Tatizo la ugonjwa wa pedofilia una sifa ya mawazo, misukumo, au tabia za kingono zinazorudiwa mara kwa mara na zenye nguvu, zinazohusisha watoto (kwa kawaida wenye umri wa miaka 13 au chini).
Watu wenye mwelekeo wa pedofilia wanaweza kuvutiwa na wavulana wadogo, wasichana wadogo, au wote wawili, na wanaweza kuvutiwa na watoto pekee au na watoto pamoja na watu wazima.
Madaktari hutambua tatizo la pedofilia pale watu wanapopata mfadhaiko mkubwa au wanaposhindwa kufanya kazi vizuri kwa sababu ya mvuto wao kwa watoto au wanapotekeleza misukumo yao.
Matibabu huhusisha tiba ya kisaikolojia ya muda mrefu na dawa zinazobadilisha hamu ya ngono na kupunguza viwango vya testosteroni .
(Tazama pia Muhtasari wa Kutelekezwa na Kunyanyaswa kwa Watoto.)
Pedofilia ni aina ya parafilia. Kwa sababu husababisha madhara kwa wengine, inachukuliwa kuwa tatizo la ugonjwa.
Iwapo mvuto au ushiriki wa kingono kati ya watu 2 utachukuliwa kuwa ni tatizo la pedofilia hutegemea umri wa watu wanaohusika. Katika jamii za nchi za magharibi, utambuzi wa tatizo la ugonjwa wa pedofilia unahitaji mtu awe na umri wa miaka 16 au zaidi na awe angalau miaka 5 zaidi ya mtoto anayehusishwa na mawazo au vitendo vya kingono. Hata hivyo, ushiriki wa kingono kati ya kijana mkubwa (miaka 17 hadi 18) na mtoto wa miaka 12- au 13 huenda usichukuliwe kuwa ni tatizo. Vigezo vya umri vinavyotumika kutambua wakati shughuli hiyo inachukuliwa kuwa uhalifu vinaweza kutofautiana katika tamaduni mbalimbali.
Ingawa sheria za majimbo hutofautiana nchini Marekani, kwa ujumla sheria hiyo humchukulia mtu mwenye umri wa zaidi ya miaka 18 kuwa anafanya kosa la ubakaji wa kisheria ikiwa mhasiriwa ana umri wa miaka 16 au chini ya hapo. Kesi za ubakaji wa kisheria mara nyingi hazikidhi ufafanuzi wa kitabibu wa pedofilia, jambo linaloonyesha hali ya kuchagua kikomo cha umri mahususi bila msingi madhubuti katika ufafanuzi wa kitabibu au kisheria. Katika maeneo mengi (ikiwa ni pamoja na katika baadhi ya majimbo nchini Marekani), watoto wenye umri mdogo wa miaka 12 hadi 14 wanaweza kuoa kisheria, jambo linalozidi kutatiza ufafanuzi wa pedofilia na ubakaji wa kisheria.
Pedofilia ni ya kawaida zaidi miongoni mwa wanaume kuliko wanawake.
Watu wenye mwelekeo wa pedofilia wanaweza kuvutiwa na wavulana wadogo, wasichana wadogo, au wote wawili. Haijulikani wazi kama wasichana au wavulana wana uwezekano mkubwa wa kuwa wahasiriwa wa pedofilia, ingawa kwa ujumla wasichana wanaonekana kuwa na uwezekano mkubwa zaidi wa kuwa wahasiriwa wa unyanyasaji wa kingono kwa ujumla.
Kwa kawaida, mtu mzima huyo humfahamu mtoto na anaweza kuwa mwanafamilia, mzazi wa kambo, au mtu mwenye mamlaka (kama vile mwalimu au mkufunzi). Baadhi yao huvutiwa tu na watoto waliomo ndani ya familia zao wenyewe (ndugu wa damu). Baadhi ya watu wenye mwelekeo wa pedofilia huvutiwa tu na watoto, mara nyingi wa umri mahususi au hatua fulani ya ukuaji. Wengine huvutiwa na watoto pamoja na watu wazima.
Kuangalia au kugusa kwa ujumla huonekana kuwa jambo la kawaida zaidi kuliko kugusa sehemu za siri au kufanya ngono.
Walawiti wanaowadhulumu watoto wanaweza kutumia nguvu au kulazimisha watoto kushiriki vitendo vya kingono na wanaweza kutishia kumdhuru mtoto au wanyama kipenzi wa mtoto ikiwa mtoto atamwambia mtu yeyote. Wengi wa watu hawa wenye mwelekeo wa pedofilia wana ugonjwa wa utu wa kupinga jamiii.
Watu wengi wenye mwelekeo wa pedofilia wana au wanapata ugonjwa wa matumizi ya vilevi au utegemezi na unyogovu. Mara nyingi hutoka katika familia zisizo na utulivu, na migogoro ya ndoa ni ya kawaida. Wengi wao walinyanyaswa kingono walipokuwa watoto.
Utambuzi wa Tatizo la Ugonjwa wa Pedofilia
Tathmini ya daktari, kulingana na vigezo vya kawaida vya uchunguzi wa magonjwa ya akili
Madaktari hutambua ugonjwa wa pedophilia wakati
Watu wamekuwa na mawazo, misukumo, au tabia zinazochochea msisimko wa kingono kwa mtoto au watoto ambazo hujirudia (kwa kawaida wakiwa na umri wa miaka 13 au chini ya hapo).
Watu huhisi mfadhaiko mkubwa au hushindwa kufanya kazi zao vizuri (kazini, katika familia, au katika mahusiano ya kijamii), au wamefanya vitendo kulingana na misukumo yao.
Watu wana umri wa miaka 16 au zaidi na wana umri mkubwa kwa angalau miaka 5 kuliko mtoto anayelengwa katika mawazo au tabia hizi. (Isipokuwa kama ni kijana mkubwa mwenye uhusiano endelevu na mtoto wa miaka 12- au 13.)
Amekuwa na hali hiyo kwa kipindi cha miezi 6 au zaidi.
Matibabu ya Tatizo la Ugonjwa wa Pedofilia
Tiba ya kisaikolojia ya mtu binafsi na/au ya kikundi
Matibabu ya matatizo mengine
Dawa
Ugonjwa wa Pedofilia unaweza kutibiwa kwa tiba ya kisaikolojia ya mtu binafsi au kikundi cha muda mrefu na dawa zinazopunguza viwango vya testosteroni na hivyo kupunguza hamu ya ngono. Dawa hizi zinajumuisha leuprolide na medroxyprogesterone acetate. Watu ni sharti watoe idhini yao ya kutumia dawa hizi, na madaktari hufanya vipimo vya damu mara kwa mara ili kufuatilia athari za dawa kwenye utendaji kazi wa ini, pamoja na vipimo vingine (ikiwa ni pamoja na vipimo vya uwiano wa mifupa na vipimo vya damu ili kupima viwango vya testosteroni).
Matokeo ya matibabu hutofautiana. Matokeo huwa bora zaidi wakati ushiriki ni wa hiari na mtu hupata mafunzo ya stadi za kijamii pamoja na matibabu ya matatizo mengine kama matumizi mabaya ya dawa au mfadhaiko. Matibabu yanayotafutwa tu baada ya kukamatwa kwa kosa la jinai na kuchukuliwa hatua za kisheria yanaweza kuwa na ufanisi mdogo.
Kuwaweka watu wenye mwelekeo wa pedofilia gerezani au katika taasisi nyingine, hata kwa muda mrefu, hakubadilishi tamaa au mawazo yao ya kingono. Hata hivyo, baadhi ya watu walioko gerezani wenye mwelekeo huo ambao wanajitolea kwa matibabu ya muda mrefu yanayosimamiwa (mara nyingi yakihusisha dawa) wanaweza kujizuia na vitendo hivyo na kurejeshwa katika jamii.
Dawa
Medroksiprojesteroni asetati, ambayo hudungwa ndani ya misuli
Makundi mengine ya dawa
Medroksiprojesteroni (projestini) inafanana na homoni ya kike ya projesteroni. Chaguo jingine ni leuprolide. Dawa zote mbili huzuia tezi ya pituitari kutuma ishara kwa korodani ili kuzalisha testosteroni. Hivyo basi kupunguza viwango vya testosteroni na hamu ya ngono. Asetati ya saiproterone ni dawa nyingine inayopunguza viwango vya testosteroni (ili kudumishwa katika kiwango cha kawaida cha wanawake), lakini haipatikani nchini Marekani. Madaktari hufanya vipimo vya damu mara kwa mara ili kufuatilia athari za dawa hizi kwenye utendaji kazi wa ini, pamoja na vipimo vingine (ikiwa ni pamoja na vipimo vya uwiano wa mifupa na vipimo vya damu ili kupima viwango vya testosteroni). Haijulikani wazi jinsi dawa hizi zinavyofaa kwa wanawake wenye mwelekeo huo wa pedofilia.
Dawa za kupunguza mfadhaiko zinazoitwa vizuizi vya uchaguzi wa kuchukua tena serotonini (SSRIs) pia zinaweza kusaidia. Huenda zikasaidia kudhibiti misukumo na mawazo ya ngono. Pia hupunguza hamu ya ngono na inaweza kusababisha kushindwa kusimama kwa uume.
Matibabu ya dawa hufanya kazi vizuri zaidi yanapounganishwa na tiba ya kisaikolojia (hasa tiba ya tabia-tambuzi) pamoja na mafunzo ya ujuzi wa kijamii.