Granuloma anulea ni nini?
Granuloma anulea ni athari za ngozi zisizo hatarishi ambazo husababisha uvimbe mdogo, imara ulioinuliwa kwenye ngozi. Uvimbe huunda kizingo chenye ngozi iliyodidimia kawaida au kidogo katikati ya kizingo.
Granuloma anulea huwapata zaidi wanawake
Unaweza kuwa na kizingo kimoja au vizingo vingi
Granuloma anulea mara nyingi hupona pasipo matibabu
Je, nini husababisha granuloma anulea?
Madaktari hawajui chanzo cha granuloma anulea. Inaweza kuwa ni athari ya mfumo wako wa kingamwili.
Zipi ni dalili za granuloma anulea?
Dalili hujumuisha uvimbe mdogo, imara ulioinuliwa ambao hutokea kwenye nyayo, miguu, mikono, au kidole chako katika umbo la kizingo. Uvimbe unaweza kuwa wa bluu, njano, au wenye rangi ya ngozi. Vinaweza kuwa laini.
Picha hii inaonyesha vizingo vyekundu vilivyoinuliwa kuzunguka eneo la katikati lililo wazi vinavyosababishwa na granyuloma anulea.
Picha kwa hisani ya Thomas Habif, MD.
Madaktari wanawezaje kujua ikiwa nina granuloma anulea?
Madaktari wanaweza kufahamu kuwa una granuloma anulea kwa kutazama ngozi yako. Ili kufahamu kwa hakika, madaktari wanaweza kuondoa kipande cha tishu kwa uchunguzi (kuchukua kipande kidogo cha ngozi ili kukichunguza kwenye hadubini).
Je, madaktari wanatibu vipi granuloma anulea?
Granuloma anulea mara nyingi hupona pasipo matibabu. Ikiwa inakupa wasiwasi, madaktari wataitibu kwa kutumia:
Malai ya kotikosteroidi au kuchoma sindano
Malai ya ngozi kwa ajili ya kutibu athari za kingamaradhi
Tiba ya mwanga na dawa za kufanya ngozi yako iathiriwe zaidi kwa mwanga
Dawa nyingine au tiba ya leza