Retinoblastoma

NaKee Kiat Yeo, MD, Harvard Medical School
Imekaguliwa naMichael SD Agus, MD, Harvard Medical School
Imepitiwa/Imerekebishwa Jun 2024 | Imebadilishwa Jul 2024
v822731_sw

Retinoblastoma (saratani ya macho kwa watoto) ni saratani ya retina, eneo linalohisi mwanga nyuma ya jicho.

  • Retinoblastoma zinaweza kutokea kutokana na mabadiliko ya kijenetiki.

  • Mtoto anaweza kuwa na mboni nyeupe au macho yanayopindana au mara kwa mara kuwa na matatizo ya kuona.

  • Madaktari mara nyingi wanaweza kutambua retinoblastoma kwa kuangalia ndani ya jicho wakitumia kifaa maalum wakati mtoto ametiwa ganzi.

  • Matibabu yanaweza kuhusisha upasuaji, tibakemikali au wakati mwingine tiba kwa njia ya eksirei.

(Angalia pia Muhtasari wa Saratani ya Utotoni.)

Retinoblastoma huwakilisha takriban 2% ya saratani za utotoni. Aina hii ya saratani mara nyingi huathiri watoto walio na umri wa chini ya miaka 2. Retinoblastoma hutokea kwa watoto pekee.

Saratani hii hutokana na mabadiliko katika jeni fulani zinazodhibiti ukuaji wa macho. Wakati mwingine, mabadiliko hayo hupitishwa (kurithiwa) kutoka kwa mzazi. Wakati mwingine, hutokea ghafla (sio kurithiwa) mapema sana wakati wa ukuaji wa kiinitete.

Wakati mabadiliko yanaporithiwa, watoto walioathiriwa wanaweza kupitisha mabadiliko hayo kwa watoto wao. Kuna uwezekano wa 50% kwamba mabadiliko hayo yatapitishwa ikiwa mzazi mmoja atakuwa na mabadiliko hayo. Ikiwa mabadiliko hayo yatapitishwa, watoto wengi wenye mabadiliko hayo watapata retinoblastoma. Retinoblastoma huwa ya kurithi kwa watoto wote wenye saratani ya macho yote mawili na kwa 15% ya watoto wenye saratani ya jicho moja.

Wakati mwingine, mabadiliko haya hutokea baadaye katika ukuaji wa kiinitete na hutokea tu katika seli za macho za kiinitete. Katika hali kama hizo, mabadiliko hayo hayarithiwi na hayawezi kupitishwa kwa watoto.

Kuangalia Retina

Retinoblastoma kwa kawaida haienei zaidi ya jicho, lakini mara kwa mara huenea hadi kwenye ubongo kupitia neva ya jicho (neva inayoenda kutoka jicho hadi kwenye ubongo). Mara chache, huenda ikaenea hadi maeneo mengine, kama vile uboho na mifupa.

Dalili za Retinoblastoma

Dalili za retinoblastoma zinaweza kujumuisha mboni nyeupe (leukocoria) au macho yanayopindana (makengeza).

Leukokoria katika Mtoto Mchanga mwenye Retinoblastoma
Ficha Maelezo

Mboni nyeupe (leukokoria) ni dalili ya retinoblastoma.

Kwa idhini ya mchapishaji. Kutoka kwa Scott I, Warman R, Murray T: Atlasi ya Ophthalmolojia. Imehaririwa na RK Parrish II na TG Murray. Philadelphia, Current Medicine, 2000.

Retinoblastoma kubwa zinaweza kuathiri uwezo wa kuona lakini huwa na dalili chache zaidi.

Ikiwa saratani imeenea, dalili zinaweza kujumuisha maumivu ya kichwa, kupoteza hamu ya kula, maumivu katika mfupa ulioathiriwa, au kutapika.

Utambuzi wa Retinoblastoma

  • Kuangalia ndani ya jicho kwa kutumia kifaa maalum wakati mtoto ametiwa ganzi

  • Ultrasonografia, tomografia ya kompyuta (CT), au upigaji picha kwa mwangwi wa sumaku (MRI) na wakati mwingine tomografia ya mshikamano wa macho

  • Wakati mwingine picha ya mfupa, uchunguzi wa uboho, na uondoaji wa maji ya uti wa mgongo

Ikiwa daktari anashuku retinoblastoma, mtoto hutiwa ganzi ya mwili mzima, jambo ambalo humfanya mtoto apoteze fahamu, na macho yote mawili huchunguzwa. Lenzi nyepesi na maalum (ophthalmoscopia isiyo ya moja kwa moja) hutumika kutazama kupitia lenzi na mboni ya mtoto kwenye retina. Nusukaputi ya mwili mzima ni muhimu kwa sababu watoto wadogo hawawezi kushirikiana wakati wa uchunguzi huu makini na unaochukua muda unaohitajika ili kutambua retinoblastoma.

Saratani inaweza pia kutambuliwa kwa kutumia picha ya mawimbi ya sauti, CT, au MRI ya macho. Vipimo hivi pia husaidia kubaini kama saratani imeenea hadi kwenye ubongo. Tomografia ya mshikamano wa macho ni kipimo kingine cha picha ambacho wakati mwingine hufanywa.

Madaktari wanaweza pia kufanya uondoaji wa maji ya uti wa mgongo (kutombolewa kwa kiuno) ili kutafuta seli za saratani katika sampuli ya maji ya ubongo na uti wa mgongo. Kupata seli za saratani katika maji haya ni ushahidi zaidi kwamba saratani imeenea hadi kwenye ubongo.

Kwa sababu saratani inaweza kuenea hadi kwenye mifupa au uboho, watoto wenye maumivu ya mifupa au dalili nyingine wanaweza kupigwa picha ya mfupa na sampuli ya uboho inaweza kuondolewa ili ifanyiwe uchunguzi.

Watoto walio na retinoblastoma wanapaswa kumuona mtaalamu wa kijenetiki na kufanyiwa upimaji wa jeni. Mtaalamu anaweza kuwashauri wazazi kama wanafamilia wengine wako hatarini na kama vipimo vingine vinapaswa kufanywa. Kwa kawaida, ikiwa watoto wana jeni la retinoblastoma la kurithi, wazazi na kaka na dada zao wanapaswa pia kupimwa kwa jeni iliyobadilika. Ndugu walio na jeni iliyobadilika wanapaswa kuchunguzwa macho yao kwa retinoblastoma kwa vipindi vinavyoamuliwa kulingana na umri wao na hatari ya kupata saratani.

Ikiwa upimaji wa jeni haupatikani, watoto wote ambao wana mzazi au ndugu aliyekuwa na retinoblastoma wanapaswa kufanyiwa uchunguzi sawa wa mara kwa mara wa macho. Wanafamilia wazima wa mtoto aliye na retinoblastoma pia wanahitaji kufanyiwa uchunguzi wa macho. Ingawa watu wazima hawatapata retinoblastoma, jeni inayosababisha retinoblastoma inaweza pia kusababisha uvimbe wa macho usio saratani (usiodhuru) unaoitwa retinosaitoma.

Matibabu ya Retinoblastoma

  • Kuondolewa kwa jicho kwa upasuaji

  • Tibakemikali

  • Tiba kwa njia ya eksirei, leza, na tiba ya cryotherapy (tiba ya baridi)

(Angalia pia Kanuni za Matibabu ya Saratani na Upasuaji wa Saratani.)

Wakati jicho moja tu limeathiriwa na jicho hilo lina uwezo mdogo wa kuona au halina uwezo wa kuona kabisa, madaktari kwa kawaida huondoa mboni nzima ya jicho pamoja na sehemu ya neva ya jicho.

Wakati saratani inapoathiri macho yote mawili, madaktari hujaribu kuhifadhi uwezo mdogo wa kuona kwa kutibu saratani bila kuondoa mboni zote mbili za macho, ingawa wakati mwingine huwa wanaondoa jicho lililoathiriwa zaidi. Chaguo za matibabu ni pamoja na dawa za tibakemikali zinazodungwa moja kwa moja kupitia ateri kuu ya damu inayoleta damu kwenye jicho (inayoitwa tibakemikali ya ndani ya ateri), tiba kwa njia ya eksirei, leza, kugandisha (cryotherapy), au, kwa saratani ndogo sana, viraka vinavyojumuisha nyenzo zenye mionzi (brachytherapy).

Mchanganyiko wa tibakemikali inayotolewa kwa mdomo au mshipa (kama vile carboplatin, etoposide, na vincristine, au cyclophosphamide pamoja na vincristine) unaweza kutumika kupunguza uvimbe mkubwa katika jicho moja, kupunguza uvimbe ulio katika macho yote mawili, kutibu saratani ambayo imeenea zaidi ya jicho, au kutibu saratani inayorudi baada ya matibabu ya kwanza. Tibakemikali hutumika pamoja na chaguo nyingine za matibabu kwa sababu ikiwa peke yake kwa kawaida haiwezi kuponya saratani hii.

Tiba kwa njia ya eksirei kwenye jicho ina madhara makubwa, kama vile mtoto wa jicho, kupungua kwa uwezo wa kuona, jicho kavu zaidi, na upotevu wa tishu zinazozunguka jicho. Mifupa ya uso huenda isikue kawaida, na kusababisha mwonekano wenye ulemavu. Aidha, hatari ya kupata saratani ya pili huongezeka katika eneo ambalo tiba kwa njia ya eksirei hutolewa.

Baada ya matibabu, daktari ambaye ni mtaalamu wa kutibu saratani kwa watoto (daktari wa saratani ya watoto) na mtaalamu wa macho wanapaswa kuendelea kumfuatilia mtoto kwa sababu ya hatari ya saratani kurudi au saratani ya pili kutokea.

Ubashiri wa Retinoblastoma

Kupitia matibabu, watoto walio na retinoblastoma ambayo haijaenea zaidi ya retina hupona zaidi ya 90% ya wakati. Ubashiri ni mbaya kwa watoto ambao saratani imeenea.

Bila matibabu, retinoblastoma husababisha kifo kwa watoto wengi ndani ya miaka 2.

Watoto walio na aina ya retinoblastoma ya kurithi wana hatari kubwa ya kupata saratani ya pili, kama vile sarcoma za tishu laini, melanoma, na osteosarkoma. Karibu nusu ya saratani za pili hutokea pale ambapo tiba kwa njia ya eksirei ilitolewa. Karibu 70% ya wakati, saratani ya pili hutokea ndani ya miaka 30 baada ya retinoblastoma.

Taarifa Zaidi

Nyenzo zifuatazo za lugha ya Kiingereza zinaweza kuwa muhimu. Tafadhali kumbuka kuwa Mwongozo hauwajibiki kwa maudhui ya nyenzo hizi.

  1. The American Cancer Society: Ikiwa Mtoto Wako Ametambuliwa kuwa na Saratani: Rasilimali kwa wazazi na wapendwa wa mtoto ambaye ana saratani ambayo hutoa taarifa kuhusu jinsi ya kukabiliana na baadhi ya matatizo na maswali yanayojitokeza mara tu baada ya mtoto kugunduliwa na ugonjwa huo