COVID 19 ni ugonjwa wa kupumua ambao unaweza kuwa mbaya. Husababishwa na maambukizi ya virusi vinavyoitwa severe acute respiratory syndrome coronavirus 2 (SARS-CoV-2).
Hatari ya kupata COVID-19 inaonekana kuwa sawa kwa wanawake wajawazito na watu wazima wengine.
Madaktari wanashuku COVID-19 kulingana na dalili na uwezekano wa kuambukizwa, lakini vipimo vinahitajika ili kuthibitisha utambuzi.
Mara dalili zinapojitokeza, COVID-19 ina uwezekano mkubwa wa kusababisha ugonjwa mbaya kwa wanawake wajawazito, hasa ikiwa wana maradhi fulani (kama vile kisukari au ugonjwa wa moyo), kuliko kwa watu ambao si wajawazito.
Hatari ya matatizo wakati wa ujauzito (kama vile uchungu wa uzazi kabla ya wakati wa kujifungua, kuzaliwa kwa mtoto mchanga kabla ya wakati, na priklampsia) huongezeka ikiwa dalili za COVID-19 ni za wastani au kali.
Hatari ya mwanamke mjamzito kuambukiza COVID-19 kijusi au mtoto mchanga wakati wa mchakato wa kuzaliwa inaonekana kuwa ndogo sana. Lakini mara tu mtoto anapozaliwa, kuenea kwa maambukizi kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine kunawezekana.
Dalili za COVID-19 Wakati wa Ujauzito
Watu wengi wenye COVID-19 wana dalili ndogo au hawana dalili zozote, lakini wengine huwa wagonjwa sana na hufa. Dalili zinaweza kujumuisha homa, kikohozi na matatizo ya kupumua. Kupoteza uwezo wa kunusa au ladha kunaweza kuwa dalili ya kwanza mara mojamoja.
Mara tu dalili za COVID-19 zinapoanza, wanawake wajawazito wana uwezekano mkubwa wa kupata magonjwa makali kuliko watu wengine, hasa ikiwa wana maradhi fulani (kama vile kisukari au ugonjwa wa moyo). Wanawake walio na ugonjwa mbaya wanaweza kuhitaji kulazwa hospitalini, huduma ya wagonjwa mahututi, na/au kipumulio. Hata hivyo, hatari ya jumla ya ugonjwa mbaya na kifo kutokana na COVID-19 inabaki kuwa ndogo kwa wanawake wajawazito.
Hatari ya kutokea kwa matatizo wakati wa ujauzito (kama vile uchungu wa uzazi kabla ya wakati wa kujifungua, kuzaliwa kwa mtoto mchanga kabla ya wakatina preklampsia) huongezeka ikiwa dalili ni za wastani au kali.
Utambuzi wa COVID-19 Wakati wa Ujauzito
Tathmini ya daktari
Vipimo vya kutambua virusi
Utambuzi wa COVID-19 kwa wanawake wajawazito ni sawa na utambuzi kwa watu walio na COVID-19 na ambao hawana mimba. COVID-19 inashukiwa ikiwa watu wana homa, kikohozi, kupoteza uwezo wa kuhisi harufu au ladha ghafla, na/au shida ya kupumua na huenda wakawa wameambukizwa virusi.
Ili kuthibitisha utambuzi, madaktari wanaweza kuchukua sampuli za majimaji kutoka kwenye njia ya upumuaji ili kupimwa. Ikiwa kipimo hakipatikani kwa urahisi au ikiwa dalili ni ndogo, utambuzi unaweza kutegemea dalili na uwezekano wa kuambukizwa (ikiwa unaweza kubainika).
Ikiwa inahitajika, eksrei ya kifua na/au tomografia ya kompyuta (CT) hufanywa.
Matibabu ya COVID-19 Wakati wa Ujauzito
Acetaminophen ili kupunguza homa na maumivu ya misuli
Wakati mwingine, mchanganyiko wa nirmatrelvir na ritonavir
Matibabu ya COVID-19 Kwa wanawake wajawazito na wanawake ambao si wajawazitohufanana.
Acetaminophen inaweza kutumika kupunguza homa na maumivu, kama vile maumivu ya misuli.
Ndani ya siku chache baada ya kupata dalili za COVID-19 zisizo kali hadi wastani, daktari anaweza kuwatibu wanawake wajawazito kwa mchanganyiko wa nirmatrelvir na ritonavir ili kufupisha muda wa ugonjwa na kufanya dalili zisiwe kali sana. Utafiti mdogo uligundua kuwa wagonjwa wajawazito hawakupata madhara yoyote makubwa kutokana na matibabu, na hakuna matatizo yoyote yaliyohusishwa na dawa hiyo.
Kabla ya kujifungua, wanawake wajawazito walio na COVID-19 wanapaswa kuiarifu hospitali kwamba wana maambukizi. Kisha wafanyakazi wa hospitali wanaweza kuchukua tahadhari zinazohitajika ili kuzuia kuenea kwa virusi.
Kinga ya COVID-19 Wakati wa Ujauzito
Njia bora ya kuzuia COVID-19 ni kuepuka kuambukizwa virusi, jambo ambalo linaweza kuwa gumu kwa sababu baadhi ya watu walioambukizwa hawajui kama wana virusi hivyo. Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC) vimetoa mapendekezo ya kuzuia kuenea kwa COVID-19. Mapendekezo haya yanawahusu watu wote (tazama pia Kuzuia COVID-19).
Ikiwa mwanamke mjamzito anaweza kuambukizwa, kumtenganisha na mtoto wake baada ya kujifungua kunaweza kuwa muhimu ili kuepuka kumwambukiza mtoto.
Chanjo za COVID-19
CDC inapendekeza chanjo ya COVID-19 kwa watu wote wanaostahiki ambao ni wajawazito, wanaonyonyesha, wanaojaribu kupata mimba sasa, au ambao wanaweza kupata mimba katika siku zijazo. Faida za kupokea chanjo ya COVID-19 zinazidi hatari zozote zinazojulikana au zinazoweza kutokea za chanjo wakati wa ujauzito. (Angalia pia CDC: Chanjo za COVID-19 Ukiwa Mjamzito au Unanyonyesha.)
Chanjo inaweza pia kutoa ulinzi kwa watoto wachanga ikiwa watanyonyeshwa. Utafiti unaoungwa mkono na Taasisi za Kitaifa za Afya (NIH) uligundua kuwa wakati mtu mjamzito ana kingamwili dhidi ya SARS-CoV-2 baada ya kuchanjwa au kuwa na COVID-19, kingamwili hizo zinaweza kuhamishiwa kwa mtoto kupitia maziwa ya mama. Kingamwili hizo huwasaidia watoto wachanga kupata kinga ambayo inaweza kuwalinda kutokana na COVID-19.
Nyonyesha
Hatari ya mama kusambaza virusi kupitia maziwa ya mama ni ndogo au haipo kabisa. (Angalia pia CDC: COVID-19 na Kunyonyesha.)
Ikiwa mwanamke mwenye maambukizi ya SARS-CoV-2 anachagua kunyonyesha moja kwa moja, anapaswa kuvaa barakoa na kudumisha usafi wa mikono.
Ikiwa mwanamke ananyonyesha maziwa ya mama kwa chupa, kabla ya kutoa maziwa, anapaswa kuvaa barakoa na kunawa mikono yake vizuri na sehemu zozote za pampu, chupa, na chuchu bandia.
Taarifa Zaidi
Nyenzo zifuatazo za lugha ya Kiingereza zinaweza kuwa muhimu. Tafadhali kumbuka kuwa MWONGOZO hauwajibiki kwa maudhui ya nyenzo hizi.
Chuo cha Madaktari wa Uzazi na Wanajinakolojia wa Marekani: Virusi vya Korona (COVID-19), Ujauzito na Kunyonyesha: Ujumbe kwa Wagonjwa: Tovuti hii inajadili jinsi COVID-19 inavyoweza kuathiri wanawake wajawazito na kijusi, kama wanawake wajawazito wanapaswa kupata chanjo ya COVID-19, jinsi ya kuepuka kupata virusi, nini cha kufanya ikiwa wanawake wajawazito wanafikiri wameambukizwa au kama wameambukizwa COVID-19, na jinsi COVID-19 inavyoathiri mipango yao ya utokeaji wa uchungu wa kujifungua na kujifungua. Kunyonyesha na COVID-19 pia vinajadiliwa.
Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC): Virusi vya Korona (COVID-19): Tovuti hii inatoa viungo vya taarifa kuhusu chanjo za COVID-19 (ikiwa ni pamoja na jinsi ya kupata chanjo), idadi na eneo la visa (ikiwa ni pamoja na ramani na chati zinazofuatilia visa, vifo, na mitindo ya COVID-19) nchini Marekani, na mapendekezo kuhusu jinsi ya kuhakikisha kuwa uko salama shuleni na mahali pa kazi.