Muda wa kuanza vyakula halisi hutegemea mahitaji na utayari wa mtoto. Kwa ujumla, watoto huhitaji vyakula halisi wanapohitaji chanzo chenye mkusanyiko mkubwa wa kalori kuliko maziwa ya mama au fomula. Hali hii hutambuliwa mtoto anapomaliza chupa na kushiba lakini akarudi kuwa na njaa baada ya saa 2 au 3, au anapotumia zaidi ya aunsi 40 (takriban mililita 1200) za fomula kwa siku. Hii hutokea mara nyingi mtoto anapokuwa na umri wa miezi 4 hadi 6. Dalili nyingine za utayari wa kula vyakula vigumu ni pamoja na udhibiti mzuri wa kichwa na shingo, uwezo wa kukaa wima kwa msaada, kuonyesha hamu ya chakula, kufungua mdomo anapopewa chakula kwa kijiko, na kumeza badala ya kukisukuma nje. Watoto wengi huanza kuonyesha dalili hizi wanapofikisha umri wa miezi 6.
Watoto wengi hula vyakula halisi baada ya kunyonyeshwa au kulishwa kwa chupa, jambo linalotosheleza hitaji lao la kunyonya na kupunguza njaa haraka. Kutanguliza vyakula vigumu kabla ya miezi 4 ya umri hakupendekezwi. Watoto walio chini ya miezi 4 hawahitaji vyakula halisi kwa lishe, hawawezi kuvimeza kwa urahisi, na hawapaswi kulazimishwa kula kwa kijiko au kwa kuchanganya chakula kwenye chupa.
Vyakula vya watoto wachanga ni pamoja na nafaka za aina moja (kama nafaka ya mchele iliyoimarishwa kwa chuma) na matunda, mboga, na nyama zilizosagwa. Kwa sasa, madaktari hawaoni tena mpangilio wa kuanzisha vyakula hivi kuwa jambo muhimu. Wakati wa kuanzisha chakula kipya, inaweza kuchukua majaribio kadhaa kwa wiki kadhaa kabla mtoto kukikubali; wazazi hawapaswi kukata tamaa baada ya jaribio la kwanza au la pili.
Chakula kinapaswa kutolewa kwa kijiko ili mtoto ajifunze mbinu mpya ya kula. Kufikia miezi 6 hadi 9, watoto wengi wanaweza kushika chakula na kukipeleka mdomoni, na wanapaswa kuhimizwa kujilisha. Vyakula vya nyumbani vilivyosagwa ni vya gharama nafuu kuliko vya kuuzwa na hutoa lishe ya kutosha. Hata hivyo, maandalizi ya kibiashara ya karoti, viazisukari, tanipu, mboga za majani, na mchicha hupendekezwa kwa watoto walio chini ya mwaka 1 kwa kuwa hukaguliwa kwa kiwango cha nitrati. Viwango vya juu vya nitrati vinaweza kusababisha methemoglobinemia (hali inayoathiri uwezo wa damu kubeba oksijeni) kwa watoto wadogo, hasa kwenye mboga zilizopandwa kwa maji yaliyochafuliwa na mbolea.
Ingawa watoto hupendelea ladha tamu, sukari si kirutubisho muhimu na inapaswa kutolewa kwa kiasi kidogo sana au kuepukwa. Vyakula vitamu vya watoto havina faida ya lishe. Juisi ni chanzo duni cha lishe, huchangia matundu ya meno, na inapaswa kupunguzwa hadi aunsi 4 hadi 6 kwa siku au kuepukwa kabisa.
Vyakula vinavyopaswa kuepukwa ni pamoja na:
Asali (hadi mtoto afikishe mwaka 1), kwa sababu inaweza kuwa na chembe za Clostridium botulinum ambazo si hatari kwa watoto wakubwa na watu wazima lakini zinaweza kusababisha ubotuli kwa watoto wachanga.
Vyakula vinavyoweza kusababisha kukabwa au kuvutwa kwenye mapafu kwa urahisi (hadi umri wa miaka 2 au 3), kama karanga au maharagwe mazima, pipi ngumu, soya, bisi, hot dog, nyama (isipokuwa iwe imesagwa), na zabibu (isipokuwa ziwe zimekatwa vipande vidogo sana).
Watoto wachanga wanaweza kupata mizio ya vyakula. Iwapo mtoto atapewa vyakula vingi vipya kwa kipindi cha muda mfupi, itakuwa vigumu kubaini ni kipi kimesababisha mzio. Kwa sababu hiyo, wazazi wanapaswa kuanzisha chakula kipya chenye kiungo kimoja kila baada ya siku 3 hadi 5. Baada ya kubainika kuwa chakula kimevumiliwa, chakula kingine kinaweza kuanzishwa.
Ili kuzuia mizio ya chakula, wazazi wengi huepuka vyakula vinavyosababisha mzio kama mayai, siagi ya karanga, samaki, samakigamba, stroberi, na ngano. Hata hivyo, ushahidi wa hivi karibuni unaonyesha kuwa kuanzisha vyakula hivi baada ya miezi 4 lakini kabla ya mwisho wa mwaka wa kwanza kunaweza kusaidia kupunguza hatari ya mizio ya chakula. Ingawa ushahidi huu si wa mwisho, kwa watoto wengi walio na miezi 4 au zaidi, hakuna haja ya kuchelewesha kuanzishwa kwa chakula chochote halisi. Hata hivyo, ni muhimu kuanzisha chakula kipya kimoja tu kila baada ya siku 3 hadi 5 ili kuhakikisha kinavumiliwa. Ushahidi wa sasa unapendekeza watoto wapewe vyakula vyenye karanga baada ya miezi 4 lakini kabla ya mwisho wa mwaka wa kwanza, kwa kuwa kuchelewesha kunaweza kuongeza hatari ya mzio wa karanga. Hata watoto wenye eksema kali, mzio wa mayai, au vyote viwili wanapaswa kuanzishwa vyakula vyenye karanga vinavyofaa umri mapema (miezi 4 hadi 6), ili kupunguza hatari ya kupata mzio wa karanga mradi vipimo fulani vya damu na vya ngozi vinaonyesha kuwa ni salama. Wazazi wanapaswa kushauriana na daktari wa watoto kuhusu lini na jinsi ya kuanzisha vyakula mbalimbali halisi.
Kuanzia au baada ya umri wa mwaka 1, watoto wanaweza kuanza kunywa maziwa ya ng’ombe kamili. Wakiwa na umri wa miaka 2, watoto wanaweza kuanza kunywa maziwa yenye mafuta kidogo kwa kuwa lishe yao hufanana na ya familia nzima. Ulaji wa maziwa kwa watoto wadogo unapaswa kupunguzwa hadi aunsi 16 hadi 24 kwa siku. Watoto wanaokunywa maziwa mengi kupita kiasi wanaweza kukosa virutubisho vingine muhimu na kupata upungufu wa madini ya chuma.
Kufikia umri wa takriban mwaka 1, kasi ya ukuaji hupungua kwa kawaida. Kwa hiyo, watoto huhitaji chakula kidogo zaidi na wanaweza kukataa kula katika baadhi ya milo. Ili kutathmini kiasi ambacho mtoto anakula, wazazi wanapaswa kuangalia jumla ya chakula alichokula kwa kipindi cha wiki nzima, badala ya kuzingatia mlo mmoja au siku moja pekee. Kutokula chakula halisi cha kutosha huwa tatizo pale tu watoto wanaposhindwa kufikia viwango vinavyotarajiwa vya uzito kwa maendeleo ya kawaida.
(Angalia pia Muhtasari wa Ulishaji wa Watoto Waliozaliwa Karibuni na wachanga.)