Mfumo wa kingamwili ni mfumo wa ulinzi wa mwili wako. Inasaidia kukulinda dhidi ya magonjwa na maambukizi. Kazi ya mfumo wa kingamwili ni kushambulia vitu ambavyo si sehemu ya mwili wako, kama vile vijidudu, vimelea, na seli za saratani.
Tatizo la upungufu wa kinga mwilini ni nini?
Upungufu wa kinga mwilini inamaanisha mfumo wa kingamwili ambao ni dhaifu (upungufu). Watu wenye upungufu wa kinga mwilini wakati mwingine husemekana kuwa kingamwili yao imekandamizwa au hawana kinga.
Ukiwa na upungufu wa kinga mwilini, magonjwa yako yanaweza kudumu kwa muda mrefu kuliko ya watu wengine, na maambukizi madogo kwa watu wengine yanaweza kukufanya uwe mgonjwa sana.
Ukiwa na mfumo wa kingamwili ambao ni dhaifu, huna ulinzi wa kutosha dhidi ya maradhi na maambukizi
Utaumwa kila mara kuliko kawaida
Maambukizi ya kawaida yanaweza kuwa hatarishi zaidi, na unaweza kupata maambukizi yasiyo ya kawaida
Unaweza kuwa umezaliwa na upungufu wa kinga mwilini au ukaupata kutokana na maambukizi, ugonjwa, au matibabu ya kiafya
Ikiwa una upungufu wa kinga mwilini, utapaswa kufanya mambo ambayo yatakuepusha kupata maambukizi
Madaktari hutibu magonjwa yanayosababishwa na upungufu wa kinga mwilini kwa kutumia dawa za kuua bakteria, globulini ya kinga mwilini (kingamwili kutoka kwa damu ya watu wenye mfumo wa kingamwili wenye afya), na wakati mwingine seli shina (seli zinazokua na kuwa seli za damu, ikiwa ni pamoja na seli nyeupe za damu zinazopambana na maambukizi) upandikizaji kutoka kwa mtu mwenye afya njema.
Je, nini husababisha tatizo la upungufu wa kinga mwilini?
Tatizo la upungufu wa kinga mwilini unaweza kusababishwa na:
Kasoro ya kijenetiki ambayo umezaliwa nayo—japokuwa hii ni kwa nadra
Maambukizi kama vile VVU vya hatua ya mwisho
Saratani fulani, hasa saratani zinazoathiri uboho wa mifupa
Matibabu ya saratani kama vile tiba ya mionzi na baadhi ya tibakemikali
Dawa fulani
Dawa nyingi ambazo madaktari wanazitumia kuzuia uvimbe zinaweza kudhoofisha mfumo wako wa kingamwili. Dawa kama hizo zinaitwa dawa za kukandammiza kingamwili. Mfano ni steroidi (wakati mwingine pia huitwa glukokotikoidi au kotikosteroidi), kama vile prednisone. Wakati mwingine madaktari hukupatia dawa za kukandamiza kingamwili kwa sababu mfumo wako wa kingamwili unashambulia mwili wako (ugonjwa wa kingamwili kwenda kinyume na mwili).
Zipi ni dalili za tatzo la upungufu wa kinga mwilini?
Dalili zinajumuisha:
Kupata maambukizi ya kila mara, kama vile maambukizi ya sanasi, mkamba, nimonia, au maambukizi ya sikio
Ugonjwa wa kuvimba ndani kwa ndani mwilini (maambukizi ya ndani ya mdomo)
Vidonda vingi vya mdomoni
Kukosa hamu ya kula na kupungua uzani
Kwa mtoto mchanga au mtoto, kuhara kwa muda mrefu na kutokukua kama inavyotarajiwa (kushindwa kustawi)
Je, madaktari wanawezaje kujua ikiwa nina tatizo la upungufu wa kinga mwilini?
Madaktari hushuku uwepo wa tatizo la upungufu wa kinga mwilini ikiwa unaumwa mara kwa mara, magonjwa yako ni makali zaidi, au matibabu hayaleti matokeo ya kawaida. Kwa kawaida, madaktari hufanya yafuatayo:
Vipimo vya damu
Vipimo vya damu vinaweza kuonyesha idadi ndogo ya seli nyeupe za damu au viwango vya chini vya dutu zinazotengenezwa na mfumo wako wa kingamwili. Utafanyiwa kipimo cha VVU ikiwa una sababu hatarishi za kukufanya upate maambukizi ya VVU. Ikiwa mtoto wako ana dalili za ukosefu wa kinga mwilini madaktari wanaweza kumfanyia kipimo cha kijenetiki.
Kwa kutegemea dalili zako, madaktari wanaweza pia kufanya:
Vipimo vya ngozi ambavyo huonyesha jinsi mfumo wako wa kingamwili unavyofanya kazi
Uondoaji wa kipande cha tishu kutoka kwenye kifundo chochote cha limfu kilichovimba (tezi zilizovimba) au wakati mwingine kwenye uboho wa mifupa kwa ajli ya uchunguzi
Je, madaktari hutibu vipi matatizo ya upungufu wa kinga mwilini?
Madaktari hutibu tatizo hilo, kama vile saratani, kisukari, au maambukizi ya VVU, ambalo ndilo chanzo cha upungufu wa kinga mwilini. Matibabu yaliyofanikiwa mara nyingi huboresha mfumo wako wa kingamwili.
Iwapo dawa unayotumia inasababisha upungufu wa kinga mwilini, madaktari wanaweza kukupunguzia kipimo cha dawa au kukuzuia kuitumia. Madaktari watazingatia kiasi unachohitaji dawa na jinsi upungufu wa kinga mwilini ulivyo mbaya wanapoamua kama wapunguze au waache kutumia dawa.
Ikiwa upungufu wa kinga mwili umesababisha maambukizi, madaktari watakupatia:
Dawa za kuua bakteria
Globulini ya kingamaradhi (kingamwili kutoka kwenye damu ya watu wenye mfumo wa kingamwili wenye afya)
Ikiwa tatizo lako la upungufu wa kinga mwilini limesababishwa na tatizo la uboho wa mifupa, madaktari wanaweza kufanya:
Seli shina ni seli ambazo hukua na kuwa seli za damu, ikijumuisha seli nyeupe za damu ambazo hupambana na maambukizi. Madaktari wanaweza kupata seli shina kutoka kwa watu wenye afya njema na kukupa kwa njia ya IV (kupitia mshipa). Seli shina zinaweza kwenda kwenye uboho wako na kuanza kutengeneza seli nyeupe za damu zenye afya.
Je, ninawezaje kuzuia maambukizi ikiwa nina upungufu wa kinga mwilini?
Unapaswa kujaribu kuepuka maambukizi kwa:
Kuepuka kugusana na watu ambao wanaumwa
Kupata chanjo zote (sindano) zilizopendekezwa na daktari wako
Kujiepusha na vyakula vilivyopikwa kupita kiasi, au maji ambayo si safi
Ikiwa utaanza kuumwa, unapaswa kuwasiliana na daktari wako hata kama hali yako haionekani kuwa mbaya sana.