Maambukizi ya Homa Kali ya Ini

Imepitiwa/Imerekebishwa May 2025 | Imebadilishwa Jul 2025
v34408826_sw

Ni nini maana ya maambukizi ya homa kali ya ini?

Homa kali ya ini ni uvimbe (kuvimba) wa ini lako ambao huja haraka na kuisha haraka zaidi pia. Maambukizi ya homa kali ya ini wakati mwingine huwa homa ya ini inayodumu kwa muda mrefu. Homa ya ini ya aina hii hudumu kwa muda mrefu.

  • Maambukizi ya homa kali ya ini mara nyingi husababishwa na virusi.

  • Dalili zako zinaweza kuwa ndogo zinazofanana na za homa ya mafua au dalili kali na za kutishia maisha

  • Madaktari hufanya vipimo vya damu ili kubaini iwapo una maambukizi ya homa kali ya ini na virusi vilivyoisababisha

  • Unaweza kupata chanjo (sindano) za kuzuia baadhi ya aina za homa ya ini inayosababishwa na virusi

  • Shughuli fulani, kama vile kuweka chale au kutoboa sehemu za mwili, kutumia kwa pamoja sindano za kudungia dawa za kulevya, au kuwa na wenzi wengi wa ngono, huongeza hatari yako ya kuugua homa ya ini

Ni nini husababisha homa kali ya ini?

  • Kuna aina 5 za virusi vya homa ya ini ambazo zinaweza kusababisha homa ya ini kali ya virusi na zinajulikana kama homa ya ini A, B, C, D na E

  • Virusi vya homa ya ini A ndivyo vinavyotokea sana kama kisababishi cha maambukizi ya ghafla ya homa ya ini

  • Kisababishi cha pili kinachotokea sana ni homa ya ini B

Virusi tofauti vya homa ya ini huenezwa kwa njia tofauti:

  • Homa ya ini A: kupitia maji au chakula kilichoharibiwa na kinyesi kutoka kwa watu walioambukizwa

  • Homa ya ini B: kupitia kugusana na damu au majimaji ya mwili ya watu walioambukizwa, kwa mfano, kwa kushiriki tendo la ngono au kutumia sindano kwa pamoja (kudungia dawa za kulevya au kuweka chale)—pia, mwanamke mjamzito anaweza kuambukiza mtoto wake virusi vya homa ya ini B

  • Homa ya ini C: kupitia kugusana na damu ya watu walioambukizwa, kwa mfano, kwa kutumia sindano kwa pamoja—kushiriki tendo la ngono hakusambazi virusi vya homa ya ini C

  • Homa ya ini D: kupitia mgusano na damu au viowevu vya mwili kutoka kwa watu walioambukizwa, kwa mfano, kwa kushiriki ngono au kushiriki sindano (ili kutumia dawa au kupata tatoo)—pia, wanawake wajawazito wanaweza homa ya ini D kwa mtoto wake

  • Homa ya ini E: kupitia maji au chakula kilichoharibiwa na kinyesi kutoka kwa watu walioambukizwa

Ni dalili zipi za maambukizi ya homa kali ya ini?

Huenda usionyeshe dalili zozote au huenda ukaonyesha dalili kama vile:

  • Kutohisi njaa kama kawaida

  • Homa, kutapika, au kuhisi kichefuchefu tumboni

  • Maumivu kwenye sehemu ya juu kulia ya tumbo yako, ambapo ini lako linapatikana

  • Ngozi na sehemu nyeupe za macho yako kugeuka kuwa manjano (homa ya nyongo ya manjano)

  • Mkojo mweusi

  • Kuchukia sigara, ikiwa unavuta

Dalili nyingi kwa kawida huwa zinatoweka ndani ya siku 3 hadi 10 na unaanza kujisikia vizuri. Hali ya ngozi na macho yako kuwa ya manjano inaweza kudumu kwa wiki 2 hadi 4.

Matatizo ya homa kali ya ini ni yapi?

Watu wengi wanakuwa hawana matatizo lakini wakati mwingine:

  • Ukiwa na homa ya ini A au B ini lako linashindwa kufanya kazi (ini kushindwa kufanya kazi)

  • Ukiwa na homa ya ini B, C, au D homa ya ini inakuwa sugu

  • Ukiwa na homa ya ini B, C, au D unaweza kupata saratani ya ini miaka mingi baadaye

Madaktari wanawezaje kujua kuwa nina homa kali ya ini?

Madaktari watafanya:

  • Vipimo vya damu ili kuona jinsi ini lako linavyofanya kazi na kuangalia ikiwa una virusi vya homa ya ini

  • Mara kwa mara, wataondoa kipande cha tishu ya ini lako kwa ajili ya uchunguzi kwa kuchukua sampuli yake kwa sindano ili kuichunguza chini ya hadubini

Je, madaktari wanatibu vipi homa kali ya ini?

Ikiwa una homa ya ini kiasi ya virusi kali:

  • Pengine utapona ndani ya wiki 4 hadi 8 bila matibabu maalumu

  • Daktari wako atakuwambia usinywe pombe au kutumia dawa fulani hadi uwe mwenye afya

Ikiwa una homa ya ini sugu ya virusi, huenda ukahitaji:

  • Kuhudumiwa hospitalini

  • Dawa zinazosaidia kuua virusi

  • Kwa nadra, kubadilisha ini

Je, ninawezaje kuzuia homa kali ya ini?

Unaweza kuchomwa sindano (chanjo) ili kuzuia maambukizi ya homa ya ini A au B. Watu nchini China pia wanapata chanjo ya homa ya ini E.

Ikiwa umegusana na mtu mwenye homa ya ini A au B na hujapata chanjo, unaweza kuchoma sindano (chanjo au globulini ya kinga) ambayo inasaidia kuzuia maambukizi hayo.

Unaweza pia kusaidia kuzuia homa ya ini kali ya virusi ikiwa:

  • Unanawa sana mikono yako kabla hujagusa chakula

  • Hushiri miswaki, nyembe na vitu vingine ambavyo vinaweza kuwa na damu ya watu wengine

  • Unafanya ngono salama, kama vile kutumia kondomu

  • Punguza idadi ya watu ambao unafanya nao ngono

  • Usishiriki sindano za kudunga dawa