Matibabu ya Kupunguza Makali ya Virusi vya UKIMWI (VVU)

NaEdward R. Cachay, MD, MAS, Mayo Clinic, Arizona
Imekaguliwa naChristina A. Muzny, MD, MSPH, Division of Infectious Diseases, University of Alabama at Birmingham
Imepitiwa/Imerekebishwa May 2024 | Imebadilishwa Apr 2025
v44314771_sw

Dawa za kupunguza makali ya virusi zinazotumika kutibu maambukizi ya virusi vya UKIMWI (VVU) hulenga kufanya yafuatayo:

  • Kupunguza kiwango cha RNA ya VVU (idadi ya virusi) katika damu hadi kufikia kiwango kisichoweza kugundulika

  • Kurejesha idadi ya seli za CD4 hadi viwango vya kawaida

Madarasa kadhaa ya dawa za kupunguza makali ya VVU hutumiwa kwa pamoja kutibu maambukizi ya VVU. Dawa hizi huzuia VVU kuingia katika seli za binadamu au huzuia shughuli za mojawapo ya vimeng’enya ambavyo VVU huhitaji ili kujizalisha ndani ya seli za binadamu na/au kuunganisha nyenzo zake za kijenetiki katika DNA ya binadamu.

Dawa hizo zimegawanywa katika makundi kulingana na jinsi zinavyofanya kazi dhidi ya VVU:

  • Vizuizi vya reverse transcriptase huzuia kimeng’enya cha reverse transcriptase cha VVU kubadilisha RNA ya VVU kuwa DNA. Kuna aina tatu za dawa hizi: nukleosidi, nukleotidi, na zisizo za nukleosidi.

  • Vizuizi vya protease huzuia kimeng’enya cha protease kuamilisha protini fulani ndani ya virusi vipya vinavyozalishwa. Matokeo yake ni virusi vya VVU ambavyo havijakomaa, vyenye kasoro, na visivyoweza kuambukiza seli mpya.

  • Vizuizi vya kuingia (fusion) huzuia VVU kuingia kwenye seli. Ili kuingia kwenye seli ya binadamu, VVU lazima vijifunge kwenye kipokezi cha CD4 na kipokezi kingine kimoja, kama vile kipokezi cha CCR-5. Aina moja ya vizuizi vya kuingia, vizuizi vya CCR-5, hufunga kipokezi cha CCR-5 na hivyo kuzuia VVU kuingia kwenye seli za binadamu.

  • Vizuizi vya baada ya kushikamana pia huzuia VVU kuingia kwenye seli, lakini kwa njia tofauti na vizuizi vya fusion. Dawa hizi hutumiwa hasa kwa maambukizi ya VVU ambayo yamekuwa sugu kwa dawa nyingine kadhaa.

  • Vizuizi vya integrase huzuia DNA ya VVU kuunganishwa na DNA ya binadamu.

  • Vizuizi vya kushikamana huzuia VVU kushikamana na seli T za mwili na seli nyingine za kinga; hivyo, virusi haviwezi kuingia kwenye seli hizo.

Sehemu za Kazi ya Dawa kwenye Mzunguko wa Maisha wa VVU

Dawa zilizotumika kutibu maambukizi ya VVU zilitengenezwa kulingana na mzunguko wa maisha wa VVU. Dawa hizi huzuia VVU kuingia kwenye seli lengwa au huzuia vimeng’enya vitatu (reverse transcriptase, integrase, na protease) ambavyo virusi hutumia kujizalisha.

  1. 1. VVU huambatisha na kupenya kiini chake lengwa kwanza. Makundi yote ya dawa zinazofanya kazi dhidi ya VVU katika hatua hii huitwa vizuizi vya kuingia, na yanajumuisha vizuizi vya kushikamana, vizuizi vya baada ya kushikamana, na vizuizi vya fusion.

  2. 2. VVU hutoa RNA, msimbo wa jenetiki wa virusi, ndani ya seli. Ili virusi viweze kurudufiwa, ni lazima RNA yake ibadilishwe kuwa DNA. Dawa zinazoitwa vizuizi vya reverse transcriptase zinaweza kuzuia kimeng’enya cha reverse transcriptase cha VVU kubadilisha RNA ya VVU kuwa DNA.

  3. 3. DNA ya virusi huingia kwenye kiini cha seli.

  4. 4. Kwa msaada wa kimeng'enya kinachoitwa integrase (pia kinachozalishwa na VVU), DNA ya virusi huunganishwa na DNA ya seli. Katika hatua hii, dawa ziitwazo vizuizi vya integrase huzuia DNA ya VVU kuunganishwa na DNA ya binadamu.

  5. 5. DNA ya seli iliyoambukizwa sasa hutoa RNA ya kirusi pamoja na protini zinazohitajika ili kukusanya VVU mpya.

  6. 6. Virusi mpya hukusanywa kutoka kwenye RNA na visehemu vifupi vya protini.

  7. 7. Kirusi husukuma (huchipuka) kupitia utando wa seli, hujifunga kwenye kipande cha utando wa seli na kujibana kutoka kwenye seli iliyoambukizwa.

  8. 7.5 na 8. Ili kuweza kuambukiza seli nyingine, ni lazima virusi vilivyochipuka vikomae. Kimeng’enya kingine cha VVU (protease ya VVU) ni muhimu katika mchakato wa ukomavu wa virusi. Katika hatua hii, dawa zinazoitwa vizuizi vya protease zinaweza kuzuia kukomaa kwa virusi vya VVU.

Dawa hizi huzuia VVU kujizalisha ndani ya seli na hupunguza kwa kiasi kikubwa kiwango cha VVU katika damu ndani ya siku hadi wiki kadhaa. Wakati uzalishaji wa virusi unapunguzwa vya kutosha, uharibifu wa limfosaiti za CD4+ husababishwa na VVU hupungua, na idadi ya CD4 huanza kuongezeka. Kutokana na hayo, sehemu kubwa ya uharibifu wa mfumo wa kinga unaosababishwa na VVU inaweza kurekebishwa. Madaktari hutambua mabadiliko haya kwa kupima idadi ya CD4, ambayo huanza kurejea kwenye viwango vya kawaida ndani ya wiki hadi miezi kadhaa. Idadi ya CD4 huendelea kuongezeka kwa miaka kadhaa, lakini kwa kasi ndogo zaidi.

Utambuzi wa mapema wa maambukizi ya VVU ni muhimu kwa sababu huwawezesha madaktari kutambua maambukizi kabla idadi ya seli za CD4 haijapungua sana. Kadiri watu wanavyoanza kutumia dawa za kupunguza makali ya virusi mapema, ndivyo idadi ya CD4 inavyoongezeka haraka zaidi na kufikia viwango vya juu zaidi.

Je, Ulijua...

  • Dawa za kutibu VVU hufanya kazi ipasavyo iwapo tu watu watazitumia bila kusitisha. Kukosa dozi huruhusu virusi kujizalisha na kuwa sugu dhidi ya dawa.

VVU huanza kuwa sugu dhidi ya dawa yoyote kati ya hizi ikiwa itatumika peke yake. Hali ya kuwa sugu huanza ndani ya siku chache hadi miezi kadhaa, kulingana na aina ya dawa na virusi. VVU huwa sugu kwa dawa kutokana na mabadiliko ya kijenetiki yanayotokea wakati wa kujizalisha.

Matibabu huwa na ufanisi zaidi pale dawa mbili au zaidi zinapotumika kwa pamoja. Mchanganyiko huu wa dawa huitwa tiba mchanganyiko ya kupunguza makali ya virusi (cART). cART hutumiwa kwa sababu

  • Mchanganyiko wa dawa hupunguza kiwango cha VVU katika damu kwa ufanisi zaidi kuliko dawa moja.

  • Pia husaidia kuzuia virusi visiwe sugu kwa dawa.

  • Baadhi ya dawa za VVU, kama ritonavir, huongeza viwango vya damu vya dawa nyingine za VVU (ikiwa ni pamoja na vizuizi vingi vya protease) kwa kupunguza kasi ya kuondolewa mwilini, hivyo kuongeza ufanisi wake.

cART inaweza kuongeza idadi ya CD4 kwa watu wenye VVU, na hivyo kuimarisha mfumo wa kinga, na kuongeza muda wa maisha.

Athari mbaya za dawa za matibabu ya kupunguza makali ya virusi vya UKIMWI

Hata hivyo, mchanganyiko wa dawa za kupunguza makali ya virusi unaweza kusababisha madhara yasiyopendeza na wakati mwingine makubwa. Madaktari wanaweza kuzuia matatizo mengi makubwa (kama upungufu wa damu, homa ya ini, matatizo ya figo, na kongosho) kwa kufanya uchunguzi wa mara kwa mara na vipimo vya damu. Vipimo hivi hutambua madhara mapema na kuwawezesha madaktari kubadilisha dawa inapohitajika. Kwa watu wengi, inawezekana kupata mchanganyiko wa dawa wenye madhara madogo.

Umetaboli wa mafuta unaweza kuvurugika, hasa kutokana na matumizi ya vizuizi vya protease. Yafuatayo yanaweza kusababisha:

  • Mafuta yanaweza kujikusanya tumboni na kifuani kwa wanawake (unene wa kati), huku yakipungua usoni, mikononi, na miguuni.

  • Mwili hupunguza mwitikio kwa athari za insulini (hali inayojulikana kama upinzani wa insulini)

  • Viwango vya lehemu na trigliseridi (aina 2 za mafuta katika damu) huongezeka.

Mchanganyiko wa matatizo haya, unaoitwa ugonjwa wa kimetaboliki, huongeza hatari ya mshtuko wa moyo, kiharusi, na shida ya kumbukumbu.

Vipele (athari za ngozi) ni madhara ya kawaida ya dawa nyingi. Baadhi ya athari za ngozi zinaweza kuwa hatari sana, hasa zikisababishwa na nevirapine au abacavir.

Mitochondria, miundo ndani ya seli inayozalisha nishati, inaweza kuharibika wakati baadhi ya vizuizi vya nucleoside reverse transcriptase vinapotumika. Madhara yanaweza kujumuisha upungufu wa damu, maumivu ya miguu kutokana na uharibifu wa neva (neuropathy), uharibifu wa ini unaoweza kuendelea hadi ini lishindwe kufanya kazi kabisa, na uharibifu wa moyo unaoweza kusababisha moyo kushindwa kufanya kazi. Dawa tofauti hutofautiana katika uwezekano wa kusababisha madhara haya.

Uzito wa mifupa unaweza kupungua wakati wa kutumia cART, na kusababisha osteopenia au osteoporosis. Watu wengi walio na hali hizi hawana dalili, lakini wako kwenye hatari kubwa ya kuvunjika mfupa.

Ugonjwa wa uchochezi wa urekebishaji wa kinga

Ugonjwa wa uchochezi wa kurejesha kinga (IRIS) unaweza kutokea wakati cART inapoanza kufanya kazi vizuri.

Katika IRIS, dalili za maambukizi huzidi au hujitokeza kwa mara ya kwanza kwa sababu mfumo wa kinga huimarika, na hivyo kuongeza uvimbe kwenye maeneo ya maambukizi. Dalili zinaweza kuongezeka kwa sababu mabaki ya virusi vilivyokufa hubaki na kuchochea mwitikio wa kinga.

Kuna aina mbili za ugonjwa huu:

  • IRIS ya paradoksia, ambayo husababisha kuongezeka kwa dalili za maambukizi yaliyokwisha tambuliwa

  • IRIS isiyotambuliwa, ambayo ni mwonekano wa kwanza wa dalili za mambukizi ambayo madaktari hawakutambua awali

IRIS ya paradoksia hutokea mara nyingi katika miezi ya kwanza ya matibabu na kwa kawaida huisha yenyewe. Ikiwa hali haitulii, corticosteroids za muda mfupi mara nyingi husaidia. IRIS ya paradoksia huwa kali zaidi pale cART inapoanzishwa mapema sana baada ya kuanza kutibu maambukizi nyemelezi. Kwa baadhi ya maambukizi nyemelezi, cART hucheleweshwa hadi matibabu ya maambukizi hayo yayapunguze au kuyaondoa.

Kwa watu walio na IRIS isiyotambuliwa, madaktari hutibu maambukizi mapya nyemelezi kwa dawa za kuua vijidudu. Ikiwa dalili ni kali, corticosteroids pia hutumiwa. Kwa kawaida, cART huendelea hata IRIS isiyotambuliwa inapotokea. Isipokuwa pale maambukizi ya cryptococcal yanapohusisha ubongo. Katika hali hiyo, cART husitishwa kwa muda hadi maambukizi yadhibitiwe.

Mwingiliano na dawa za matibabu ya kupunguza makali ya virusi vya UKIMWI

Mwingiliano wa dawa unaweza kutokea kati ya dawa za kupunguza makali ya virusi au kati ya dawa hizi na dawa nyingine. Hivyo, ni muhimu watu kumjulisha daktari wao kuhusu dawa zote wanazotumia.

Mwingiliano huu unaweza kuongeza au kupunguza ufanisi wa dawa.

St. John’s wort, mmea wa dawa, haipaswi kutumiwa kwa sababu hufanya mwili uchakate kwa haraka zaidi vizuizi vya protease na vya reverse transcriptase visivyo vya nukliosidi na hivyo kupunguza ufanisi wake.

Matumizi ya dawa za matibabu ya kupunguza makali ya virusi vya UKIMWI

Matibabu ya kupunguza makali ya virusi hufanya kazi tu ikiwa dawa zinatumiwa kwa utaratibu uliopangwa. Kukosa dozi huwezesha virusi kujizalisha na kuwa sugu dhidi ya dawa.

Matibabu hayawezi kuondoa kirusi mwilini, ingawa kiwango cha VVU mara nyingi hupungua sana kiasi kwamba hakiwezi kugunduliwa katika damu au viowevu au tishu nyingine. Lengo la matibabu ni kufikia kiwango cha virusi kisichoweza kugundulika. Ikiwa matibabu yatasitishwa, kiwango cha VVU huongezeka, na idadi ya CD4 huanza kupungua.

Ni vyema kuanza matibabu haraka iwezekanavyo, hata kama mtu hana dalili na idadi ya CD4 bado iko juu ya 500 (kawaida huwa ni 500 hadi 1,000). Hapo awali, madaktari walisubiri hadi CD4 ishuke chini ya 500 kabla ya kuanza matibabu. Utafiti umeonyesha kuwa matibabu ya mapema hupunguza hatari ya matatizo na vifo vinavyohusiana na VVU/UKIMWI.

Kabla ya kuanza utaratibu wa matibabu, watu hufunzwa kuhusu umuhimu wa yafuatayo:

  • Kunywa dawa vile imeelekezwa

  • Kutoruka dozi yoyote

  • Kutumia dawa kwa maisha yao yote

Kunywa dawa vile imeelekezwa maisha yote sio rahisi. Baadhi ya watu huruka dozi au huacha kutumia dawa kwa muda (inayoutwa likizo ya dawa). Tabia hii ni hatari kwa sababu yanawezesha VVU kukuza upinzani dhidi ya dawa.

Kwa sababu kutumia dawa za VVU bila uendelevu mara nyingi husababisha usugu wa dawa, wataalamu wa afya hujaribu kuhakikisha kwamba watu wako tayari na wanaweza kufuata utaratibu wa matibabu. Ili kurahisisha ratiba ya dawa, mara nyingi madaktari huagiza tembe moja inayochanganya dawa mbili au zaidi, inayotumika mara moja kwa siku.

Matibabu yanaweza kusitishwa kwa muda ikiwa madhara ni makubwa au ikiwa kuna ugonjwa mwingine unaohitaji matibabu. Kusitisha dawa zote kwa wakati mmoja kwa kawaida ni salama. Dawa huanza tena baada ya kipimo kubadilishwa au dawa kubadilishwa, na madaktari kuthibitisha usalama. Abacavir ni tofauti. Ikiwa mtu alipata homa au vipele alipokuwa akitumia abacavir, dawa hiyo lazima isisitishwe kabisa. Kuitumia tena kunaweza kusababisha athari kali na hatari kwa maisha.

Kuuzuia maambukizi nyemelezi

Ikiwa idadi ya CD4 ni ndogo, dawa za kuzuia maambukizi nyemelezi huagizwa, kama ifuatavyo:

Maambukizi mengine

Dawa nyingine zinaweza kusaidia kupunguza udhaifu, kupungua uzito, na unene wa kati unaoweza kusababishwa na maambukizi ya VVU.

  • Megestrol na dronabinol (dawa inayotokana na bangi) huchochea hamu ya kula. Watu wengi huripoti kuwa bangi asilia ina ufanisi zaidi, na matumizi yake kwa madhumuni haya yameruhusiwa kisheria katika baadhi ya majimbo.

  • Iwapo wanaume wana viwango vya chini vya testosterone pamoja na uchovu, upungufu wa damu, na/au kupoteza misuli, wanaweza kupewa testosterone kwa sindano au kupitia viraka vya ngozi. Matibabu ya testosterone yanaweza kuongeza viwango vya testosterone na kupunguza dalili.

  • Homoni ya ukuaji na tesamorelin (dawa ya sindano inayochochea utolewaji wa homoni ya ukuaji) hupunguza unene wa kati unaoweza kusababishwa na VVU na matibabu yake.

Iwapo upinzani wa insulini utatokea, dawa zinazoongeza usikivu wa mwili kwa insulini zinaweza kusaidia. Iwapo viwango vya lehemu na triglyceridi katika damu vitaongezeka, dawa za kupunguza mafuta mwilini (statins) zinaweza kutumika kuvipunguza.

Taarifa Zaidi

Nyenzo zifuatazo za lugha ya Kiingereza zinaweza kuwa muhimu. Tafadhali kumbuka kuwa MWONGOZO hauwajibiki kwa maudhui ya nyenzo hizi.

  1. Office of AIDS Research: Maelezo kutoka Taasisi za Kitaifa za Afya (NIH), ikijumuisha kamusi ya maneno yanayohusiana na VVU na hifadhidata ya dawa

  2. The American Foundation for AIDS Research: Rasilimali kuhusu usaidizi wa utafiti wa UKIMWI, kinga dhidi ya VVU, elimu ya matibabu na utetezi

  3. Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC): Matibabu ya VVU kama Kinga: Taarifa kwa wagonjwa kuhusu tiba ya dawa za kupunguza makali ya virusi inayotumika kupunguza kiwango cha VVU mwilini, kudumisha mfumo wa kinga, na kuzuia magonjwa.