
Muhtasari kuhusu Saratani
Mwili wa binadamu una mamilioni ya seli zinazotofautiana kwa ukubwa, maumbo na majukumu. Seli ndizo kiini cha tishu zote tofauti ndani ya mwili. Kwenye tishu zenye afya bora, seli mpya huundwa wakati wa mgawanyiko wa seli, mchakati uitwao maitosisi. Seli zinapozeeka, "zinajiharibu zenyewe" na kufa, mchakato uitwao apotosisi. Uwiano maalum ni lazima uwepo kati ya kiwango ambacho seli mpya huundwa na kiwango ambacho seli za zamani hufa.
Saratani huanza uwiano huu unapokatizwa na seli kukua bila udhibiti. Ukatizaji huu unaweza kutokana na ukuaji wa seli bila udhibiti au seli kupoteza uwezo wa kujiharibu, hali inayosababisha bonge la seli, au uvimbe. Uvimbe tulivu, au usio na kansa, ni ukuaji usio na mpangilio maalumu wa seli zinazoonekana kuwa za kawaida. Seli hizi hupatikana mahali halisi pa ukuaji. Hata hivyo, seli mbaya (zenye saratani) zinaweza kuhama, au kueneza kansa, kwenye sehemu nyingine ya mwili kupitia mifumo ya usafirishaji wa damu au ya limfu, na kuunda uvimbe mpya kwenye sehemu hizi.
Saratani hupewa jina kulingana na mahali ilipoanza, ambapo hujulikana kama sehemu ya msingi. Saratani ya mapafu ikienea kwenye ubongo, uvimbe wa ubongo huchukuliwa kuwa ni saratani ya mapafu iliyoenea—wala si saratani ya ubongo. Uvimbe wa ubongo huchukuliwa kuwa ni sehemu ya ziada.