoto

Kuzuia UTI ni vigumu, lakini usafi sahihi unaweza kusaidia.

Wasichana wanapaswa kufundishwa kujipangusa kutoka mbele kwenda nyuma (badala ya kutoka nyuma kwenda mbele) baada ya kwenda haja kubwa na baada ya kukojoa ili kupunguza uwezekano wa bakteria kuingia kwenye uwazi wa mrija wa mkojo.

Kuepuka kuoga mara kwa mara kwa viputo, ambayo inaweza kuwasha ngozi karibu na uwazi wa mrija wa mkojo, kunaweza kusaidia kupunguza hatari ya kupata UTI kwa wavulana na wasichana.

Kutahiri wavulana hupunguza hatari ya kupata UTI wakiwa wachanga. Wavulana waliotahiriwa huambukizwa UTI mara 1/10 pekee mara nyingi ikilinganishwa na wavulana ambao hawajatahiriwa, lakini haijulikani wazi kama faida hii yenyewe ni sababu ya kutosha ya kutahiriwa.

Kukojoa mara kwa mara na kwenda haja kubwa mara kwa mara (hasa matibabu ya kuvimbiwa) kunaweza kupunguza hatari ya kupata UTI.