Kinyesi na Mkojo kwa Watoto Wachanga

NaDeborah M. Consolini, MD, Thomas Jefferson University Hospital
Imekaguliwa naAlicia R. Pekarsky, MD, State University of New York Upstate Medical University, Upstate Golisano Children's Hospital
Imepitiwa/Imerekebishwa Imebadilishwa Sept 2023
v813760_sw

Baada ya siku chache za kwanza za maisha, watoto wachanga wanapaswa kuwa na nepi zenye mkojo angalau 6 hadi 8 kwa siku, na wakati mwingine zaidi. Rangi ya mkojo hutofautiana kutoka njano iliyokolea hadi usio na rangi..

Kinyesi cha watoto wachanga hutofautiana sana katika idadi ya mara za kutolewa, rangi, na hali, kulingana na mtoto binafsi na aina ya lishe anayopata. Watoto wachanga wanaweza kujisaidia haja kubwa kuanzia mara moja kila siku hadi mara 6 au 8 kwa siku. Kinyesi kinaweza kuwa kigumu na chenye umbo au laini na chenye majimaji. Rangi ya kinyesi inaweza kuwa manjano ya haradali au hata kahawia iliyokolea. Kinyesi cha watoto wanaonyonyeshwa maziwa ya mama huwa laini zaidi na chenye rangi isiyokolea kikilinganishwa na cha watoto wanaolishwa fomula.

Nepi zinapaswa kubadilishwa mara kwa mara ili kuweka ngozi ikiwa kavu. Ngozi yenye unyevunyevu huchubuka kwa urahisi zaidi kuliko ngozi kavu na ina uwezekano mkubwa wa kupata upele wa nepi. Nepi za kisasa zinazotupwa baada ya matumizi zina safu ya jeli inayofyonza kioevu na kukiweka mbali na ngozi. Nepi hizi huweka ngozi ikiwa kavu zaidi kuliko nepi za kitambaa baada ya kiasi kidogo hadi cha wastani cha mkojo, lakini nepi za aina yoyote zinapaswa kubadilishwa mara ngozi inapolowa. Bakteria waliopo kawaida kwenye kinyesi huvunja urea iliyo kwenye mkojo, na kusababisha pH ya alkali inayochubua ngozi; hivyo, nepi zinapaswa kukaguliwa mara kwa mara na kubadilishwa mara moja endapo kuna kinyesi.

Poda za watoto zinaweza kusaidia kuweka ngozi ikiwa kavu mtoto anapotokwa na jasho kidogo, lakini hazisaidii dhidi ya unyevunyevu unaotokana na mkojo au kinyesi na si za lazima. Poda zenye talcum zinaweza kusababisha matatizo ya mapafu endapo zitavutwa na mtoto; kwa hiyo, wazazi wanaopenda kutumia poda wanashauriwa kuchagua poda ya mtoto yenye wanga wa mahindi (cornstarch).