Je, Ugonjwa wa Akili ni Nini?

Je, ugonjwa wa akili ni nini?

Ugonjwa wa akili unajumuisha aina mbalimbali za matatizo ya fikira, hisia, na/au tabia.

Kuna aina nyingi za magonjwa ya akili, na yanaweza kudumu kwa mufa mfupi au muda mrefu.

Wakati mwingine inaweza kuwa vigumu kutofautisha ugonjwa wa akili na wasiwasi wa kawaida au huzuni, lakini ugonjwa wa akili ni mbaya zaidi, hudumu kwa muda mrefu, na huathiri kwa kiasi kikubwa uwezo wa mtu wa kukabiliana na maisha.

Karibu nusu ya watu wazima hupata dalili za ugonjwa wa akili wakati fulani. Mfadhaiko huwapata watu wengi.

Matibabu ya msingi ni dawa na ushauri nasaha. Familia, marafiki, na vikundi vya usaidizi pia vinaweza kusaidia watu kukailiana na ugonjwa wa akili.

Je, zipi ni aina za magonjwa ya akili?

Ugonjwa wa akili ni matatizo mengi tofauti.

Magonjwa haya yamegawanyika katika vikundi vikubwa, yakijumuisha magonjwa ya hali, wasiwasi (kama vile kuwa na uhuzuni sana au shauku sana), skizofrenia, matatizo ya haiba, na magonjwa ya haiba ya kutojizuia kurudia rudia matendo.

Magonjwa mengine ya afya ya akili yanajumuisha matatizo ya kula, magonjwa ya mfadhaiko (kama vile PTSD), na tabia ya kutaka kujiua.

Je, nini husababisha ugonjwa wa akili?

Ugonjwa wa akili bila shaka unasababishwa na mchanganyiko wa mambo mengi, ikiwa ni pamoja na sababu za kurithi, mifadhaiko ya kimaisha, mazingira na utamaduni unaoishi, na matatizo ya kiafya yanayoathiri ubongo wako.

Mawazo mengi, kama vile kupoteza kazi, talaka, au kutumia dawa nyingi, huongeza hatari ya kupata ugonjwa wa akili.

Matatizo fulani ya kiafya yanayoathiri ubongo wa mtoto, kama vile matatizo wakati wa kuzaliwa au ubongo kupata maambukizi ya virusi, huongeza hatari ya ugonjwa wa akili hapo baadaye maishani.

Ugonjwa wa akili hautokei kwa sababu mtu ni mvivu au mwenye kutokuwajibika. Sio kitu ambacho watu hufanya kwa makusudi.

Dalili za ugonjwa wa akili ni zipi?

Dalili ni tofauti kulingana na aina ya tatizo ulilo nalo.

Vinaweza kujumuisha

  • Mabadiliko makubwa ya sifa au tabia, haswa ikiwa yanatokea bila sababu dhahiri

  • Kuchanganyikiwa na kutowaza vyema

  • Mawazo ya ajabu, yasiyo na mpangilia, kama vile kuhama hama mada au kujibu maswali rahisi kwa majibu marefu, yenye kuchanganya

  • Tabia isiyofaa, kama vile kuvua nguo hadharani

  • Kuona au kuskia vitu ambavyo havipo

  • Kuamini mambo ambayo si ya kweli licha ya uwepo wa uthibitisho wenye nguvu unaoonyesha kunyume chake

  • Usununu mwingi

Je, madaktari wanawezaje kujua ikiwa mtu ana ugonjwa wa akili?

Madaktari hugundua ugonjwa wa akili kwa kuzungumza na mtu. Wakati mwingine pia huzungumza na walezi au wanafamilia.

Wakati mwingine dalili zinadhihirisha kuwa mtu ana ugonjwa wa akili. Kwa mfano, mtu kushikilia kuwa yeye ndiye rais au kwamba mawazo yake yanadhibitiwa na redio iliyopandikizwa kwenye ubongo wao.

Wakati mwingine ni vigumu kutofautisha ugonjwa wa akili na hali za kawaida. Kwa mfano, inaweza kuwa vigumu kutofautisha kati ya huzuni na mfadhaiko baada ya kifo cha mchumba au mtoto kwa sababu yote yanahusisha hali ya huzuni na kufadhaika.

Vivyo hivyo, kuna tofauti ndogo kati ya kuwa nadhifu au mwenye mpangilio mzuri na ugonjwa wa kushindwa kudhibiti mawazo na misukumo.

Utofauti wake kwa kawaida hutegemea kiwango cha ukubwa wa dalili, kiasi cha muda ambao dalili hudumu, na kiasi cha dalili kinachoathiri uwezo wa kufanya kazi.

Madaktari hutibuje ugonjwa wa akili?

Madaktari wamepiga hatua kubwa katika kutibu magonjwa ya akili kwa mafanikio.

Tiba kuu hujumuisha dawa na tiba ya kuzungumza. Kwa matatizo mengi ya afya ya akili, mchanganyiko unafaa zaidi kuliko kutumia njia moja pekee.

Matibabu mengine ni pamoja na tiba ya mshtuko wa umeme na uchangamshaji wa sumaku kupitia fuvu la kichwa.

Zamani, wenye ugonjwa wa akili mara nyingi waliwekwa katika taasisi au hospitali. Leo, watu wana uwezekano mkubwa wa kuishi kwa tija katika jamii, lakini watu wengi wenye ugonjwa wa akili bado hawapati huduma na usaidizi wanaohitaji.

Hakimiliki © 2023 Merck & Co., Inc., Rahway, NJ, USA na washirika wake. Haki zote zimehifadhiwa.