Mimba husababisha mabadiliko mengi katika mwili wa mwanamke. Mengi ya mabadiliko haya hupotea baada ya kujifungua. Mabadiliko haya husababisha dalili fulani (hisia mpya au tofauti mwilini mwako), ambazo nyingi ni za kawaida. Hata hivyo, matatizo fulani, kama vile shinikizo la juu la damu, yanaweza kutokea wakati wa ujauzito na baadhi ya dalili zinaweza kuonyesha ugonjwa kama huo.
Ikiwa uchungu wa kujifungua ulikuwa wa haraka katika ujauzito uliopita, wanawake wanapaswa kumfahamisha daktari wao mara tu wanapoona dalili zozote kwamba uchungu wa kujifungua unaanza.
Dalili za kawaida za ujauzito
Dalili nyingi ni za kawaida wakati wa ujauzito. Mara nyingi huwa ndogo na kwa kawaida husababishwa na mabadiliko ya kawaida yanayohusiana na ujauzito. Hata hivyo, ikiwa dalili ni mpya, kali, au inayoendelea, mwanamke anapaswa kuwasiliana na daktari wake.
Dalili ambazo kwa kawaida husababishwa na mabadiliko ya kawaida yanayohusiana na ujauzito ikiwa dalili ni ndogo ni pamoja na
Kichefuchefu na kutapika, hasa kipindi cha awali cha ujauzito
Tamaa ya aina fulani ya chakula au kuchukia chakula fulani (baadhi ya vyakula huwa na ladha mbaya)
Kuongezeka kwa hisia ya kunusa
Kuvimba kwa matiti
Uchovu
Maumivu ya sehemu ya chini ya mgongo
Kuvimba kwa miguu na kifundo cha mguu
Dalili zinazoweza kuongeza wasiwasi kuhusu ujauzito
Baadhi ya dalili ni sehemu ya mchakato wa kawaida wa uchungu wa kujifungua na kujifungua, zinapotokea katika ujauzito uliokamilisha kipindi kinachofaa. Hata hivyo, iwapo dalili hizi zitatokea mapema wakati wa ujauzito, wanawake wanapaswa kuwasiliana na daktari wao. Dalili hizi huenda zikasababishwa na tatizo la ujauzito, kama vile uwezekano wa kuharibika kwa mimba au uchungu wa uzazi kabla ya wakati.
Dalili za uchungu wa kawaida wa uzazi au uwezekano wa kuwepo kwa tatizo kwenye ujauzito ni pamoja na
Uchungu au maumivu ya tumbo (maumivu ya fupanyonga)
Mikazo
Kuvuja kwa maji ya amniotiki (yaliyofafanuliwa kama "kupasuka kwa maji")
Kupungua kwa mwendo wa kijusi (baada ya wiki 24 za ujauzito)
Dalili zinazoweza kuongeza wasiwasi kuhusu matatizo mengine
Wanawake wajawazito wanaweza kupata matatizo yanayotokea wakati wa ujauzito pekee. Pia wanaweza kupata matatizo mengine yasiyohusiana na ujauzito. Haya huenda yakasababisha dalili zisizo za kawaida, kali, au zinazoendelea.
Wanawake wajawazito wanapaswa kuwasiliana na daktari wao iwapo wana dalili ambazo hazihusiani na mabadiliko ya kawaida ya ujauzito, ikiwa ni pamoja na
Homa
Maumivu wakati wa kukojoa au hitaji la kukojoa mara kwa mara au kwa njia ya dharura.
Maumivu makali ya mgongo au ubavu
Kiungulia
Kichefuchefu na kutapika kunaoendelea, hasa ikiwa viowevu havisalii tumboni
Kizunguzungu au kuwa na kisulisuli
Mapigo ya moyo ya haraka au mpapatiko wa moyo
Maumivu ya kichwa yanayoendelea au yasiyo ya kawaida
Matatizo ya macho
Kupungua kwa kukojoa
Maumivu makali au yanayoendelea katikati au sehemu ya juu ya tumbo
Dalili zozote za maambukizi au ugonjwa mwingine (kama vile upele, kuhisi mgonjwa)