Disleksia ni tatizo maalum la kusoma linalohusisha ugumu wa kutenganisha maneno ya pekee kutoka kwenye makundi ya maneno na sehemu za maneno (fonimu) ndani ya kila neno.
Watoto walioathiriwa wanaweza kuchelewa kuanza kuzungumza, kuwa na matatizo ya kutamka maneno, au kuwa na ugumu wa kuchanganya sauti au kutambua sauti ndani ya maneno.
Vipimo vya kitaaluma na akili vinatolewa.
Matibabu yanahusisha mafunzo ya moja kwa moja katika utambuzi wa maneno.
Disleksia ni aina maalum ya tatizo la kujifunza. Hakuna makadirio ya idadi ya watoto walioathirika na disleksia, lakini takribani asilimia 15 ya watoto shuleni hupokea marekebisho au mafunzo maalum kwa ajili ya ugumu wa kusoma. Hutambuliwa kwa wavulana wengi kuliko wasichana. Hata hivyo, inaweza kutotambulika mara nyingi zaidi kwa wasichana. Disleksia huonekana mara nyingi katika familia.
Disleksia hutokea wakati ubongo unapata ugumu kuunganisha sauti na alama (herufi). Ugumu huu husababishwa na matatizo yasiyoeleweka vizuri katika baadhi ya muunganiko wa ubongo. Matatizo haya yapo kuanzia kipindi anapozaliwa na yanaweza kusababisha kasoro ya tahajia na uandishi na kupungua kwa kasi na usahihi wakati wa kusoma kwa sauti. Ingawa kubadilisha herufi huku kunakotokea mara kwa mara kwa watoto wenye disleksia kunapendekeza matatizo ya kuona, katika visa vingi matatizo hayo yanahusiana na jinsi sauti zinavyopokelewa na ubongo, yaani, jinsi ubongo unavyozielewa na kuzifasiri. Watu wenye disleksia hawana matatizo ya kuelewa lugha inayozungumzwa.
Dalili za Kilema cha Kusoma
Watoto wa umri wa shule ya chekechea wenye disleksia wanaweza
Kuchelewa kuzungumza
Kutatizika kutamka maneno (matatizo ya matamshi)
Kutatizika kukumbuka majina ya herufi, nambari na rangi
Kutatizika kujibu maswali ya maelezo ya hisabati licha ya kuwa na ujuzi wa kawaida wa hisabati
Watoto wenye disleksia mara nyingi hutatizika kuunganisha sauti, kuunda maneno yanayofanana kimaandishi, kutambua nafasi za sauti katika maneno, kugawanya maneno kuwa sauti, na kubaini idadi ya sauti katika maneno. Kuchelewa au kusitasita katika kuchagua maneno, kubadilisha maneno, na kutambua herufi na picha ni dalili za mapema za disleksia. Matatizo ya kumbukumbu ya muda mfupi kwa sauti na kupanga sauti kwa mpangilio sahihi ni jambo la kawaida.
Watoto wengi wenye disleksia huchanganya herufi na maneno na yale yanayofanana. Kubadilisha herufi wakati wa kuandika—kwa mfano, on badala ya nona saw badala ya was—au herufi zenye utata—kwa mfano, b badala ya d, w badala ya m, n badala ya h—ni jambo la kawaida. Hata hivyo, watoto wengi wasio na kilema cha kusoma hubadilisha herufi wakati wa miaka ya mwanzoni ya shule ya msingi.
Utambuzi wa Kilema cha Kusoma
Tathmini ya usomaji
Tathmini za usemi, lugha, na kusikia
Tathmini ya Kisaikolojia
Watoto ambao hawaendelei katika ujuzi wa kujifunza maneno kufikia katikati au au mwishoni mwa darasa la kwanza wanapaswa kujaribiwa kwa dyslexia na matatizo mengine yanayoweza kuathiri ujifunzaji. Upimaji kawaida hufanywa na wafanyakazi wa shule na unajumuisha vipimo vya hotuba, lugha, na kusikia, vipimo vya akili, na vipimo vya ujuzi wa kimasomo.
Matibabu ya Kilema cha Kusoma
Mikakati ya kielimu
Matibabu bora kwa matatizo ya utambuzi wa maneno ni mafunzo ya moja kwa moja yanayojumuisha mbinu za hisia nyingi. Aina hii ya matibabu inahusisha kufundisha foniki kwa kutumia ishara mbalimbali, kawaida kando kando na, inapowezekana, kama sehemu ya mpango wa usomaji.
Maagizo yasiyo ya moja kwa moja ya utambuzi wa maneno pia yanasaidia. Maagizo haya kwa kawaida yanajumuisha mafunzo ya kuboresha matamshi ya maneno au uelewa wa usomaji. Watoto hufundishwa jinsi ya kuchakata sauti kwa kuchanganya sauti ili kuunda maneno, kwa kutenganisha maneno katika sehemu, na kwa kutambua nafasi za sauti katika maneno.
Maagizo ya ujuzi wa vipengele kwa ajili ya utambuzi wa maneno pia yanasaidia. Inajumuisha mafunzo ya kuchanganya sauti ili kuunda maneno, kugawanya maneno katika sehemu za maneno, na kutambua nafasi za sauti dhani ya maneno.
Sheria ya Elimu ya Watu Wenye Ulemavu ya Serikali Kuu (IDEA) inahitaji shule za umma kutoa elimu bila malipo na inayofaa kwa watoto na vijana wenye disleksia au matatizo mengine ya kujifunza. Ni lazima elimu itolewe katika mazingira yenye vizuizi kidogo zaidi, jumuishi zaidi iwezekanavyo—yaani, katika mazingira ambayo watoto wana kila nafasi ya kuingiliana na wenzao wasio na ulemavu na kupata ufikiaji sawa wa rasilimali za jamii. Sheria ya Wamarekani Wenye Ulemavu na Kifungu cha 504 cha Sheria ya Urekebishaji pia huhakikisha kuwa wanajumuishwa katika shule na maeneo mengine ya umma.
Kadri watoto wenye disleksia wanavyoendelea kukua, mikakati ya fidia inaweza kusaidia. Mikakati hii inaweza kujumuisha matumizi ya vitabu vya sauti, visomaji vya skrini ya kompyuta (vinavyopatikana kwenye kompyuta nyingi), vinasa sauti vya kidijitali, na marekebisho mengine ya kiteknolojia.
Matibabu mengine (kwa mfano, mafunzo ya kusaidia kuona, mafunzo ya utambuzi, mafunzo ya ujumuishaji wa kusikia) na matibabu ya dawa hayajathibitishwa na hayapendekezwi.
Taarifa Zaidi
Nyenzo zifuatazo za lugha ya Kiingereza zinaweza kuwa muhimu. Tafadhali kumbuka kuwa MWONGOZO hauwajibiki kwa maudhui ya nyenzo hizi.
Sheria ya Elimu ya Watu Wenye Ulemavu (IDEA): Sheria ya Marekani inayotoa elimu ya umma mwafaka bila malipo kwa watoto wenye ulemavu wanaostahiki na kuhakikisha elimu maalum na huduma zinazohusiana kwa watoto hao
Shirika la Kimataifa Linaloshughulikia Disleksia: Shirika linalotoa rasilimali na huduma kwa wataalamu, watetezi, watu binafsi, na familia zilizoathiriwa na disleksia
Sheria ya Wamarekani wenye Ulemavu: Sheria ya Marekani inayokataza ubaguzi unaotokana na ulemavu
Kifungu cha 504 cha Sheria ya Urekebishaji: Sheria ya Marekani inayohakikisha haki fulani kwa watu walio na ulemavu
Shirika Linalotoa Msaada kwa Walemavu wa Kujifunza Nchini Amerika (LDA): Shirika linalotoa rasilimali za kielimu, usaidizi, na utetezi kwa watu wenye ulemavu wa kujifunza