Kubana kwa aota ni aota kuwa nyembamba, mshipa mkuu wa damu unaoleta damu nyekundu yenye oksijeni kutoka moyoni hadi mwilini.
Aota huwa nyembamba, na kusababisha moyo kusukuma kwa nguvu zaidi ili kusukuma damu kupitia aota nyembamba ili kupata mtiririko wa kutosha wa damu hadi nusu ya chini ya mwili.
Watoto wachanga walio na aota iliyobana kwa kiwango kikubwa huugua ghafla wanapokuwa na umri wa siku chache, wakionyesha dalili za moyo kushindwa kufanya kazi na kupungua kwa mtiririko wa damu kwenda sehemu ya chini ya mwili. Watoto wakubwa walio na aota iliyobana mara nyingi hawana dalili.
Utambuzi hushukiwa kulingana na dalili na matokeo wakati wa uchunguzi wa daktari na unathibitishwa kwa kutumia ekokadiografia.
Watoto wengi walio na aota iliyobana wanahitaji upasuaji wa kurekebisha au utaratibu wa kufungua mishipa ya damu iliyoziba kwa kutumia (angioplasty) puto ili kupanua aota iliyo nyembamba.
(Angalia pia Muhtasari wa Kasoro za Moyo.)
Kubana kwa aota, kasoro ya moyo ya kuzaliwa, ni sehemu moja tu ya aota kuwa nyembamba, si aota nzima. Wembamba huu kwa kawaida hupatikana sehemu ambapo ductus arteriosus inaungana na aota. Ductus arteriosus ni mshipa wa damu unaounganisha mishipa miwili mikubwa inayotoka moyoni, ateri ya mapafu na aota (angalia Mzunguko wa Kawaida wa Damu kwenye Kijusi). Katika tumbo la uzazi na wakati wa siku chache za kwanza za maisha, ductus huwa wazi, kwa hivyo damu inayopita hupita sehemu nyembamba ya aota.
Kubana kwa aota kunaweza kupunguza mtiririko wa damu hadi nusu ya sehemu ya chini ya mwili, ikiwa ni pamoja na figo, ini, na viungo vingine tumboni. Shinikizo la damu huwa chini kuliko kawaida kwenye miguu na huwa juu kuliko kawaida kwenye mikono. Kubana kwa aota ni sababu kubwa sana ya shinikizo la damu inayotibika. Wakati mwingine kuna mvumo wa moyo (sauti inayotokana na mtiririko wa damu unaovurugika kupitia vali za moyo zilizobana au zinazovuja au kupitia miundo isiyo ya kawaida ya moyo).
Bila matibabu, kubana kwa aota kwa kiwango kikubwa kunaweza kusababisha kifo kwa watoto wachanga. Kubana kwa aota kwa kiwango kidogo hatimaye huzidisha na kupanua moyo na kusababisha shinikizo la damu. Kubana kwa aota humfanya mtoto awe katika hatari ya kupata maambukizi ya moyo (endokadaitisi inayoambukizwa) na kutokwa na damu kwenye ubongo. Watoto wenye ugonjwa wa kubana kwa aota mara nyingi huwa na kasoro nyingine za moyo, kama vile kuziba kwa vali ya aota au kasoro ya septamu ya atiria au ventrikali.
Dalili za Kubana kwa Aota
Watoto wachanga waliobana aota kiasi kwa kawaida huwa na dalili chache au hawana dalili zozote. Watoto wachanga waliobana aota kwa wastani wanaweza kuwa na upumuaji wa kasi, wakati mwingine kwa shida, mapigo ya moyo ya haraka, kunyonya vibaya, rangi ya ngozi ya kijivu, kupata choo mara chache, na kuwa mkali au uchovu.
Kwa watoto wachanga waliobana aota kwa kiwango kikubwa, damu inaweza kutiririka hadi sehemu ya chini ya aota (katika hatua iliyopita wembamba wake) kupitia muunganisho wa wazi kati ya aota na ateri ya mapafu, ductus arteriosus. Kwa kawaida dalili hazitokei hadi ductus ifungwe, kwa kawaida mtoto mchanga anapokuwa na umri wa siku chache. Baada ya kufungwa, damu inayotolewa kupitia ductus hutoweka, wakati mwingine ikisababisha upotevu wa ghafla wa karibu damu yote inayoingia kwenye sehemu ya chini ya mwili. Moyo kushindwa kufanya kazi ghafla au kutokana na janga na shinikizo la chini la damu inaweza kutokea.
Watoto wengi wakubwa waliobana aota hawana dalili. Wakati mwingine, watoto waliobana aota huhisi maumivu ya kichwa au kutokwa na damu puani kutokana na shinikizo la juu la damu kwenye sehemu ya juu ya mwili au maumivu ya miguu wakati wa mazoezi kwa sababu damu inayoingia kwenye miguu haitoshi.
Utambuzi wa ugonjwa wa Kubana kwa Aota
Ekokadiografia
Wakati mwingine tomografia ya kompyuta (CT) au upigaji picha kwa mwangwi wa sumaku (MRI)
Kwa kawaida kubana kwa aota hushukiwa wakati daktari anapogundua mvumo wa moyo au tofauti katika mapigo ya moyo au shinikizo la damu kati ya mikono na miguu anapofanya uchunguzi wa kimwili. Kuvuma kwa moyo ni sauti inayotokana na mtiririko wa damu wenye msukosuko kupitia vali za moyo zilizofinyana au zinazovuja au kupitia miundo isiyo ya kawaida ya moyo. Aidha, shinikizo la damu linalopimwa mikononi linaweza kuwa la juu sana.
Ekokadiografia (sonografia ya moyo) na, wakati mwingine, CT au MRI huthibitisha utambuzi.
Elektrocardiografia (ECG) na eksirei za kifua zinafanywa kwa kawaida. Huenda zikaonyesha moyo uliopanuka.
Matibabu ya Kubana kwa Aota
Wakati mwingine dawa, prostaglandin
Upasuaji, angioplasty kwa kutumia puto, au uwekaji wa kifaa cha kuweka wazi mishipa (stent)
Matibabu hulingana na ukali wa kubana kwa aota na dalili kunakosababisha.
Watoto wachanga wenye dalili kali kutokana na kubana kwa aota wanahitaji matibabu ya dharura, ikiwa ni pamoja na
Matibabu kwa kutumia prostaglandin, dawa ambayo inaweza kufungua tena ductus arteriosus ili kuboresha mtiririko wa damu hadi sehemu ya chini ya mwili.
Dawa nyingine za kuimarisha mapigo ya moyo
Upasuaji wa dharura ili kupanua sehemu nyembamba
Upasuaji ni matibabu yanayopendelewa zaidi kwa kubana kwa aota kwa kiwango cha wastani au kikali kwa watoto wachanga na watoto wadogo. Sehemu nyembamba ya aota inaweza kukatwa na kuondolewa kisha sehemu mbili za kawaida kushonwa pamoja, au kiraka kinaweza kutumika kupanua sehemu nyembamba ya aota. Wakati mwingine, tishu kutoka kwenye mshipa wa damu unaotoa mkono wa kushoto (ateri ya subklavia) hutumiwa kutengeneza kiraka hiki.
Kubana aota kwa kiwango kidogo sana ambako hakusababishi dalili zozote huenda kusigundulike mapema maishani. Kunaweza kutambuliwa watoto wakiwa wakubwa kidogo na aota ikiwa nyembamba. Daktari anaweza kugundua mapigo ya moyo yenye nguvu zaidi na shinikizo la juu zaidi la damu mkononi kuliko mguu. Kwa watoto kama hao, upasuaji na angioplasty kwa kutumia puto ni chaguo za kurekebisha aota iliyo nyembamba. Angioplasty kwa kutumia puto hufanywa wakati wa kuweka katheta moyoni, ambapo mrija mwembamba (katheta) wenye puto kwenye ncha yake hupitishwa kupitia mshipa wa damu kwenye mkono au mguu hadi kwenye aota iliyo nyembamba. Puto huvimbishwa, na kupanua aota iliyo nyembamba. Wakati mwingine, mirija inayonyumbulika inayoweza kupanuka (kifaa cha kuweka wazi mishipa) huingizwa ili kusaidia kuzuia aota isiwe nyembamba tena.
Baadhi ya watoto waliofanyiwa upasuaji wa kurekebisha kubana aota hupata tishu za kovu kwenye aota mahali paliporekebishwa. Kovu kama hilo hufanya aota iwe nyembamba na hutokea kwa kawaida kwa watoto wachanga waliohitaji upasuaji wa dharura mapema sana maishani. Angioplasty kwa kutumia puto ikiwa na au bila kuwekwa kifaa cha kuweka wazi mishipa kwa kawaida ni matibabu bora sana kwa wembamba huu unaojirudiarudia.
Watoto wanahitaji kutumia antibiotiki kabla ya kumtembelea daktari wa meno na kabla ya upasuaji fulani (kama vile kwenye njia ya upumuaji) kwa kipindi cha miezi 6 baada ya kupona. Dawa za kuua bakteria hizi hutumika kuzuia maambukizi makubwa ya moyo yanayoitwa endokardaitisi.
Taarifa Zaidi
Nyenzo zifuatazo za lugha ya Kiingereza zinaweza kuwa muhimu. Tafadhali kumbuka kuwa MWONGOZO hauwajibiki kwa maudhui ya nyenzo hizi.
Ushirika wa Masuala ya Moyo Nchini Marekani: Kasoro za Moyo za Kawaida: Hutoa muhtasari wa kasoro za kawaida za kuzaliwa kwa moyo kwa wazazi na walezi
Ushirika wa Masuala ya Moyo Nchini Marekani: Endokadaitisi inayoambukizwa: Hutoa muhtasari wa endokadaitisi inayoambukizwa, ikijumuisha muhtasari wa matumizi ya dawa za kuua bakteria, kwa wazazi na walezi.