Homa ya ini B (homa ya ini aina ya B) husababisha ini kuvimba.
Watoto huambukizwa zaidi wakati wa kuzaliwa au mara chache baada ya kuzaliwa.
Watoto wenye dalili hupata manjano (jaundice), unyong'onyevu, na kusuasua kwa ukuaji na uzito (failure to thrive).
Utambuzi hufanyika kupitia vipimo vya damu.
Chanjo ya homa ya ini B na wakati mwingine globulini ya kinga (HBIG) hutolewa kwa watoto ili kuwalinda.
Watoto hawa wako kwenye hatari ya kupata matatizo ya ini ukubwani.
(Tazama pia Muhtasari wa Maambukizi kwa Watoto Wachanga na Muhtasari wa Homa ya Ini.)
Homa ya ini B ni aina ya virusi vya homa ya ini ambavyo watoto wachanga wanaweza kupata na husababisha wasiwasi mkubwa kwa watoto wachanga.
Maambukizi hutokea wakati wa uchungu wa uzazi au kujifungua ikiwa atagusana na damu au majimaji ya mama mwenye maambukizi. Hata hivyo, mtoto anaweza pia kuambukizwa baada ya kuzaliwa kupitia mate, kinyesi, mkojo, au maziwa ya mama.
Dalili za Maambukizi ya HBV kwa Watoto Waliozaliwa Karibuni
Watoto wengi wenye virusi vya homa ya ini B (HBV) hawana dalili wakati wa kuzaliwa lakini hubaki na virusi hivyo mwilini mwao.
Watoto waliozaliwa na akina mama waliokuwa na homa kali ya ini B wakati wa ujauzito mara nyingi huzaliwa na uzito mdogo.
Mara chache, mtoto anaweza kupata homa ya ini kali (homa kali ya ini B) muda mfupi baada ya kuzaliwa, ambayo kawaida hupotea yenyewe bila tiba. Dalili ni pamoja na manjano (macho na ngozi kuwa njano), unyonge, kusuasua kwa ukuaji, tumbo kuvimba, na kinyesi chenye rangi ya udongo. Mara chache sana, maambukizi yanaweza kuwa makali na kusababisha kifo.
Magonjwa sugu ya ini (kama homa ya ini sugu au cirrhosis) yanaweza kuanza kujitokeza lakini kawaida hayaonyeshi dalili wakati wa utoto.
Utambuzi wa Maambukizi ya HBV kwa Watoto Waliozaliwa Karibuni
Vipimo vya damu
Kipimo cha picha kwa kutumia mawimbi ya sauti cha ini.
Madaktari hupima damu kutafuta virusi vya homa ya ini B na kingamwili zake. Vipimo vya damu hufanywa pia kuona ikiwa ugonjwa wa ini umeanza kujitokeza (tazama Vipimo vya Damu ya Ini).
Ultrasonografia hufanyika ili kupata picha ya ini.
Matibabu ya Maambukizi ya HBV kwa Watoto waliozaliwa karibuni
Matibabu ya dalili na lishe bora.
Kuchanja
Madaktari hutibu matatizo yanayosababishwa na maambukizi ya virusi vya homa ya ini B. Lishe bora ni muhimu sana kwa watoto walioathirika.
Chanjo ya homa ya ini B ni moja ya chanjo za kawaida zinazopendekezwa kwa watoto wote. Watoto wote hupewa dozi ya kwanza ya chanjo ya virusi vya homa ya ini B kabla ya kuruhusiwa kutoka hospitalini.
Ubashiri wa Maambukizi ya HBV kwa Watoto Wachanga
Ingawa utabiri wa muda mrefu wa maambukizi ya virusi vya homa ya ini B sugu hayawezi kutabiliwa, inafahamika kwamba maambukizi sugu ya mapema maishani huongeza hatari ya ugonjwa wa ini hapo baadaye ikiwa ni pamoja na homa ya ini sugu, sirosisi, awamu ya mwisho ya ugonjwa wa ini inayohitaji upandikizaji, naa saratani ya ini.
Uzuiaji wa Maambukizi ya HBV kwa Watoto Waliozaliwa Karibuni
Wajawazito wanapaswa kupimwa virusi vya homa ya ini mapema wakati wa kliniki ya kwanza ya ujauzito. Ikiwa hawakupimwa hapo awali, wanapaswa kupimwa wakati wa kufika hospitalini kujifungua. Wajawazito wenye maambukizi makali wanaweza kupewa dawa za kuzuia virusi katika miezi mitatu ya mwisho ya ujauzito.
Watoto waliozaliwa na mama mwenye virusi vya homa ya ini B hupewa globulini ya kinga na chanjo ya homa ya ini B Dozi moja ya kila dawa hutolewa ndani ya saa 12 za kwanza baada ya kuzaliwa. Dozi zinazofuata za chanjo ya homa ya ini B hutolewa kulingana na ratiba ya kawaida ya chanjo.