Watu wenye afya njema huishi kwa amani wakiwa na vijiumbe vingi vinavyojiweka kwenye au katika (kuishi) maeneo yasiyo na vijidudu mwilini, kama vile ngozi, pua, mdomo, koo, utumbo mpana, na uke. Vijiumbe ambavyo kwa kawaida hukaa katika eneo fulani la mwili huitwa vijiumbe wakazi. Seli za vijiumbe wakazi huzidi seli za mtu mwenyewe kwa idadi ya 10 hadi 1. Vijiumbe vinavyoishi kwa watu kwa saa nyingi hadi wiki lakini havikai kwa kudumu huitwa vijiumbe wa muda mfupi.
Vijiumbe wakazi katika kila eneo vinajumuisha aina kadhaa tofauti za vijiumbe. Baadhi ya maeneo kwa kawaida huishi aina mia kadhaa tofauti za vijiimbe. Sababu za kimazingira, kama vile lishe, matumizi ya viuavijasumu, hali ya usafi, uchafuzi wa hewa, na mazoea ya usafi, huathiri spishi zinazounda vijiumbe wakazi. Ikiwa wataathirika kwa muda (kwa mfano, kwa kuosha ngozi au kutumia viuavijasumu), vijiumbe wakazi hujirejesha wenyewe mara moja.
Badala ya kusababisha magonjwa, vijiumbe wakazi mara nyingi hulinda mwili dhidi ya viumbe vinavyosababisha magonjwa. Hata hivyo, katika hali fulani, vijiumbe ambavyo ni sehemu ya vijiumbe wakazi wa mtu huweza kusababisha magonjwa. Hali kama hizo ni pamoja na
Matumizi ya viuavijasumu
Jeraha au upasuaji
Mfumo dhaifu wa kinga (kama inavyotokea kwa watu walio na maambukizi ya VVU au saratani, watu wanaotumia dawa za kortikosteroidi, na wale wanaopokea tibakemikali ya saratani)
Wakati viuavijasumu vinavyotumika kutibu maambukizi vinaua sehemu kubwa ya aina fulani za bakteria wa vijiumbe wakazi, bakteria au kuvu wengine wakazi wanaweza kukua bila kudhibitiwa. Kwa mfano, ikiwa wanawake watatumia viuavijasumu kwa ajili ya maambukizi ya kibofu cha mkojo, viuavijasumu huua baadhi ya vijiumbe wakazi, na kuruhusu chachu kwenye uke kuongezeka na kusababisha maambukizi ya chachu kwenye uke.
Jeraha au wakati mwingine upasuaji unaweza kuruhusu vijiumbe wakazi kuingia katika maeneo ambayo hayapaswi kuwa na bakteria na kusababisha maambukizi. Kwa mfano, jeraha kwenye ngozi linaweza kuruhusu vijiumbe wakazi wa ngozi kusababisha maambukizi chini ya ngozi. Upasuaji kwenye utumbo mkubwa wakati mwingine huruhusu vijiumbe wakazi kwenye utumbo kuingia kwenye maeneo safi tumboni na kusababisha maambukizi makubwa sana.
(Angalia pia Muhtasari wa Ugonjwa wa Kuambukiza.)