Kukuza Afya Bora na Maendeleo ya Watoto

NaDeborah M. Consolini, MD, Thomas Jefferson University Hospital
Imekaguliwa naAlicia R. Pekarsky, MD, State University of New York Upstate Medical University, Upstate Golisano Children's Hospital
Imepitiwa/Imerekebishwa May 2023 | Imebadilishwa Aug 2023
v817289_sw

Wazazi na walezi wanaweza kuwasaidia watoto kufikia afya zao bora iwezekanavyo. Miaka ya mwanzo ya maisha ni muhimu kwa afya na ukuaji wa kimwili, kiakili, na kijamii/kihisia. Ikiwa mahitaji ya kimwili ya watoto yanatimizwa mara kwa mara na kwa uthabiti, watoto hujifunza haraka kwamba mlezi wao ni anawaridhisha, hiyo huunda kifungo imara cha uaminifu na ushikamano. Watoto wenye afya njema hukua na kuwa watoto na vijana wenye afya njema.

Afya ya utotoni

Ziara za huduma ya kinga ya afya (pia huitwa ziara za ustawi wa mtoto) ni muhimu kwa kukuza na kutunza afya njema kwa watoto wachanga (tazama Ziara za Huduma ya Kinga ya Afya kwa Watoto Wachanga), watoto (tazama Ziara za Huduma ya Kinga ya Afya kwa Watoto), na vijana (tazama Ziara za Huduma ya Kinga ya Afya kwa Vijana). Ziara hizi husaidia kuzuia ugonjwa kupitia chanjo ya kawaida, hatua zingine za kinga za kiafya, na tathmini ya matatizo ya kiafya. Ziara hizi pia huwapa wazazi fursa ya kuuliza maswali na kujifunza jinsi ya kuwasaidia watoto wao kukua kimwili, kihisia, na kiakili.

Maendeleo ya mtoto

Ili kukua kihisia na kiakili, watoto wachanga wanahitaji upendo na kuchangamshwa. Wazazi wanaoonesha uso wenye tabasamu, usemi wa kirafiki mara kwa mara, mgusano kimwili, na upendo wanasaidia ukuaji wa mtoto wao. Mahusiano mazuri na chanya yanayofurahiwa na mzazi na mtoto ndio jambo muhimu zaidi na ni muhimu zaidi kuliko aina ya vitu au uwingi wa vitu vya mtoto kuchezea nyumbani.

Kukuza ukuaji bora kwa mtoto kunafaa zaidi ikiwa kutafanywa kwa njia inayoendana, huku ukizingatia umri wa mtoto binafsi, tabia yake, hatua ya ukuaji wake, na mtindo wake wa kujifunza. Mbinu iliyoratibiwa inayowahusisha wazazi, walimu, na mtoto kwa kawaida hufanya vizuri zaidi. Katika miaka hii yote, watoto wanahitaji mazingira yanayokuza udadisi na ujifunzaji wa kudumu. Watoto wanapaswa kupewa vitabu na muziki. Utaratibu wa kusoma kwa njia shirikishi kila siku, huku wazazi wakiuliza na kujibu maswali, huwasaidia watoto kuzingatia na kusoma kwa uelewa na kuwapa moyo wa kupenda shughuli za kujifunza. Muda wa kutazama skrini (kwa mfano, televisheni, michezo ya video, simu za mkononi na vifaa vingine vya mkononi, na muda usio wa kielimu wa kompyuta) unaweza kusababisha kutoshughulisha mwili na unene kupita kiasi, na udhibiti wa muda ambao mtoto hutumia kwenye vifaa vya skrini unapaswa kuanzia wakati wa kuzaliwa na kudumishwa katika ujana wake wote.

Vikundi vya michezo na shule ya awali vina faida kwa watoto wadogo wengi. Watoto wanaweza kujifunza stadi muhimu za kijamii, kama vile kushirikisha. Zaidi ya hayo, wanaweza kuanza kutambua herufi, nambari, na rangi. Kujifunza stadi hizi hufanya kwenda shuleni iwe rahisi zaidi. Muhimu zaidi, katika mazingira ya shule ya awali yaliyopangiliwa, matatizo ya ukuaji yanayoweza kutokea yanaweza kutambuliwa na kushughulikiwa mapema.

Wazazi wanaohitaji malezi ya mtoto wanaweza kujiuliza mazingira gani ni bora na kama kulelewa na wengine kunaweza kumdhuru mtoto wao. Taarifa zilizopo zinaonesha kwamba watoto wadogo wanaweza kufanya vizuri nyumbani kwao na katika malezi nje na nyumbani, mradi tu mazingira yana upendo na kulea. Kwa kufuatilia kwa makini mwitikio wa mtoto katika mazingira fulani ya malezi ya watoto, wazazi wataweza kuchagua mazingira bora zaidi. Baadhi ya watoto hustawi katika mazingira ya malezi ya watoto ambapo kuna watoto wengi, ilhali wengine wanaweza kustawi vizuri zaidi nyumbani kwao au katika kundi dogo.

Mtoto anapoanza shule na kupokea kazi za kwenda kufanyia nyumbani, wazazi wanaweza kusaidia kwa

  • Kuonesha kupendezwa na kazi ya mtoto

  • Kuwepo kwaajili ya kutatua maswali lakini si kumaliza kazi zenyewe

  • Kutoa mazingira tulivu ya kazi nyumbani kwaajili ya mtoto

  • Kuwasiliana na mwalimu kuhusu wasiwasi wowote

Kadri miaka ya shule inavyoendelea, wazazi wanahitaji kuzingatia mahitaji ya mtoto wao anapochagua shughuli za nje ya masomo. Watoto wengi hustawi wanapopewa fursa ya kushiriki katika shughuli hizi, kama vile kucheza michezo kwa timu au kujifunza ala za muziki. Shughuli hizi zinaweza pia kutoa nafasi ya kuboresha stadi za kijamii. Kwa upande mwingine, baadhi ya watoto hupata msongo wa mawazo wanapopangiwa ratiba kupita kiasi na kutarajiwa kushiriki katika shughuli nyingi mno. Watoto wanahitaji kutiwa moyo na kuungwa mkono katika shughuli zao za nje ya masomo bila kuwa na matarajio yasiyoendana nao.