
Ugonjwa wa kuchochewa kwa fupanyonga (PID) ni nini?
PID ni maambukizi kwenye uterasi, mfuko wa uzazi, kwenye mirija inayounganisha ovari zako na uterasi yako, mirija ya uzazi au kwenye vyote viwili. PID pia inaweza kusambaa kwenye ovari zako (viungo vya ngono ambavyo vinashikilia mayai yako) na kwenye mtiririko wa damu.
Ni nini husababisha ugonjwa wa kuchochewa kwa fupanyonga?
PID inasababishwa na bakteria kutoka kwenye uke wako. Unapata bakteria hawa kwa kufanya mapenzi na mpenzi ambaye ana magonjwa ya zinaa (STI). Kwa kawaida, STI ni kisonono au klamidia. Wakati mwingine mshiriki wako hana dalili zozote lakini bado anaweza kuwa na STI.
Dalili za ugonjwa wa kuchochewa kwa fupanyonga ni zipi?
Dalili za awali za PID ni pamoja na
Maumivu katika sehemu ya chini ya tumbo, ambayo yanaweza kuwa mabaya zaidi kwa upande mmoja kuliko mwingine
Kuvuja damu ukeni hali ambayo si sehemu ya hedhi yako ya kila mwezi
Vitu kutoka ukeni, ambavyo vinaweza kutoa harufu mbaya
Dalili za baadaye za PID ni pamoja na
Maumivu makali sana katika sehemu ya chini ya tumbo
Homa, kwa kawaida chini ya 102° F (38.9° C) lakini inaweza kwenda juu zaidi
Kuhisi mgonjwa kwenye tumbo lako au kutapika
Vitu kutoka ukeni vyenye rangi ya manjano-kijani au kama usaha
Uchungu wakati wa ngono au wakati wa kukojoa (kutoa mkojo)
Dalili ambazo hutokea kuelekea mwisho wa hedhi yako ya kila mwezi au katika siku chache baada ya hedhi yako kuisha zinaashiria uwepo wa PID. PID inaweza kuwa kali lakini isababishe dalili kiasi au kutokuwa na dalili.
Madaktari hutambuaje kama nina ugonjwa wa kuchochewa kwa fupanyonga?
Daktari atakuuliza maswali na kwa kawaida kufanya uchunguzi ya fupanyonga. Wakati wa uchunguzi wa fupanyonga, daktari wako huchunguza sehemu ya ndani ya uke wako kwa kuufungua akitumia kifaa kidogo kinachoitwa spekulumu. Daktari wako anaweza kuchukua sampuli ya majimaji kutoka kwa shingo ya kizazi kwa kutumia pamba ili kupima kisonono na klamidia au kuagiza kipimo cha damu. Daktari akifikiri kuwa unaweza kuwa na usaha au ujauzito kwenye mrija wako wa uzazi, kwa kawaida utafanyiwa kipimo cha ultrasound.
Ninawezaje kupunguza hatari yangu ya PID?
Huwezi kuzuia PID kila wakati. Lakini ili kupunguza hatari yako, fanya ngono na mpenzi mmoja tu, au tumia kondomu na dawa za kuua manii wakati wa ngono.
Hakimiliki © 2023 Merck & Co., Inc., Rahway, NJ, USA na washirika wake. Haki zote zimehifadhiwa.