Sirosisi ya ini

Imepitiwa/Imerekebishwa Imebadilishwa Apr 2025
v27318842_sw

Je, ini lako ni nini?

Ini ni kiungo kinachotoshana na mpira kwenye upande wa kulia wa tumbo lako, chini ya mbavu zako. Lina kazi nyingi muhimu:

  • Kutengeneza kioevu (nyongo) ambacho husaidia mwili wako kusaga mafuta

  • Kumeng’enya virutubisho kutoka kwenye njia yako ya mmeng'enyo wa chakula

  • Kutengeneza protini zinazosaidia damu kuganda

  • Kusaidia kuvunjavunja dawa na sumu ili mwili wako uweze kuziondoa

Mfumo wa Kusaga Chakula

Sirosisi ya ini ni nini?

Sirosisi ni ugonjwa ambapo tishu za kovu huchukua nafasi ya tishu za kawaida za ini. Kovu la tishu hukua ini lako linapoharibika mara kwa mara baada ya muda.

  • Sirosisi husababishwa hasa na kunywa pombe kupita kiasi kwa muda mrefu, kuwa na virusi vya homa ya ini, au kurundikana kwa mafuta kwenye ini lako (ini lenye mafuta)

  • Dalili ni pamoja na kutohisi njaa, kupungua uzani, na kujihisi mdhaifu na mchovu mwili mzima

  • Wakati mwingine madaktari wanaweza kutibu dalili na matatizo ya sirosisi, lakini uharibifu wa ini ni wa kudumu

Matatizo yatokanayo na sirosisi ni gani?

Sirosisi kali inayodumu kwa muda mrefu inaweza kusababisha matatizo kadhaa:

Ini kushindwa kufanya kazi husababisha matatizo mengi hatari:

  • Kutokwa na damu kupita kiasi

  • Matatizo ya ubongo (ubongo wako hautafanya kazi ipasavyo)

  • Figo kushindwa kufanya kazi

  • Ugumu wa kusaga na kufyonza chakula

Shinikizo la juu la damu kwenye mshipa wa portal husababisha damu kukwama kwenye mishipa inayounganishwa ini. Mishipa hii inaweza kutanuka na kujipinda. Mishipa iliyo kwenye ncha ya chini ya umio, tumboni, au kwenye rektamu inaweza kuathirika. Mishipa iliyotanuka, iliyojipinda ni dhaifu na iko katika hatari ya kuvuja damu, kwa hivyo unaweza:

  • Kutapika kiasi kikubwa cha damu

  • Kutoa damu nyingi kutoka kwenye rektamu yako

Ukivuja damu polepole na iendelee kwa muda mrefu, unaweza kuwa na kiwango cha chini cha damu (anemia). Ukivuja damu kwa haraka, shinikizo lako la damu linaweza kushuka sana (mshtuko). Unaweza hata kufariki.

Saratani ya ini inaweza kutokea. Ikiwa una ugonjwa wa sirosisi, daktari wako atakupiga picha ya ndani ya mwili kila baada ya miezi 6 ili kuchunguza kama una saratani ya ini.

Ni nini husababisha ugonjwa wa sirosisi?

Vyanzo vya sirosisi ni pamoja na:

  • Kunywa pombe kupita kiasi kwa muda mrefu

  • Kuwa na homa ya ini B au C sugu (ya muda mrefu)

Dalili za sirosisi ni nini?

Watu wengi wenye sirosisi hawaonyeshi dalili yoyote kwa miaka.

Unapopata dalili, zinaweza kujumuisha:

  • Kujihisi mgonjwa na uchovu

  • Kutohisi njaa na kupoteza uzani

  • Homa ya nyongo ya manjano (ngozi kuwa ya manjano na macho kuwa meupe)

  • Upele wa mwekundu hadi zambarau wa madoa madogo au makubwa

  • Kuwashwa kote

Ikiwa ugonjwa wa sirosisi umesababishwa na pombe au tatizo la ini la muda mrefu, unaweza pia kupata:

  • Misuli kudhoofika

  • Viganja vyekundu

  • Tumbo lililovimba (kutokana na majimaji mengi kupita kiasi)

  • Madoa madogo, mekundu yanayong'aa kwenye ngozi yako yenye mishipa membamba ya damu karibu nayo inayofanana na miguu ya buibui (angioma ya buibui)

  • Kuvimba kwa tezi za mate - tezi zinazotengeneza mate yako (mate)

  • Kuvimba kwa matiti, korodani, na nywele chache chini ya mikono (kwa wanaume)

Madaktari wanawezaje kujua kama nina ugonjwa wa sirosisi?

Daktari wako atashuku kuwa una ugonjwa wa sirosisi ikiwa unakunywa kupita kiasi au una homa ya ini na una baadhi ya dalili zilizoorodheshwa hapo juu. Ili kujua ikiwa una ugonjwa wa sirosisi, madaktari watafanya haya:

  • Vipimo vya damu ili kuona jinsi ini lako linavyofanya kazi (hakuna kipimo cha damu ambacho kinaweza kujua ikiwa kweli una ugonjwa wa sirosisi)

  • Wakati mwingine watafanya uchunguzi wa picha kama vile picha ya mawimbi sauti au uchanganuzi wa CT ya ini lako

Kuondoa kuipande cha tishu ya ini kwa ajili ya uchunguzi (pale ambapo kipande kidogo cha ini huondolewa ili kuangaliwa kwenye hadubini) kunaweza kuhitajika ikiwa vipimo vingine havina matokeo yanayoeleweka.

Madaktari hutibu vipi ugonjwa wa sirosisi?

Hakuna tiba ya sirosisi Uharibifu wa ini ni wa kudumu. Daktari atakutibu dalili zako. Unaweza pia kusaidia kuzuia ugonjwa wa sirosisi kuwa mbaya kwa kufanya yafuatayo:

  • Kuacha kunywa pombe

  • Ikiwa una homa ya ini C sugu, tumia dawa ili kuitibu

  • Epuka dawa zinazoweka mkazo kwenye ini (kama vile acetaminophen)

  • Kula vyakula vinavyokufaa

Iwapo una shinikizo la juu la damu kwenye mshipa wa portal na mishipa iliyotanuka, iliyojipinda kwenye umio wako (mrija unaounganisha koo na tumbo lako), madaktari wanaweza:

  • Kukupa dawa fulani zinazoitwa vizuizi vya beta ili kupunguza shinikizo la damu kwenye mishipa ya ini

  • Kutazama chini ya koo lako kwa kifaa kinachonyumbulika na kufunga mishipa iliyotanuka kwa kuidungia kwa dutu fulani au kuvivika mikanda maalum ya mpira.

Usipopata nafuu bada ya hayo, daktari wako anaweza kufanya upasuaji ili kubadilisha njia ya damu kutoka kwenye mishipa ya pota na kupunguza shinikizo.

Ikiwa ini lako lina ugonjwa na linashindwa kufanya kazi, unaweza kuhitaji kipandikizo cha ini (upasuaji wa kurekebisha ini lako ambalo lina ugonjwana ini zuri). Kwa sababu pombe itaharibu pia ini lililopandikizwa, kawaida madaktari hufanya tu upandikizaji ikiwa umeacha kunywa pombe.