Amebiasisi ni maambukizi kwenye utumbo mkubwa na wakati mwingine ini na viungo vingine ambayo husababishwa na kimelea cha protozoa cha seli moja Entamoeba histolytica, ambayo ni amiba.
Amebas inaweza kusambaa moja kwa moja kutoka kwa mtu kwenda kwa mtu kupitia maambukizi kutoka kwenye kinyesi hadi mdomo wa mtu mwingine, ikiwa ni pamoja na kukutanisha mdomo na mkundu au isivyo moja kwa moja kupitia chakula au maji.
Watu wanaweza wasiwe na dalili au wanaweza kuharisha, kufunga choo, maumivu ya tumbo yanayokaza, ulaini kwenye sehemu ya juu ya tumbo na homa.
Madaktari hukita utambuzi wa ugonjwa kwa kuchanganua sampuli ya kinyesi na, ikiwa inahitajika, vipimo vingine kama vile kolonoskopia au atrasonografia na vipimo vya damu.
Watu wanapewa dawa ambazo zinaua amebas, ikifuatiwa na dawa zinazoua aina tuli (uvimbe) ya emebas kwenye utumbo mpana.
(Angalia pia Muhtasari wa Maambukizi ya Vimelea.)
Amebiasisi huwa inatokea kwenye maeneo ambapo usafi haufanywi vya kutosha. Vimelea vipo duniani kote, lakini maambukizi mengi yanatokea kwenye maeneo ya Afrika, baradogo la India na sehemu za Amerika ya Kati na Kusini. Katika nchi yenye vyakula safi na maji, matukio mengi hutokea miongoni mwa wahamiaji wa hivi karibuni na wasafiri wanaotoka katika nchi zenye usafi duni.
Kila mwaka duniani kote, karibu watu milioni 50 wanakuwa na amebiasisi, na wengi kufikia 73,000 kati yao wanakufa.
Spishi za Entamoeba zipo katika aina 2:
Kimelea tuli (jipu)
Kimelea amilifu (trophozoite)
Spishi nyingine za ameba haziwaambukizi watu kupitia utumbo na zinaweza kuathiri ubongo moja kwa moja (maambukizi ya amiba kwenye ubongo) au jicho (amebic keratitis).
Uenezaji wa amoebiasisi
Maambukizi huanza wakati uvimbe unamezwa. Uvimbe huo unapasuka, unatoa trophozoiti ambao wanaongezeka na kusababisha vidonda kwenye utando wa utumbo. Mara chache huenea hadi kwenye ini au sehemu zingine za mwili. Baadhi ya trophozoiti wanakuwa uvimbe, ambao unatolewa katika kinyesi sambamba na trophozoiti. Nje ya mwili, trophozoiti dhaifu hufa. Hata hivyo, uvumbe mgumu unaweza kuendelea kuishi kwa wiki au miezi kadhaa.
Uvimbe unaweza kuenea moja kwa moja kutoka kwa mtu kwenda kwa mtu kupitia kinyesi kwenda mdomoni, ikiwa ni pamoja na mkundu kukutana na mdomo.
Katika maeneo yenye usafi duni, amebiasisi inaweza kupatikana moja kwa moja kwa kutumia chakula au maji ambayo yana kinyesi. Matunda na mbogamboga yanaweza kuchafuliwa yanapomea kwenye udongo wenye kinyesi cha binadamu, kuoshwa kwenye maji yaliyochafuliwa, au kuandaliwa na mtu ambaye ameambukizwa. Amebiasisi inaweza kutokea na kuenea katika maeneo yenye usafi wa kutosha ikiwa watu wenye maambukizi hawajali au usafi ni duni (kwa mfano, katika vituo vya kulelea watoto au tasisi za wagonjwa wa akili).
Dalili za amoebiasisi
Watu wengi walioambukizwa wana dalili chache au hawana dalili kabisa. Hata hivyo, wanatoa uvimbe wa vimelea kwenye kinyesi na kwa hivyo wanaweza kueneza maambukizi.
Dalili za amebiasisi kwa kawaida zinaanza kwa zaidi ya wiki 1 hadi 3 na zinaweza kujumuisha
Kuharisha, wakati mwingine damu ikionekana kwenye kinyesi
Maumivu ya tumbo la kukaza
Kupungua uzito
Katika hali mbaya, tumbo linakuwa laini linapoguswa na watu wanaweza kuwa na hali mbaya ya kuharisha wakitoa kinyesi ambayo kina kamasi na damu (huitwa ugonjwa wa kuhara damu). Baadhi ya watu wana maumivu ya tumbo la kukaza na homa kali. Kuhara kunaweza kusababisha kupungukiwa maji. Kupungua mwili na kupungua damu kunaweza kutokea kwa watu wenye maambukizi sugu.
Wakati mwingine uvimbe mkubwa (amebomas) unaweza kuonekana ndani ya utumbo mpana.
Kwa baadhi ya watu, amebas inaenea kwenye ini ambapo inaweza kusababisha usaha. Dalili zinajumuisha homa, jasho, ubaridi, udhaifu, kichefuchefu, kutapika, kupungua uzito na maumivu au kutojisikia vizuri upande wa juu kulia wa tumbo juu ya ini.
Kwa nadra, amebas inaenea kwenye viuongo vingine (ikiwa ni pamoja na mapafu au ubongo). Ngozi pia inaweza kuambukizwa, kwenye eno la makalio (maambukizi ambayo yanaenea kutoka kwenye kinyesi chenye vimelea), sehemu za siri (kwa mfano, vidonda kwenye uume kutokana na ngono kinyume na maumbile na mtu mwenye maambukizi) au vidonda vinavyosababishwa na upasuaji au jeraha la tumbo.
Utambuzi wa ugonjwa wa amoebiasisi
Vipimo vya kinyesi
Wakati mwingine vipimo vya damu hufanywa ili kubaini kingamwili dhidi ya amebas
Wakati mwingine uchunguzi wa sampuli ya tishu kutoka kwenye utumbo mpana
Ili kutambua ugonjwa wa amebiasisi, daktari anakusanya sampuli za kinyesi kwa ajili ya uchanganuzi. Mbinu bora ni kupima kinyesi ili kuona protini inayotolewa na amebas (kupima antijeni) au kutumia mbinu ya mmenyuko wa mnyororo wa polima (PCR) ili kuangalia kinyesi endapo kina vitu vya jumla vya ameba. Mbinu ya PCR inazalisha nakala nyingi za vitu vya jumla vya amiba na kwa hivyo hufanya iwe rahisi kuibaini ameba. Vipimi vya antijeni au PCR vinafaa zaidi kuliko uchunguzi wa kihadubini wa sampuli za kinyesi, ambao mara nyingi hautoa hitimisho. Pia, uchunguzi wa kihadubini unaweza kuhitaji sampuli 3 hadi 6 za kinyesi ili kupata ameba na hata wakati zinapoonekana, Entamoeba histolytica haiwezi kutofautishwa na amiba zingine zinazohusiana. Kwa mfano, Entamoeba dispar, ambayo inaonekana kufanana lakini kwa ujumla ni tofauti, haisababishi ugonjwa.
Neli jongevu ya kutazamia (endoskopi) inaweza kutumia kutazama ndani ya utumbo mpana. Endapo vidonda au dalili nyinginezo za maambukizi zinapatikana hapo, endoskopi inatumika kupata sampuli ya kimiminika au tishu kutoka kwenye eneo lisilo la kawaida.
Amebas inapoenea kwenye maeneo nje ya utumbo (kama vile ini), inaweza isionekane tena kwenye kinyesi. Atrasonografia, tomografia ya kompyuta (CT), au upigaji picha kwa mwangwi wa sumaku (MRI) unaweza kufanywa ili kuthibitisha usaha kwenye ini, lakini vipimo hivyo haviashirii chanzo. Kisha vpimo vya damu vinafanywa ili kuangalia kingamwili dhidi ya amebas. (Kingamwili ni protini zinazozalishwa na mfumo wa kingamwili ili kusaidia kulinda mwili dhidi ya mashambulizi fulani, ikiwa ni pamoja na yale ya vimelea.) Au, ikiwa madaktari wanashuku kwamba usaha kwenye ini unatokana na amebas, wanaweza kuanza kutoa dawa inayoua amebas. Ikiwa mtu anapata unafuu, utambuzi wa ugonjwa pengine ni amebiasisi.
Matibabu ya amoebiasisi
Dawa zinazoua amebas (tinidazole, metronidazole, secnidazole, au ornidazole)
Dawa zinazoua aina tuli ya amebas (uvimbe) (iodoquinol, paromomycin, au diloxanide furoate)
Ikiwa amebiasisi inashukiwa na mtu anakuwa na dalili, dawa ya kuua amebas, ama tinidazole, metronidazole, secnidazole, au ornidazole, inatumika. Watu hawapaswi kunywa pombe wanapotumia dawa zozote kati ya dawa hizi au kwa siku kadhaa baada ya kuacha kuzitumia kwa sababu kufanya hivyo kunaweza kusababisha, kichefuchefu, kutapika, kusawijika na maumivu ya kichwa. Nitazoxanide imependekezwa kama njia mbadala ya kutibu amebiasisi.
Metronidazole, tinidazole, secnidazole, ornidazole, na nitazoxanide haziui uvimbe wote ambao upo kwenye utumbo mpana. Dawa ya pili (kama vile paromomycin, diiodohydroxyquin, au diloxanide furoate) hutumika kuua uvimbe huu na hivyo kuzuia kurudia tena. Moja wapo ya dawa hizi inaweza kutumika peke yake kutibu watu ambao hawaumwi lakini wana Entamoeba histolytica kwenye kinyesi chao. Paromomycin ni salama kutumia kwa mjamzito. Diloxanide furoate haipatikani kibiashara nchini Marekani lakini inaweza kupatikana kupitia baadhi ya maduka ya dawa ya jumla.
Watu ambao wamepungikiwa maji wanapewa vimiminika.
Uzuiaji wa amoebiasisi
Ili kupunguza hatari ya amebiasisi, watu wanapaswa kufuata tahadhari za chakula na maji, kuwana mazoea ya usafi bora na kuepuka kukutana na kinyesi wakati wa ngono. (Angalia Kituo cha Udhibiti na Uzuiaji wa Magonjwa): Kitabu cha Njano: Amebiasis na Tahadhari za Chakula na Maji.)
Kuzuia chakula na maji yasichafuliwe na kinyesi cha binadamu ni muhimu katika kuzuia amebiasisi. Kuboresha mfumo wa usafi kwenye maeneo ambapo maambukizi yameenea kunaweza kusaidia.
Unaposafiri kwenda kwenye maeneo ambapo maambukizi yameenea, watu wanapaswa kuepuka kula vyakula ambavyo havijapikwa, ikiwa ni pamoja na saladi na mboga za majani, na wanapaswa kuepuka kutumia maji au barafu ambayo imechafuliwa. Kuchemsha maji kunaua uvimbe. Kunawa mikono kwa sabuni na maji ni muhimu. Kuchuja maji kupitia kichujio cha mikroni 0.1 au 0.4 kunaweza kuondoa Entamoeba histolytica na vimelea vingine, vilevile bakteria inayoweza kusababisha magonjwa. Kuyeyusha iodini au klorini kwenye maji kunaweza kusaidia. Hata hivyo, ufanisi wa iodini au klorini dhidi ya Entamoeba histolytica hutegemea sababu nyingi, kama vile, maji yana vumbi au tope kiasi gani na hali joto yake ni ipi.
Utafiti unaendelea kuhusu utengenezaji wa chanjo, hakuna chanjo iliyopo tayari.
Taarifa Zaidi
Nyenzo zifuatazo za lugha ya Kiingereza zinaweza kuwa muhimu. Tafadhali kumbuka kuwa MWONGOZO hauwajibiki kwa maudhui ya nyenzo hizi.
Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC): Kitabu cha Njano: Amebiasisi
CDC: Kitabu cha Njano: Tahadhari za Chakula na Maji
CDC: Vimelea - Amebiasisi: Taarifa za Jumla