Uwasilishaji wa Fetasi, Nafasi, na Mkao (Ikijumuisha Utaratibu wa mtoto kuwa kinyume)

NaJulie S. Moldenhauer, MD, Children's Hospital of Philadelphia
Imekaguliwa naSusan L. Hendrix, DO, Michigan State University College of Osteopathic Medicine
Imepitiwa/Imerekebishwa Jan 2024 | Imebadilishwa Mar 2024
v8578243_sw

Wakati wa ujauzito, kijusi kinaweza kukaa katika mikao mingi tofauti ndani ya uterasi ya mama. Kijusi kinaweza kuelekeza kichwa juu au chini au kuelekea upande wa mgongo au wa mbele ya mama. Mwanzo, kijusi kinaweza kugeuka kwa urahisi au kubadilisha mkao mama anapojitikisa. Kuelekea mwishoni mwa ujauzito, kijusi kinakuwa kikubwa zaidi, kinakuwa na nafasi ndogo ya kugeuka na husalia katika mkao mmoja. Jinsi kijusi kilivyokaa ina athari muhimu katika kujifungua na, kwa mikao fulani, kujifungua kwa njia ya upasuaji ni ya lazima. Kuna istilahi za kimatibabu zinazoelezea kwa usahihi jinsi kijusi kilivyokaa, na kutambua mkao wa kijusi husaidia madaktari kutabiri changamoto zinazoweza kutokea wakati wa uchungu na kujifungua.

Utaratibu wa kutoka linarejelea sehemu ya mwili wa kijusi inayotangulia kutoka nje kupitia njia ya uzazi (inayoitwa sehemu inayotangulia). Kwa kawaida, kichwa ndicho hutangulia, lakini wakati mwingine matako (utaratibu wa mtoto kuwa kinyume), bega au uso hutangulia.

Mkao unarejelea kama kijusi kimeelekea nyuma (osipati kutangulia) au mbele (osipati kuja baadaye). Osipati (occiput) ni mfupa ulioko nyuma ya kichwa cha mtoto. Kwa hivyo, kuelekea nyuma huitwa "osipati kutangulia" (mtoto kuelekea mgongo wa mama na kutazama chini mama anapolala chali). Kuelekea mbele huitwa "osipati kuja baadaye" (mtoto kuelekea mfupa wa fupanyonga wa mama na kutazama juu mama anapolala chali).

Ulalo (Lie) inarejelea pembe ya kijusi kuhusiana na mama na uterasi. Ulalo wa juu nachini (uti wa mgongo wa mtoto ukiwa sambamba na uti wa mgongo wa mama, uitwao ulalo wa longitudo) ni wa kawaida, lakini wakati mwingine ulalo huwa wa upande (kukingama) au wa mshazari.

Kwa vipengele hivi vya ukaaji wa kijusi, mchanganyiko ambao ni wa kawaida zaidi, salama zaidi na rahisi zaidi kwa mama kujifungua ni ufuatiliaji huu:

  • Kichwa kutangulia (huitwa vertex au utaratibu wa kichwa kutangulia)

  • Kuelekea nyuma (mkao wa osipati kutangulia)

  • Uti wa mgongo ukiwa sambamba na uti wa mgongo wa mama (ulalo wa longitudo)

  • Shingo kuinama mbele huku kidevu kikiwa kimegusa kifua

  • Mikono ikiwa imekunjwa kifuani

Ikiwa kijusi kipo katika mkao, ulalo au utaratibu tofauti ambapo kichwa hakitangulii, uchungu unaweza kuwa mgumu zaidi, na kujifungua kwa njia ya kawaida kupitia uke kunaweza kusiwezekane.

Mabadiliko katika utaratibu wa kijusi kutoka, mkao au ulalo wa kijusi yanaweza kutokea wakati

  • Kijusi ni kikubwa mno kwa fupanyonga ya mama (hali inayoitwa kutowiana kwa fupanyonga na kijusi).

  • Uterasi ina umbo lisilo la kawaida au ina uvimbe kama vile tumbawe.

  • Kijusi kina kasoro ya kuzaliwa.

  • Kuna zaidi ya kijusi kimoja (ujauzito zaidi).

Mkao na Uwasilishaji wa Kijusi

Kuelekea mwisho wa ujauzito, kijusi huingia katika nafasi kwa ajili ya kujifungua. Kwa kawaida, utaratibu ni wa kichwa kutangulia na mkao ni wa osipati kutangulia (mtoto akiangalia upande wa uti wa mgongo wa mwanamke mjamzito) huku uso na mwili vikiwa vimekaa upande mmoja na shingo ikiwa imeinama.

Mabadiliko ya utaratibu wa kijusi kutoka ni pamoja na uso, kipaji, tako na bega. Mkao wa osipati kuja baadaye (mtoto kuelekea mbele, kuelekea mfupa wa fupanyonga wa mama) ni nadra zaidi kuliko mkao wa osipati kutangulia (mtoto kuelekea nyuma, kuelekea uti wa mgongo wa mama).

Utofauti wa Hali ya Ukaaji na Uwasilishaji wa Kijusi

Baadhi ya mabadiliko katika mkao na utaratibu yanayofanya kujifungua kuwa mgumu hutokea mara kwa mara.

Ukaaji wa kijusi kwa Kichwa Kuwa Chini Kikitazama Juu

Katika mkao wa osipati kuja baadaye (wakati mwingine huitwa "sunny-side up"), kijusi kinatanguliza kichwa (vertex presentation) lakini kimeelekea mbele (kuelekea mfupa wa fupanyonga wa mama—yaani, kinaangalia juu wakati mama amelala chali). Huu ni mkao wa kawaida sana ambao si ulemavu, lakini hufanya kujifungua kuwa mgumu zaidi kuliko wakati kijusi kipo katika mkao wa osipati kutangulia (kuelekea uti wa mgongo wa mama—yaani kinaangalia chini wakati mama amelala chali).

Wakati kijusi kinaangalia juu, mara nyingi shingo huwa imenyooka badala ya kutanuka, jambo ambalo linahitaji nafasi kubwa zaidi kwa ajili ya kichwa kupita kwenye njia ya uzazi. Kujifungua kwa usaidizi wa kifaa cha kuvuta au koleo au kujifungua kwa njia ya upasuaji unaweza kuhitajika.

Utaratibu wa mtoto kuwa kinyume

Katika utaratibu wa mtoto kuwa kinyume, matako ya mtoto au wakati mwingine miguu ndiyo inayotangulia kutoka wakati wa uzazi (kabla ya kichwa).

Wanapozaliwa kwa njia ya kawaida ya ukeni, watoto wanaotanguliza matako wako katika hatari zaidi ya kupata majeraha au hata kifo kuliko wale wanaotanguliza kichwa.

Sababu ya hatari kwa watoto walio katika utaratibu wa kuwa kinyume ni kwamba nyonga na matako ya mtoto hayana upana mkubwa kama kichwa. Kwa hivyo, nyonga na matako yanapopita kwenye mlango wa kizazi kwanza, njia ya uzazi inaweza isiwe na upana wa kutosha kuruhusu kichwa kupita. Aidha, kichwa kinapofuata baada ya matako, shingo inaweza kupinda kidogo kuelekea nyuma. Shingo inapopinda kuelekea nyuma huongeza upana unaohitajika kwa ajili ya uzazi ikilinganishwa na wakati kichwa kinapokuwa kimeinama mbele huku kidevu kikiwa kimegusisha kifua, ambao ndio mkao rahisi zaidi kwa ajili ya uzazi. Hivyo, mwili wa mtoto unaweza kuzaliwa na kisha kichwa kikakwama na kushindwa kupita kwenye njia ya uzazi. Wakati kichwa cha mtoto kinapokwama, hii huleta shinikizo kwenye kitovu ndani ya njia ya uzazi, hivi kwamba oksijeni kidogo sana inaweza kumfikia mtoto. Uharibifu wa ubongo kutokana na ukosefu wa oksijeni hutokea mara nyingi zaidi miongoni mwa watoto wanaozaliwa kwa kao la makalio kuliko wale wanaotanguliza kichwa.

Katika uzazi wa kwanza, matatizo haya yanaweza kutokea mara nyingi zaidi kwa sababu tishu za mwanamke hazijawahi kuvutika kutokana na vizazi vilivyotangulia. Kwa sababu ya hatari ya majeraha au hata kifo kwa mtoto, kujifungua kwa njia ya upasuaji hupendekezwa zaidi wakati kijusi kipo katika utaratibu wa mtoto kuwa kinyume, isipokuwa kama daktari ana uzoefu mkubwa na ujuzi wa kutosha wa kuzalisha watoto katika kao la makalio, au ikiwa hakuna kituo chenye vifaa vya kutosha kufanya upasuaji wa kumtoa mtoto.

Utaratibu wa mtoto kuwa kinyume una uwezekano mkubwa wa kutokea katika mazingira yafuatayo:

  • Uchungu wa uzazi kuanza mapema mno (uchungu wa uzazi kabla ya wakati).

  • Kuna zaidi ya kijusi kimoja (ujauzito zaidi).

  • Uterasi kuwa na umbo lisilo la kawaida au kuwa na uvimbe usio wa kawaida kama vile tumbawe.

  • Kijusi kina kasoro ya kuzaliwa.

Wakati mwingine daktari anaweza kugeuza kijusi ili kichwa kitangulie kabla ya uchungu kuanza kwa kufanya utaratibu unaohusisha kukshinikiza fumbatio la mwanamke mjamzito na kujaribu kumgeuza mtoto. Jaribio la kumgeuza mtoto huitwa external cephalic version (ECV) na kwa kawaida hufanywa katika wiki ya 37 au 38 ya ujauzito. Wakati mwingine wanawake hupewa dawa (kama vile terbutaline) wakati wa utaratibu huu ili kuzuia misuli ya uterasi kubana.

Utaratibu mwingine

Katika utaratibu wa uso kutangulia, shingo ya mtoto hujipinda kuelekea nyuma hivi kwamba uso ndio unaotangulia badala ya utosi wa kichwa.

Katika utaratibu wa kipaji kutangulia, shingo imejipinda kiasi hivi kwamba kipaji cha uso ndicho kinachotangulia.

Kwa kawaida, kijusi hakibaki katika utaratibu wa uso au kipaji kutangulia. Utaratibu huu mara nyingi hubadilika na kuwa wa kichwa kutangulia (vertex) kabla au wakati wa uchungu. Usipobadilika, mara nyingi upasuaji wa kumtoa mtoto hupendekezwa.

Katika ulalo wa kingamo, kijusi hulala kimlalo katika njia ya uzazi na hutanguliza bega kwanza. Upasuaji wa kumtoa mtoto hufanywa, isipokuwa kama kijusi ni cha pili kwa mapacha. Katika hali kama hiyo, kijusi kinaweza kugeuzwa ili kizaliwe kupitia uke.