Subacute sclerosing panencephalitis, ugonjwa wa ubongo unaoendelea na ambao kwa kawaida husababisha kifo, ni tatizo nadra la surua litokealo miezi au miaka baadaye na husababisha kuzorota kwa akili, kutetemeka kwa misuli, na kifafa.
Subacute sclerosing panencephalitis husababishwa na virusi vya surua.
Dalili za kwanza kwa kawaida huwa ni mafanikio duni shuleni, kusahau, milipuko ya hasira, kukengeushwa fikira, kukosa usingizi, na kuona mambo ambayo hayapo na yasiyoeleweka.
Utambuzi unategemea dalili.
Hakuna matibabu maalum ya ugonjwa huu.
Ugonjwa huu kwa kawaida unaweza kusababisha kifo.
Subacute sclerosing panencephalitis (SSPE) hudhaniwa kuwa ni maambukizi ya muda mrefu ya virusi vya surua. Wakati mwingine virusi huingia kwenye ubongo wakati wa maambukizi ya surua. Virusi vya surua vinaweza kusababisha dalili za haraka za maambukizi ya ubongo (encephalitis) au virusi vinaweza kusalia kwenye ubongo kwa muda mrefu bila kusababisha matatizo.
SSPE hutokea kwa sababu virusi vya surua hufufuka tena. Hapo awali nchini Marekani, kwa sababu zisizojulikana, ugonjwa huo ulitokea kwa takriban watu 7 hadi 300 kwa kila watu milioni moja waliokuwa na maambukizi ya surua na kwa takriban mtu 1 kwa kila watu milioni moja waliopokea chanjo ya surua. Hata hivyo, madaktari wanafikiri watu ambao walipata SSPE baada ya chanjo huenda walikuwa na kisa cha surua isiyokithiri ambayo haikutambuliwa kabla ya kupata chanjo na kwamba maambukizi ya surua, na sio chanjo, ndiyo yaliyosababisha SSPE.
SSPE haipatikani sana nchini marekani na Ulaya Magharibi kwa sababu ya kuenea kwa chanjo ya surua. Hata hivyo, uchambuzi wa milipuko ya hivi karibuni ya surua unaonyesha kuwa kiwango cha SSPE kinaweza kuwa kikubwa zaidi kuliko ilivyodhaniwa hapo awali.
Wanaume huathiriwa mara nyingi zaidi kuliko wanawake. Hatari ya kupata SSPE ni kubwa zaidi kwa watu wanaopata surua kabla ya kufikisha umri wa miaka 2. SSPE kwa kawaida huanza kwa watoto au vijana, kwa kawaida kabla ya umri wa miaka 20.
Dalili za SSPE
Dalili za kwanza za SSPE huenda zikawa mafanikio duni katika kazi za shule, kusahau, milipuko ya hasira, kukengeushwa fikira, kukosa usingizi, na kuona mambo ambayo hayapo na ambayo hayaeleweki. Mienendo ya ghafla ya mikono, kichwa, au mwili huenda ikatokea. Hatimaye, ugonjwa wa kifafa unaweza kutokea, pamoja na mienendo isiyo ya kawaida ya misuli isiyoweza kudhibitiwa. Akili na usemi huendelea kuzorota.
Baadaye, misuli hukakamaa zaidi, na inaweza kuwa vigumu kumeza. Ugumu wa kumeza wakati mwingine husababisha watu kupaliwa na mate yao, na kusababisha nimonia. Watu wanaweza kuwa vipofu.
Katika awamu za mwisho, joto la mwili linaweza kuongezeka, na shinikizo la damu na mapigo ya moyo kuwa yasiyo ya kawaida.
Utambuzi wa SSPE
Vipimo kwenye maji ya ubongo au damu
Vipimo vya picha
Daktari hushuku SSPE kwa vijana ambao wana matatizo ya akili na kutetemeka kwa misusli.
Utambuzi huo huthibitishwa kwa uchunguzi wa maji ya ubongo, kipimo cha damu kinachoonyesha viwango vya juu vya kingamwili kwa virusi vya surua, elektroencephalogram ambayo sio ya kawaida (EEG), na upigaji picha wa mwangwi wa sumaku (MRI) au tomografia iliyokadiriwa (CT) inayoonyesha matatizo ya ubongo.
Biopsi ya ubongo inaweza kuhitaji kufanywa ikiwa vipimo haviwezi kuonyesha chanzo.
Matibabu ya SSPE
Dawa ya kupunguza shinikizo la damu
Hakuna kinachoweza kufanywa kuzuia kuendelea kwa subacute sclerosing panencephalitis.
Dawa za kuzuia kifafa zinaweza kutumiwa ili kudhibiti au kupunguza vifafa.
Ubashiri wa SSPE
SSPE karibu kila mara husababisha kifo ndani ya mwaka 1 hadi miaka 3.
Ingawa kisababishi cha kifo kwa kawaida ni nimonia, nimonia hutokana na udhaifu mkubwa na udhibiti usio wa kawaida wa misuli ambao husababishwa na ugonjwa huo.
Baadhi ya watu huwa na vipindi ambapo wana afya njema na vipindi vya kuibuka kwa ugonjwa huo.