Homa ya Lassa na homa ya kutokwa na damu ya Amerika Kusini inayosababishwa na virusi vya arena ni maambukizo ya virusi yanayosababisha kuvuja damu (kutokwa na damu) na viungo kutofanya kazi ipasavyo. Mara nyingi husababisha kifo.
Maambukizo haya huenea kutoka kwa wanyama wagugunaji hadi kwa watu, kwa kawaida watu wanapokula chakula kilichochafuliwa.
Dalili zinaweza kujumuisha homa, maumivu ya misuli, maumivu ya kichwa, kichefuchefu, kutapika, kikohozi na koo kuuma, pamoja na kutokwa na damu mdomoni, puani, au viungo vya ndani.
Ili kuthibitisha utambuzi, madaktari hufanya vipimo vya mkojo na damu.
Matibabu yanajumuisha kupewa maji pamoja na matibabu mengine yanayosaidia kudumisha utendaji kazi wa mwili.
Homa ya Lassa imetokea Nigeria, Liberia, Guinea, Togo, Benin, Ghana, na Sierra Leone. Homa ya kuvuja damu ya virusi vya arena ya Amerika Kusini hutokea Bolivia, Ajentina, Venezuela, na Brazili.
Husababishwa na virusi vya arena, maambukizo haya huenea kutoka kwa wanyama wagugunaji au mkojo au kinyesi chao hadi kwa watu, kwa kawaida wanapokula chakula kilichochafuliwa. Wanaweza kuenezwa kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine kupitia kugusana na viowevu vya mwili (kama vile mate, mkojo, kinyesi, au damu).
Dalili
Dalili za homa ya Lassa na homa ya kuvuja damu ya virusi vya arena ya Amerika Kusini kwa kawaida huanza siku 5 hadi 16 baada ya watu kuambukizwa virusi. Maambukizo haya husababisha homa, hisia ya jumla ya ugonjwa (unyonge), udhaifu, maumivu ya mwili yanayoenea, kuhara, na kutapika. Kwa siku 4 hadi 5 zinazofuata, maumivu ya kifua, koo kuuma, kikohozi, na kutapika vinaweza kutokea. Takribani asilimia 80 ya visa vya homa ya Lassa ni hafifu na mara nyingi havitambuliwi. Dalili ni kali kwa takribani asilimia 20 ya watu.
Ikiwa ni kali, homa ya Lassa inaweza kusababisha uvimbe usoni na shingoni, viowevu kujikusanya kwenye mapafu, kutokwa na damu mdomoni, puani, ukeni, au njia ya kumeng'enya chakula, na shinikizo la chini la damu. Takribani asilimia 20 hadi 30 ya watu wenye homa ya Lassa hupoteza uwezo wao wa kusikia. Kupoteza uwezo wa kusikia kunaweza kuwa kwa kudumu.
Kutokwa na damu mdomoni, puani, tumboni, na njia ya utumbo ni jambo la kawaida ukiwa na homa za kuvuja damu za Amerika Kusini. Kutokwa na damu dhahiri si jambo la kawaida sana ukiwa na homa ya Lassa, lakini wakati mwingine kuvuja damu hutokea kutokana na majeraha ya kutobolewa, fizi, au pua na chini ya ngozi (yanayoonekana kama madoa madogo ya zambarau). Kifo kinapotokea, kwa kawaida hutokana na mshtuko unaosababishwa na uvujaji mkubwa wa viowevu kutoka kwenye mishipa ya damu.
Kupona au kifo kwa kawaida hutokea siku 7 hadi 31 baada ya dalili kuanza. Takribani asilimia 15 hadi 20 ya watu ambao hulazwa hospitalini kutokana na homa kali ya Lassa hufa kutokana na ugonjwa huo.
Ugonjwa huo ni mkali wakati wa ujauzito, hasa katika miezi mitatu ya mwisho ya ujauzito. Wanawake wengi wajawazito walioambukizwa hupoteza kijusi.
Utambuzi wa Ugonjwa
Vipimo vya damu
Maambukizo haya hushukiwa wakati watu ambao huenda wameambukizwa virusi hivyo wana dalili maalum. Utambuzi wa homa ya Lassa au homa ya kuvuja damu ya Amerika Kusini huthibitishwa na vipimo vya damu ili kubaini virusi au kingamwili za virusi.
Matibabu
Huduma ya usaidizi, ikiwa ni pamoja na viowevu
Ribavirin
Matibabu ni huduma ya usaidizi, ambayo inajumuisha kuwekwa viowevu na elektroliti ikihitajika.
Dawa ya kuzuia virusi ya ribavirin haiponyi homa ya Lassa lakini hupunguza hatari ya kifo. Inaweza pia kuwa na manufaa kwa watu walio na homa ya kuvuja damu ya Amerika Kusini.
Kuzuia
Kutengwa kabisa kunahitajika ili kuzuia kuenea kwa wataalamu wa huduma za afya na wanafamilia. Wataalamu wa afya wako katika hatari kubwa ya kuambukizwa wanapowatibu wagonjwa waliolazwa hospitalini wenye homa ya Lassa na wanapaswa kuvaa vifaa vya kinga binafsi. Wakati wa mlipuko wa ugonjwa, kuwaweka karantini watu wenye dalili za maambukizo (homa na kuvuja damu) kumekuwa njia bora ya kudhibiti mlipuko wa maambukizo haya. Tahadhari huchukuliwa ili kuzuia kuenea kwa njia ya hewa.
Hakuna chanjo inayopatikana kwa homa ya Lassa.
Taarifa Zaidi
Nyenzo zifuatazo za lugha ya Kiingereza zinaweza kuwa muhimu. Tafadhali kumbuka kuwa Mwongozo hauwajibiki kwa maudhui ya rasilimali hizi
Shirika la Afya Duniani (WHO): Homa ya Lassa. Tarehe 5 Desemba, 2024.
Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC): Kuhusu Homa ya Lassa. Tarehe 31 Januari, 2025