Tatizo la Kuamsha/Tamaa ya ngono

(Libido ya Chini kwa Wanawake)

NaAllison Conn, MD, Baylor College of Medicine, Texas Children's Pavilion for Women;
Kelly R. Hodges, MD, Baylor College of Medicine, Texas Children's Pavilion for Women
Imekaguliwa naOluwatosin Goje, MD, MSCR, Cleveland Clinic, Lerner College of Medicine of Case Western Reserve University
Imepitiwa/Imerekebishwa Imebadilishwa Jul 2023
v804754_sw

Tatizo la kuvutiwa au kuamshwa kingono kwa wanawake ni ukosefu au kupungua kwa hamu ya kufanya ngono (hamu ndogo ya ngono), pamoja na mawazo ya kingono na/au ukosefu wa mwitikio kwa msisimko wa kingono.

  • Mambo mengi yanaweza kuathiri hamu ya mwanamke ya ngono na uwezo wake wa kuamshwa kingono, yakiwemo matatizo ya uhusiano, kukoma hedhi, matumizi ya dawa, magonjwa, mfadhaiko, wasiwasi, msongo wa mawazo, na historia ya kiwewe cha kingono.

  • Madaktari hutambua tatizo la kuvutiwa/kuamshwa kingono kwa kuzingatia maelezo ya mwanamke kuhusu tatizo pamoja na vigezo maalum vya utambuzi.

  • Kuboresha uhusiano, mazingira ya shughuli za ngono, na kutambua kinachomchochea mwanamke kingono kunaweza kusaidia.

  • Dawa au tiba za kisaikolojia, hasa tiba ya utambuzi inayotegemea umakinifu (mindfulness-based cognitive therapy), zinaweza kupendekezwa.

(Angalia pia Muhtasari wa Ukosefu wa Ngono kwa Wanawake.)

Mabadiliko ya muda katika hamu ya ngono au kuamshwa kingono ni ya kawaida katika maisha ya kingono ya mwanamke. Hata hivyo, tatizo la kuvutiwa/kuamshwa kingono husababisha kupungua kwa kudumu au kutokuwepo kabisa kwa hamu ya ngono na mwitikio kwa msisimko wa kingono. Ukosefu wa hamu ya ngono na kutoweza kuamshwa kingono huchukuliwa kuwa tatizo la kiafya tu ikiwa kunamsumbua mwanamke na ikiwa hamu haipo katika tukio nzima la kingono.

Kwa kawaida, mwanamke huhisi msisimko wa kingono kiakili na kihisia anapochangamshwa kingono. Huenda pia kukawa na mabadiliko fulani ya kimwili. Kwa mfano, uke hutoa ute unaosaidia kulainisha (na kusababisha unyevunyevu). Mtiririko wa damu kwenda kwenye sehemu za siri huongezeka, na kusababisha tishu zinazozunguka uwazi wa uke (labia) na kisimi (ambacho hulingana na uume kwa wanaume) kuvimba; matiti huvimba kidogo, na maeneo haya yanaweza kutoa hisia ya kuwashwa au kuchomachoma. Katika tatizo la kuvutiwa/kuamshwa kingono, hisia hizi zote au baadhi yake hukosekana au hupungua kwa kiasi kikubwa.

Tatizo la kuvutiwa/kuamshwa kingono linaainishwa kama ifuatavyo:

  • Kihisia (subjective): Mwanamke hahisi kuamshwa na aina yoyote ya msisimko wa kingono, ikiwemo kubusiana, kucheza, kutazama video za kimapenzi au za ngono, au kuchangamshwa kimwili kupitia sehemu za siri. Hata hivyo, mwanamke mwenye tatizo la kuvutiwa/kuamshwa kingono la kihisia anaweza bado kuwa na mwitikio wa kimwili kwa msisimko wa kingono. Kwa mfano, mtiririko wa damu kwenda kwenye kisimi huongezeka (na kusababisha kuvimba), na uzalishaji wa ute wa uke huongezeka.

  • Kimaumbile (genital): Mwanamke huhisi kuamshwa na msisimko usiohusisha sehemu za siri (kama video ya ngono), lakini hapati msisimko wa kimwili kutokana na kuguswa sehemu za siri. Uzalishaji wa ute wa uke na/au hisi ya sehemu za siri hupungua.

  • Mchanganyiko: Mwanamke huhisi msisimko mdogo sana au msisimko hutokuwepo kabisa kwa aina yoyote ya uchangamshaji wa kingono. Mwitikio wa kimwili (kuongezeka kwa mtiririko wa damu kwenye sehemu za siri na uzalishaji wa ute wa uke) ni mdogo sana au haupo. Anaweza kuripoti kuhitaji vilainishi vya nje na kwamba kisimi hakivimbi tena.

Sababu za Tatizo la Kuamsha/Tamaa ya Ngono

Chanzo cha tatizo la kuvutiwa/kuamshwa kingono mara nyingi hakijulikani. Sababu zinazojulikana ni pamoja na:

  • Sababu za kisaikolojia, kama ukosefu wa mawasiliano kati ya wenzi, matatizo ya uhusiano, mfadhaiko, wasiwasi, mtazamo hasi wa nafsi ya kingono, msongo wa mawazo, na vikengeushi

  • Matukio ya kingono yasiyoridhisha

  • Sababu za kimwili, kama magonjwa fulani sugu, kukoma hedhi, ugonjwa wa mfumo wa mkojo-uzazi unaohusiana na kukoma hedhi, matumizi ya dawa fulani, uchovu, na udhaifu wa mwili

Magonjwa sugu fulani (kama kisukari au sclerosis nyingi) yanaweza kuharibu neva, na hivyo kupunguza mtiririko wa damu na/au hisia katika eneo la sehemu za siri.

Matumizi ya dawa fulani, zikiwemo dawa za kupunguza mfadhaiko (hasa vizuizi teule vya ufyonzaji upya wa serotonini), opioidi, baadhi ya dawa za kuzuia mshtuko, na vizuizi vya beta, yanaweza kupunguza hamu ya ngono; hali hii pia inaweza kuchangiwa na unywaji wa pombe kupita kiasi.

Wanawake wengi hupata kupungua kwa hamu ya ngono baada ya kukoma hedhi kutokana na mchakato wa asili wa kuzeeka au kuondolewa kwa ovari kwa upasuaji (oophorectomy). Viwango vya estrojeni na progesterone hupungua kwa kiasi kikubwa baada ya kukoma hedhi. Testosterone hupungua taratibu kadri umri unavyoongezeka, lakini haipungui ghafla wakati wa kukoma hedhi.

Hata hivyo, kwa ujumla, tatizo la kuvutiwa/kuamshwa kingono hutokea kwa kiwango kinachofanana kwa wanawake vijana wenye afya njema na wanawake wazee. Hata hivyo, mabadiliko katika homoni za ngono wakati mwingine yanaweza kusababisha kupungua kwa hamu ya ngono. Kwa mfano, kwa wanawake vijana wenye afya njema, kushuka kwa ghafla kwa viwango vya homoni za ngon, kama kunavyoweza kutokea katika wiki chache za kwanza baada ya kujifungua, kunaweza kusababisha kupungua kwa hamu ya ngono. Kwa wanawake wa umri wa kati na wazee, hamu ya ngono inaweza kupungua, lakini uhusiano wa moja kwa moja kati ya kupungua huko na homoni haujathibitishwa.

Kupungua kwa estrojeni kunakotokea wakati wa kukoma hedhi kunaweza kusababisha ugonjwa wa mfumo wa mkojo-uzazi unaohusiana na kukoma hedhi (ambao huathiri uke, vulva, na njia ya mkojo). Katika ugonjwa huu, tishu za uke zinaweza kuwa nyembamba, kavu, na kuwa na ugumu wa kunyooshwa. Kwa sababu hiyo, kujamiiana kunaweza kutoridhisha au kusababishe maumivu. Wanawake wenye ugonjwa huu wanaweza pia kuhisi hitaji la haraka la kukojoa (msukumo wa kukojoa) na kupata maambukizi ya mara kwa mara ya njia ya mkojo. Dalili hizi hupunguza hamu ya wanawake ya kushiriki ngono.

Msisimko wa kingono usiotosha pia unaweza kuchangia tatizo la kuvutiwa/kuamshwa kingono.

Je, Ulijua...

  • Wanawake vijana wenye afya njema wana uwezekano sawa wa kuwa na tatizo la kuvutiwa/kuamshwa kingono kama wanawake wazee.

Utambuzi wa Tatizo la Kuamsha/Tamaa ya Ngono

  • Utathmini wa daktari kulingana na kigezo mahususi

Madaktari hutegemea historia ya mwanamke, maelezo yake ya tatizo, na vigezo vya Mwongozo wa Utambuzi na Takwimu wa Matatizo ya Akili, Toleo la Tano (DSM-5), uliotolewa na Chama cha Saikolojia cha Marekani, katika kutambua tatizo la kuvutiwa/kuamshwa kingono. Vigezo hivi vinahitaji kupungua au kutokuwepo kwa angalau vitu vitatu kati ya vifuatavyo:

  • Hamu ya kushiriki shughuli za ngono

  • Kuanzisha shughuli za ngono na mwitikio kwa uanzishaji wa mwenzi

  • Msisimko au raha wakati wa karibu shughuli zote za ngono

  • Ndoto au mawazo ya ngono au ya kimapenzi

  • Hisia za kimwili katika sehemu za siri au sehemu nyingine za mwili wakati wa shughuli za ngono

  • Hamu au msisimko unaotokana na vichocheo vya ngono—vya maandishi, vya mazungumzo, au vya kuona

Ni lazima dalili hizi ziwepo kwa angalau miezi 6 na lazima zisababishe tatizo kubwa kwa mwanamke.

Uchunguzi wa nyonga hufanywa ikiwa kupenyeza wakati wa shughuli za ngono husababisha maumivu.

Matibabu ya Tatizo la Kuamsha/Tamaa ya Ngono

  • Matibabu ya chanzo cha tatizo, panapowezekana

  • Hatua za jumla

  • Tiba za kisaikolojia

  • Dawa

Huduma kwa wanawake wenye tatizo la kuvutiwa/kuamshwa kingono husimamiwa vyema na timu ya wataalamu wa afya wa taaluma mbalimbali. Timu hiyo inaweza kujumuisha madaktari wa huduma ya msingi au wataalamu wa magonjwa ya wanawake, washauri wa ngono, wataalamu wa maumivu, wataalamu wa tiba ya kisaikolojia, na wataalamu wa tiba ya mazoezi.

Mojawapo ya hatua muhimu zaidi ni kumsaidia mwanamke kutambua na kumweleza mwenzi wake ni nini humchangamsha kingono. Wanawake wanaweza kuhitaji kuwakumbusha wenzi wao kwamba wanahitaji shughuli za maandalizi—zinazoweza kuhusisha kugusana au zisizohusisha kugusana—ili kujiandaa kwa shughuli za ngono. Kwa mfano, wanaweza kutaka kuzungumza kwa karibu, kutazama video ya kimapenzi au ya ngono, au kucheza pamoja. Wanawake wanaweza pia kutamani kubusiana, kukumbatiana, au kukaa karibu kwa kugusana. Wanaweza kuhitaji utangulizi zaidi au wa aina tofauti (mwenzi kugusa sehemu mbalimbali za mwili, kisha matiti au sehemu za siri) kabla ya kuendelea na kujamiiana au shughuli nyingine za ngono zinazohusisha kupenyeza. Wanandoa wanaweza kujaribu mbinu au shughuli mbalimbali (ikiwemo ndoto za kimapenzi na vifaa vya ngono) ili kubaini vichocheo vinavyofaa zaidi.

Hatua zinazopendekezwa kutibu matatizo ya ngono kwa ujumla pia zinaweza kusaidia kuongeza hamu ya ngono. Kwa mfano, kuondoa vikengeushi (kama televisheni chumbani) na kuboresha faragha na hisia ya usalama kunaweza kusaidia. Madaktari wanaweza kupendekeza matumizi ya vichocheo vya ngono vyenye nguvu (kama video) pamoja na mawazo ya kimapenzi.

Matibabu mara nyingi hulenga mambo yanayochangia ukosefu wa hamu ya ngono na mwitikio duni kwa msisimko wa kingono, kama mfadhaiko, kujithamini kwa kiwango cha chini, na matatizo ya uhusiano.

Tiba za kisaikolojia, hasa tiba ya utambuzi inayotegemea umakinifu, zinaweza kuwasaidia baadhi ya wanawake. Umakinifu unahusisha kuzingatia kile kinachotokea katika wakati wa sasa. Tiba ya utambuzi inayotegemea umakinifu, ambayo mara nyingi hufanywa katika vikundi vidogo, huchanganya mbinu za uangalifu na tiba ya utambuzi-tabia. Inaweza kusaidia kuboresha kuamshwa kingono, kufikia kilele, na hamu ya kushiriki ngono.

Madaktari wanaweza kuwaelekeza wanawake wenye tatizo la kuvutiwa/kuamshwa kingono kwa mshauri au mtaalamu wa ngono, au kwa mtaalamu wa tiba ya kisaikolojia.

Matibabu mengine hutegemea chanzo cha tatizo. Kwa mfano, ikiwa dawa zinachangia tatizo, zinaweza kusimamishwa inapowezekana.

Matibabu ya hali zinazochangia

Ikiwa mwanamke ana maumivu ya ngono, matibabu madhubuti ya maumivu yanaweza kusaidia kutatua tatizo la ukosefu wa hamu au kuamshwa kingono. Hali hii inaweza kusababishwa na ugonjwa wa mfumo wa mkojo-uzazi unaohusiana na kukoma hedhi, vulvodynia (maumivu sugu karibu na vulva), ugonjwa wa levator ani, maambukizi ya nyonga, fibriosisi, endometriosisi, au sababu nyingine.

Tiba ya Testosteroni

Taarifa chache zinapatikana kuhusu ufanisi na usalama wa muda mrefu wa testosterone (inapotumiwa kwa kumezwa au kama krimu ya kupakwa kwenye ngozi). Inapotumiwa kwa muda mfupi, testosterone inayotumika pamoja na estrojeni (na kwa kawaida progestojeni) inaweza kuwa na manufaa kwa wanawake waliokoma hedhi wenye tatizo la kuvutiwa/kuamshwa kingono. Hata hivyo, matumizi ya testosterone kwa madhumuni haya bado huchukuliwa kuwa ya majaribio, na wanawake wanapaswa kujadili faida na hatari zake na daktari.

Hakuna dawa za testosterone zinazotengenezwa mahususi kwa wanawake kwa agizo la daktari nchini Marekani. Hata hivyo, baadhi ya madaktari huagiza krimu ya ngozi iliyochanganywa maalum. Wanawake wanapaswa kutibiwa kwa testosterone na madaktari wenye mafunzo na uzoefu maalum katika matatizo ya ngono ya wanawake pekee.

Ikiwa testosterone itaagizwa, daktari humfafanulia mwanamke kuwa hakuna hakikisho la ufanisi wake pamoja na hatari zinazoweza kuhusishwa na tiba hiyo. Madaktari hufanya vipimo vya damu ili kukagua utendaji wa figo na ini, pamoja na kupima viwango vya lipidi, kabla ya kuanza matumizi ya testosterone. Testosterone haiagizwi iwapo matokeo ya vipimo yanaonyesha kuwa mwanamke yuko katika hatari ya matatizo ya ini au dyslipidemia (kwa mfano, kiwango cha juu sana cha LDL, kinachojulikana kama lehemu “mbaya”). Ikiwa testosterone itaagizwa, madaktari hupanga ziara za ufuatiliaji wa mara kwa mara ili kuchunguza madhara yanayoweza kutokea, kama chunusi, hirsutism (ukuaji wa nywele kupita kiasi), na virilization (kujitokeza kwa sifa za kiume).

Vipimo vingine

Flibanserin inaweza kutumika kwa wanawake ambao bado hawajakoma hedhi wenye tatizo la kuvutiwa/kuamshwa kingono. Hata hivyo, ushahidi kuhusu ufanisi na usalama wake bado ni mdogo.

Bremelanotide hutumika kutibu kupungua kwa hamu ya ngono (libido) kwa wanawake. Ni dawa ya sindano inayotolewa angalau dakika 45 kabla ya shughuli ya ngono inayotarajiwa.

Vifaa kama vifaa vya mtetemo (vibrator) au vifaa vya kufyonza kisimi vinaweza kusaidia, lakini kuna ushahidi mdogo wa kuthibitisha ufanisi wake. Bidhaa nyingi kati ya hizi zinapatikana bila agizo la daktari na vinaweza kujaribiwa.