Kwa bahati mbaya, familia nyingi hulazimika kukabiliana na changamoto za kihisia za kumtunza mtoto ambaye ni mgonjwa sana au anayekufa. Watoto wanaougua sana au wanaokufa wanaweza kusaidiwa kupitia huduma ya kupunguza maumivu, huduma ya wagonjwa mahututi, au zote mbili. Huduma ya wagonjwa mahututi na huduma ya kupunguza maumivu ni aina maalum za huduma zinazowasaidia watu wenye magonjwa makali na yanayobadilisha maisha. Wahudumu wa huduma ya kupunguza maumivu na huduma ya wagonjwa mahututi wanaweza kusaidia katika nyanja nyingine za ugonjwa, kama vile kudhibiti maumivu, na wanaweza kutoa usaidizi wa kihisia.
(Angalia pia Ugonjwa na Kifo kwa Watoto Wachanga.)
Kifo cha Mtoto
Mara nyingi kifo cha mtoto hutokea hospitalini au katika idara ya dharura. Kifo kinaweza kutokea baada ya ugonjwa wa muda mrefu, kama vile saratani, au ghafla na bila kutarajiwa, kama vile baada ya jeraha, maambukizi makali, au kifo cha ghafla kisichotarajiwa cha mtoto mchanga (SUID).
Kifo cha mtoto kinaweza kuwa kigumu kwa familia kuelewa na kukubali. Kwa wazazi, kifo cha mtoto kinamaanisha kwamba lazima wasalimu ndoto na matumaini yao ya kuongeza mtoto kwenye familia yao na mustakabali waliotarajia na mtoto huyo. Wakiwa wanaomboleza, huenda wazazi wasiweze kukidhi mahitaji ya wanafamilia wengine, wakiwemo watoto wengine. Ushauri nasaha kutoka kwa mtaalamu mwenye ujuzi wa kufanya kazi na familia ambazo zimepitia kifo cha mtoto unaweza kusaidia.
Wakati mwingine wazazi hukabiliana na kifo cha mtoto kwa kupanga haraka ujauzito mwingine, labda katika jaribio la kupata mtoto "mbadala". Wazazi wanaweza kuelekeza hisia na matarajio yao kuhusu mtoto aliyekufa kwa mtoto mbadala. Wasiwasi na hofu ya kupoteza mtoto mwingine inaweza kufanya iwe vigumu kwao kujenga uhusiano na mtoto mpya. Mtoto anayezaliwa baada ya mtoto mwingine kufariki yuko katika hatari ya kupata ugonjwa wa mtoto mbadala au ugonjwa wa mtoto mdhaifu.
Kwa ugonjwa wa mtoto mbadala, wazazi hutegemea mtoto aliyezaliwa baada ya kufiwa na mtoto mkubwa apunguze huzuni yao na kujaza pengo lililoachwa na mtoto waliyempoteza. Wanaweza kukata tamaa wakati huzuni yao haipungui na hii inaweza kuathiri vibaya uwezo wao wa kuwa na uhusiano na kumlea mtoto wao mpya.
Kwa ugonjwa wa mtoto dhaifu, wazazi wanaweza kumlinda kupita kiasi na kufikiri mtoto aliyezaliwa baada ya kufiwa na mtoto mkubwa yuko katika hatari ya kupata matatizo ya kitabia, ukuaji, au kiafya na anahitaji utunzaji na ulinzi maalum kutokana na madhara yanayokisiwa.
Wazazi wanaoomboleza kifo cha mtoto wanaweza kukabiliwa na tatizo la kutoweza kuwa na uhusiano wa kihisia na mtoto mpya. Hisia hizi huwa ni za kawaida. Ushauri nasaha kwa wazazi na ndugu husaidia.
Kusaidia Watoto Kukabiliana na Kifo na Kufa
Kutembelea Watoto au Watu Wazima Walio Wagonjwa
Wazazi wanaweza kumuuliza daktari wa mtoto wao au wataalamu wengine wa afya kama wanapaswa kumruhusu mtoto wao kumtembelea mtoto au mtu mzima mgonjwa sana. Baadhi ya watoto wanaweza kuomba kuwatembelea wanafamilia au marafiki wanaokufa. Wazazi wanapaswa kuwaandaa watoto kwa ajili ya ziara kama hiyo ili wajue cha kutarajia. Wazazi wanaweza kuwasaidia watoto wao kujiandaa kwa kuwaambia kwamba mtu huyo anaweza kuonekana tofauti lakini ni mtu yule yule. Mtu huyo anaweza kuonekana mgonjwa, anaweza kuwa amepoteza au kuongeza uzito, anaweza kuwa amepoteza nywele zake, au huenda asiweze kuwasiliana kama alivyokuwa akifanya hapo awali kwa sababu ya ugonjwa.
Kifo cha Mwanafamilia au Mpendwa
Kiasi ambacho watoto wanaweza kuelewa kuhusu kifo kinategemea sana kiwango chao cha ukuaji. Watoto wanahitaji kuelezwa kifo cha mpendwa au rafiki kwa kiwango wanachoelewa. Kwa mfano, watoto wa umri wa shule ya chekechea wanaweza kuwa na uelewa mdogo kuhusu kifo. Wazazi wanaweza kujaribu kuelezea kifo kwa kukihusisha na tukio lililopita, kama vile kifo cha mnyama kipenzi wa familia. Watoto wakubwa wanaweza kuelewa kifo kwa urahisi zaidi.
Ingawa inaweza kuonekana busara kufanya hivyo wakati huo, kifo hakipaswi kulinganishwa na "kulala na kutoamka kamwe," kwa sababu mtoto anaweza kuogopa kulala.
Kuhudhuria mazishi
Mara nyingi wazazi hujiuliza kama wawapeleke watoto kwenye mazishi. Uamuzi huu unapaswa kufanywa kibinafsi, na watoto wanapaswa kuhusishwa katika kufanya uamuzi ikiwezekana. Watoto wanapohudhuria mazishi, rafiki wa karibu au jamaa anapaswa kuandamana nao ili kutoa msaada wakati wote, na watoto wanapaswa kuruhusiwa kuondoka wakitaka.
Wazazi wanapaswa kuelewa kwamba watoto wanaweza kuwa na udadisi na kuuliza maswali mengi kuhusu kifo. Wazazi wanapaswa kuwafahamisha watoto kwamba ni sawa kwao kuuliza maswali.
Ikiwa janga litaathiri mtu mwingine, watoto wanaweza kuhisi kujiamini zaidi, na kusaidika zaidi, ikiwa wanaweza kuchangia. Kwa mfano, watoto wanaweza:
Kuchuma maua
Kuandika au kuchora kadi
Kufunga zawadi
Kukusanya chakula, pesa, nguo, au vifaa vya kuchezea
Ikiwa mtoto anaonekana kuwa mpweke au mwenye huzuni baada ya kufiwa, anakataa kushiriki katika shughuli za kawaida, au anakuwa mgomvi, mzazi anapaswa kutafuta msaada wa kitaalamu ili kumsaidia mtoto.
Taarifa Zaidi
Nyenzo zifuatazo za lugha ya Kiingereza zinaweza kuwa muhimu. Tafadhali kumbuka kuwa Mwongozo hauwajibiki kwa maudhui ya nyenzo hizi.
Huduma hizi hutoa taarifa kuhusu usaidizi kwa wazazi, walezi, na ndugu baada ya mtoto kufariki: